-->

Siku ya Kucheza Muziki wa Nyumbani Yatafutwa

Dar es Salaam. Serikali imesema itafanya mazungumzo na viongozi wa muziki kujadili kuwa na siku maalumu ya muziki wa nyumbani.

Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe

Hayo yamesemwa na Waziri wa Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo Dk Harrison Mwakyembe alipokuwa akizungumza na waimbaji wa muziki wa injili ikiwa ni mwendelezo wa ziara yake ya kukutana na vikundi mbalimbali vya sanaa.

Amesema katika kuhakikisha muziki wa nyumbani unakuwa na thamani, kuna haja ya kuupa nafasi zaidi kwa kuutengea siku maalumu.

“Nitakaa na rais wa Shirikisho la muziki nchini Ado November tuangalie ni siku gani itakuwa mahususi kucheza muziki wa nyumbani katika vyombo vyote vya habari, ”amesema Dk Mwakyembe.

Katika hatua nyingine Dk Mwakyembe amesema kuwa changamoto za wasanii zinatatulika na zina majibu yasiyohitaji fedha zaidi ya uamuzi.

Amesisitiza kuwa asilimia 90 ya kero zao zinatatulika , ila na wao wanatakiwa kubadili mtizamo wao na kuamini inawezekana.

“Nimeshakutana na wasanii wa filamu, muziki na ilikuwa nikutane na wanamuziki wa dansi, lakini ninakwenda kwenye shughuli za Shirikisho la soka nchini (TFF), zinazofanyika kesho Dodoma.

“Nitakutana nao wiki ijayo, waniambie changamoto zao, na tunajadili jinsi ya kuzitatua, hakuna maendeleo ya muziki bila kuihusisha Serikali, kwa sababu ndiyo inabadili sheria na haiwezekani kubadilishwa studio, ” amesema.

Amesema atasimamia haki za wasanii hadi kufikia mwisho wa mwaka huu ziwe zimepungua kwa asilimia kubwa na inawezekana kuondokana na upuuzi huo.

Ameeleza wenye fedha wanawagawa wasanii kipuuzi , “Nawaambia mlinzi wa kwanza wa kazi zao ni wao wenyewe wasanii, mezani kwangu nina mafaili ya wao kwa wao kukubaliana kulipwa na wengine wakikataa.

Kwa upande wa mwimbaji Christina Shusho amesema kitendo cha viongozi katika ngazi ya juu kama waziri kujitokeza na kuzungumza na wasanii na kusikia kero zao kinamaanisha kuna mwanga mbele ya safari.

Kwa upande wa mwimbaji Emmanuel Mgaya (Masanja Mkandamizaji) amemwambia Dk Mwakyembe afuatilie ilipo studio iliyotolewa kwa ajili ya wasanii.

“Kulikuwa na studio iliyotolewa kwa ajili ya wasanii, sidhani kama kuna mwimbaji hata mmoja humu ndani aliyewahi kurekodia huko, Waziri tunaomba angalau na sisi tujidai kwa sababu ilitolewa kwa wasanii wote, ” amesema Mgaya.

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364