-->

Kitanda Changu Ndani ya Kaburi la Kanumba!

USIKU mtulivu. Kelele za mbu nje ya chandarua walionigasi kabla sijapitiwa na usingizi mnono, sizikumbuki na sasa niko kwenye ulimwengu mwingine kabisa.

Niko dunia ambayo ni vigumu kuieleza, lakini ninachokumbuka ni kwamba pembeni yangu alikuwepo mtu ambaye ametuachia pengo kubwa kwenye tasnia ya filamu, Steven Charles Meshack Kusekwa Ngamba Kanumba ‘The Great Pioneer’.

Amejiegemeza kwa pozi ambalo nashindwa kueleza kama amekaa, amelala au amejiegesha, lakini macho yake yote yako kwangu na tunatazamana kwa mshangao.

Mimi namshangaa kwa mengi, lakini yeye anashangaa namna ambavyo sibadiliki kwa maana ya kutonenepa, alivyoniacha ndivyo nilivyo na hapa chini ni mahojiano yangu na Kanumba, Jumatatu ya wiki hii:

Mimi: Kaka kwema? Huku ni wapi?

Kanumba: Salama, siwezi kukueleza huku ni wapi ingawa mimi najua umetoka wapi, mu-wazima huko?

Mimi: Safi lakini umetuacha na maumivu makali sana.

Kanumba: (kwa mshtuko wa wazi), maumivu kivipi?

Mimi: Kuondoka kwako wewe kama wewe lakini pia filamu hazina msisimko tena kama ilivyokuwa enzi za uwepo wako duniani.

Kanumba: Sikuelewi mdogo wangu. Filamu zimekuwaje tena?

Mimi: Ule ushindani ulioutengeneza na Ray haupo tena. Watu wamepunguza mapenzi na filamu za Kibongo na sasa akili zao zimetekwa na tamthiliya za Kikorea, Kifilipino, Kikanada na kwingineko, kifupi kama hali ni mbaya sana kwenye Bongo Muvi.

Kanumba: (akajiweka sawa na kukaa vyema), hebu fafanua vizuri, kwani Ray ameacha kuigiza? JB hayupo? Richie amekwenda wapi? Johari anaumwa? Gabo na Mlela wako likizo? Mainda kapatwa na nini? Kuna pia Hemed Suleiman ‘PHD’ na bila kusahau Uwoya na Rose Ndauka, imekuwaje na mbona sikuelewi?

Mimi: (huku nikishika vyema kalamu yangu), Wote hao wapo. Ray aliwahi kuniambia haoni tena wa kushindana naye ingawa anaamini wapo wanaojua kuigiza kuliko yeye. Aliniambia ushindani wenu ndani na nje ya filamu ulikuwa unampa mzuka wa kuandaa kazi nzuri akilenga kukupiku wewe lakini sasa hivi hakuna tena mtu wa kumfikirisha na kwamba uwepo wako ulikuwa kama mapacha, kifupi amekata tamaa kabisa.

Kanumba: Kwani tangu nimeondoka huko hajawahi kutoa filamu nyingine?

Mimi: (kwa sauti ya unyonge), tangu uondoke ametoa kazi nyingi tu, tena zingine ninazo kwenye begi langu ngoja nikupe (natoa CD za Ray kwenye begi langu), kuna hii Gate Keeper ndiyo ya hivi karibuni, kuna hii Too Much, tazama na hii Fan’s Death, shika na hii inaitwa Tajiri Mfupi, malizia na hii ya… (ananipokonya na kuziweka chini kwa hasira).

Kanumba: (Anainamisha uso na kupitisha vidole viwili kwenye paji la uso…) unajua mdogo wangu, wewe ni mwandishi na wakati niko huko ulikuwa unaandika ukweli ambao wengi ulikuwa unatuuma na nataka ukitoka huku ukaandike haya nitakayokueleza hapa tena bila kuacha neno hata moja, najua watakuchukia sana lakini ujumbe utakuwa umefika, sawa mdogo wangu?

Mimi: (naitika kwa kutingisha kichwa kutoka chini kwenda juu).

Kanumba: Tatizo moja la wasanii wa Filamu za Kibongo ni kuacha mstari wa sanaa na kujikita zaidi kwenye mambo mengine. Kama unakumbuka kuna wakati nilijiondoa kwenye kile kikundi chao cha Bongo Muvi, unajua ni kwa sababu gani nilifanya hivyo?

Mimi: Hapana. Nakusikiliza kaka.

Kanumba: Majungu, uongo, wivu na kuoneana wivu kwa mambo ya kijinga kabisa, samahani kwa kutumia lugha hii kali lakini inauma na ndiyo maana nimeamua kufunguka na niseme tu kwamba nimefurahi mno kukuona huku. (anaendelea)…

Wasanii hawapendani, usoni wanachekeana lakini mioyoni wamebeba chuki nzito. Yaani mdogo wangu, ulimi ni kiungo kidogo sana lakini kikitumika vibaya kinaweza kuang-amiza ulimwengu, unajua… (anainama tena na kugusisha kichwa kwenye goti la kulia na kisha kunitazama tena)

Mimi: Pole kaka, najua unaumia lakini jikaze, mmh!

Kanumba: (akipenga kidogo kuipa pua wepesi), ulimi ni kama njiti ya kiberiti, ni ndogo lakini inaweza kuunguza pori kubwa lenye ukubwa wa hekta nyingi. Wasanii wa Bongo muvi wako hivi, akikuta uongo fulani unazungumzwa kuhusu wewe, hata kama hajui chochote yeye anauchukua na kuueneza kwa mapana ambayo unabaki unashangaa. Hapa nataka nisistize, ni baadhi na siyo wote.

Mimi: Nini kifanyike ili filamu zetu ziendelee kubamba kama wakati wa uwepo wako?

Kanumba: Wasanii wawe makini na kazi zao, wapendane na wawe na mshikamano. Mfano sasa hivi nasikia kuna baadhi ya wasanii wanapiga kampeni ya uzalendo lakini kuna wengine hawaungi mkono na badala yake wanapika majungu pembeni, waambie Tanzania ni nyumba moja hivyo hakuna sababu ya kupigania fito.

Mwambie Ray aendelee kupambana zaidi, ana uwezo mkubwa na ikiwezekana aachane na wasambazaji ambao wanachukua hadi haki miliki ya kazi zetu, kama nilivyofanya mimi.

Nimeigiza filamu nyingi sana lakini sina hata moja ambayo ni mali yangu halali, naamini kuna wakati mama yangu kwa sasa anahangaika kwa baadhi ya mahitaji muhimu lakini kama filamu zangu zingekuwa mali zangu, angeendelea kuzifanyia chochote na kumuingizia kipato (anaendelea)

Mimi nimemaliza kwa leo, lakini kama ukija siku nyingine tutazungumza mambo mengi sana, wasalimie wote huko. Vipi, una muda nikupeleke kwa Rachel Haule na Adam Kuambiana? Hawako mbali sana na hapa nilipo, sema kila mtu yuko bize, nitawa-fikishia salamu zako kwamba ulikuwa hapa leo.

Mimi: Nakus-hukuru kaka.

Hata hivyo, wakati najiandaa kuondoka, ghafla nashtuka na kujikuta niko ndani kwangu na kugundua kwamba mazungumzo yangu na Kanumba ilikuwa ndoto lakini bahati ni moja, nakumbuka yote na ndiyo maana nimeweza kuyaanika hapa.

Maoni na ushauri; 0673 42 38 45.

BRIGHTON MASALU

Chanzo:GPL

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364