-->

Vigoma Dili, Lakini kwa Wema Hapana Aisee!

NANI alikuwa na uwezo wa kupinga ushindi wa Wema Sepetu mbele ya Jokate Mwegelo na Lisa Jensen, mwaka 2006 katika  jukwaa la Miss Tanzania? Hakuna na asingetokea sababu ilikuwa ni halali yake.

wema sepetu3332

Macho ya majaji yaling’amua uwezo wa kipekee uliobebwa ndani ya urembo wa Wema. Ndiyo maana magwiji kwenye tasnia ya filamu walimvuta na kumwingiza kwenye kiwanda hicho ili achochee ukuaji wa filamu nchini.

Anajitambua na kujielewa vilivyo ndiyo maana alipopata nafasi ya kushiriki kwenye tasnia ya filamu hakuficha kipaji alichopewa bure na Mungu wake; alikionyesha na kutoa nafasi kwa Watanzania kumpokea kama staa wa sinema za Kibongo.

WINGI WA MASHABIKI

Huwenda hufahamu ila Juma3tata linakujuza kuwa Wema mpaka sasa ana mtaji wa mashabiki zaidi ya milioni 2.2 kwenye mtandao wa Instagram, levo ambayo hakuna staa yeyote wa kike anayegusa, ukiacha ile ya Diamond Platnumz kwa mastaa wa kiume anayeongoza kwa kuwa na mashabiki milioni 2.8.

Bado una shaka juu ya ustaa na thamani ya Wema Sepetu, mlimbwende mwenye vipaji lukuki? Lakini kumbuka kuwa, hapo  bado kuna wale mashabiki ambao hawapo kwenye mtandao huo.

NI LEVO ZA KIM KARDASHIAN

Unyamwezini kuna mastaa wengi wa kike wenye mvuto ila unapotaka kumlinganisha Wema na mastaa wanaosumbua ulimwenguni hivi sasa moja kwa moja utamfikiria Kim Kardashian, mke wa Kanye West na mama wa Saint na North.

Off-course Wema ni kama Kim Kardashian wa Bongo, urembo wake ndiyo utajiri wake hasa akipata mtu anayeweza kumshika mkono na kumwonyesha fursa nyingi alizozikalia, zinazowindwa na mastaa wenzake wa kike wanaotamani thamani yake  ingekuwa ndani yao.

DILI ZINAMPITA, ANATAMBUA ANAPOKWENDA?

Mastaa mbalimbali wamekuwa wakiingizia mkwanja nje ya kazi zao, kuna mirabaha na mikataba minono ambayo nyota hao huingia na kampuni kubwa ili majina ya mastaa hao yatumike kunadi bidhaa zao.

Licha ya urembo wote wa Wema ni nadra kuonekana kwenye matangazo ya kampuni nyingi. Urembo na sifa anazo ila kipi kinafanya urembo wake usiwe dili, hilo mimi na wewe tunaweza tusifahamu ingawa kuna kitu mrembo huyu anakipoteza.

Unajua urembo una mwanzo na tamati. Ni kama mawio na machweo ya jua, hali kadhalika umri unavyozidi kwenda ndiyo urembo na thamani ya kitu kizuri inavyotoweka, itakuwaje kwa Wema baada ya miaka kadhaa?

Ukizingatia kizazi hiki kimebarikiwa na kinatoa warembo wenye viwango vinavyokidhi soko la utandawazi kila leo. Hapo bila kupepesa macho ni lazima Wema acheze vyema na muda, huu ndiyo wakati wake wa kutengeneza fedha, kuwekeza ila hapo machweo yakitimba awe tayari ameseto.

MJASIRIAMALI WA KWELI

Kama nilivyochombeza hapo awali kuwa Wema ana akili mno, hakuacha ustaa wake uishie kwenye mitandao ya kijamii ndiyo maana akaamua kama wewe ni shabiki yake wa kike basi zile lipstick uzinunue, uzitumie na upendeze kama yeye.

Hakuishia hapo, Wema amejiongeza mno, akaingia ubia na kampuni flani ya simu ili kama wewe ni shabiki na unataka upate habari zake basi kuna namba fulani unazibofya na unakuwa unapata habari zake kila siku.

Akaona haitoshi akabuni sendoz, ndala, malapa yenye logo yake ili iwe burudani murua kwako wewe shabiki wake wa damu.

USHAURI KWA WEMA

Hivi sasa Wema amejiingiza kwenye uaandaaji wa maonyesho ya ngoma za uswahilini maarufu kama vigoma vinavyonogeshwa na muziki wa Singeli.

Ni wazi muziki huo umelikamata jiji. Ni habari ya mjini na unatoa pesa nyingi kwa wasanii na waandaaji wa vigoma hivyo. Hadhi ya Wema ni kubwa mno, haifanani na vigoma, kwa kifupi vigoma siyo saizi yake hata kama vina fedha kiasi gani.

Wema Sepetu ni ‘brand’ inayojiuza yenyewe endapo ikikutana na washauri wazuri ambao wataweza kuzishauri kampuni na taasisi mbalimbali kuwekeza fedha zao kwake, naamini wakifanya hivyo lazima majibu chanya yatapatikana kwenye biashara ya kampuni hizo.

Vigoma siyo saizi ya Wema, vigoma vinampwaya na kuishusha thamani yake. Kuna kazi ambazo hadhi yako inakukataza kuzifanya, moja wapo ya kazi hizo ni vigoma, ila ukicheka vyema na fursa za ukubwa wa jina lako hakika unaweza kuwa mrembo tajiri hata pale machweo ya uzuri wako yatakapowadia.

Mtanzania

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364