-->

Kisa cha Aslay Kuachia Nyimbo Nyingi

ILINICHUKUA kama saa tano kuweza kukutana na Aslay. Mmoja ya waimbaji wanaokimbiza sana katika muziki wa kizazi kipya nchini.

Aslay

Saa nne zilipotea kwa kumsubiri na moja tu ndilo lililotumika kufanya naye mahojiano maalumu, bahati nzuri alikuwa muungwana kwa kutambua alinichomesha mahindi kwa muda na kuomba radhi. Ni wasanii wachache wanaobaini kosa kama hilo.

Aslay wa sasa sio yule Dogo Aslay wa Yamoto Band, huyu wa sasa yupo bize kinoma na hata kupata muda huo wa kupiga mbili tatu ni kama zali tu.

Mwanaspoti liliamua kumbana katika mahojiano na kufunga mengi, huku mengine akiyapotezea kwa kubaini yatamwanika sana hasa kwa mambo binafsi.

NYIMBO MFULULIZO

Aslay tangu aanze kutoa kazi kama ‘solo’, amekuwa na mtindo wa bandika bandua na mwenyewe anafunguka hasa alipoulizwa haogopi kuzimika mapema.

“Kwanza muziki mzuri haufi, lazima watu wajue na kingine nimeamua kuachia nyimbo mfululizo nikitaka kuwa na hazina kubwa ili hata nikipata shoo nisiwanyime burudani mashabiki wangu.

“Nitakuwa naangalia upepo ulivyo na kuendelea kutupia hewani, watu wasinichukulie poa na kuniona kama limbukeni wa kutoa kazi kila mara.”

Baada ya kuachana na Mkubwa Fella, Aslay anasema kwa sasa kazi zake anasimamiwa na Chambuso, mtu aliyekuwa naye tangu akiibukia Mkubwa na Wanawe na katika Yamoto Band. “Huyu ndiye meneja wangu kila kitu kuhusu muziki wangu na mambo mengine mbalimbali ndiye anasimamia, nashukuru anafanya kile nikipendacho,” anasema.

YAMOTO KUFA

Kuhusu kundi lao kufa Aslay anasema mwenye majibu yote ni Mkubwa Fella kwa vile yeye hawezi kusema wazi kama bendi imekufa ama la.

“Unajua suala la Yamoto nisikudanganye siwezi kusema chochote, anayepaswa kujibu ni Mkubwa Fella, ila kama tukiwezesha kurudi kufanya kazi sina tatizo, ila kwa sasa acha mambo yaendelee,” anasema. Kundi hilo lilikuwa linaundwa na wasanii wanne akiwamo yeye, Beka Flavour, Maromboso na Enock Bella, lililowahi kukimbiza ndani na nje ya nchi.

NJE YA KUNDI

Licha ya kutopenda kuelezea kuvunjika kwa kundi lao, lakini anasema kutoka kundini changamoto kubwa anayokumbana nayo kwa sasa ni kujaribu kutaka kupendwa na kila mtu jambo ambalo ni kazi, ila anajitahidi kuhakikisha mashabiki wengi wanamkubali na kufurahia kazi zake.

“Unajua ndani ya bendi mko wengi, hivyo chochote kikitokea wote kwa pamoja mnabeba msalaba, lakini peke yako kama hivi hasa unapojaribu kupendezesha watu changamoto huja sababu ni kazi.”

ISHU YA FLASHI

“Ni kweli nilipoteza flash yenye nyimbo zangu kibao, lakini ilikuwa muda sana japo niliogopa kazi zangu zisivuje, ila namshukuru Mungu haikuwa hivyo na hata madai natoa ili kuepuka kuingizwa mkenge sio kweli,” anasema. “Kuhusu kuendelea ama kuacha kuachia ngoma kama hivi, hiyo ndiyo fomula yangu ila nitakuwa naangalia upepo unaendaje ili wasinione mjinga pia.”

JUU YA NYIMBO KALI

“Napenda nyimbo zangu zote, lakini nadhani nyimbo ambazo nazisikiliza sana ni Rudi na Angekuona, nazipenda sana,”

“Mimi naona niko fresh hakuna kitendo kibaya nimewahi kufanya au labda kuna mtu nilimkosea mimi naona niko freshi na hivyo sina cha kujutia,” anasema Aslay ambaye anasema ana hazina kubwa ya kazi zinasubiriwa kuachiwa.

“Kwa sasa sifikirii kufanya kolabo lolote lakini sababu muziki nao kuna muda unaenda kwa upepo tunaweza kufikiria mbele.”

MISHEMISHE NYINGINE

Anasema hana mishe yoyote nyingine zaidi ya muziki, lakini anafichua yeye ni shabiki wa Simba na soka la kimataifa ni mnazi mkubwa wa Chelsea.

“Pia naipenda Real Madrid na ninavutiwa na Samatta, Didier Drogba japo amestaafu na Mata.”

SOKA MGUUNI

Aslay anasema kama sio muziki, angekuwa mwanasoka kwani kipaji cha soka anacho na anamudu nafasi zote za mbele.

“Kama sio muziki, ningebanana na Samatta uwanjani, napenda sana soka ila mzuka ulihamia huku baada ya kuonwa na Mkubwa,” anasema.

SHOO KALI

“Ilikuwa Uingereza, Yamoto tulienda kupiga shoo, watu walijaa sana siku ile. Sikuamini nilihisi kama nipo Bongo kumbe nipo nje, halafu ilitulipa sana,” anasema Aslay anayependa kula wali kwa njegere hasa vikipigwa kwa nazi.

MSHIKO MNENE

Aslay anafichua mtandao wa YouTube unalipa hasa kama video zake zikifikisha watazamaji milioni moja.

“Lazima niseme ukweli Youtube imenipa kipato, pili ni heshima sababu unajua kwanza kuna baadhi ya wasanii hawajawahi kufikisha watazamaji kwa idadi hiyo ndiyo maana najivunia na ninaomba mashabiki waendelee kuniunga mkono,” anasema Aslay ambaye ndoto zake ni kuja kumiliki lebo ya wasanii kama Diamond na kuwasaidia kama alivyoweza kusaidiwa yeye wakati akiibuliwa.

Mwanaspoti

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364