-->

NASA Wataka Odinga Atangazwe Rais

Muungano wa upinzani nchini Kenya, NASA, umeitaka Tume ya Uchaguzi nchini humo kumtangaza mgombea wake Raila Odinga kuwa mshindi wa Uchaguzi wa urais.

Mmoja wa kiongozi wa muungano huo Musalia Mudavadi amesema wana ushahidi kutoka ndani ya Tume ya Uchaguzi kuwa, Odinga amepata kura Milioni 8, huku mpinzani wake rais Uhuru Kenyatta akipata kura Milioni 7.

Kauli hiyo wameitoa wakati Tume ya Uchaguzi ikiendelea na zoezi la kuhakiki matokeo yaliyotumwa kupitia fomu 34 A na 34 B kutoka maeneo mbalimbali ya bunge na vituo vya kupigia kura.

Aidha, Mudavadi amesema, hawaridhiki na zoezi linaloendelea kuhakiki matokeo hayo ya urais na tayari wameiandikia barua Tume ya Uchaguzi.

Haya yanajiri baada ya NASA kudai kuwa mfumo wa kujumuisha matokeo ya Tume ya Uchaguzi ulidukuliwa, madai ambayo Tume imesema kulikuwa na jaribio hilo lakini halikufaulu.

Katika hatua nyingine, Ekuru Aukot amekuwa mgombea wa pili wa urais kujitokeza na kukubali kushindwa hata kabla ya matokeo ya mwisho kutangazwa. Japhet Kaluyu na Cyrus Jirongo pia wamekubali kushindwa.

Tume ya Uchaguzi nchini Kenya, IEBC imesema inatarajiwa kumtangaza mshindi wa Uchaguzi wa urais siku ya Ijumaa.

EATV.TV

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364