Crazy GK Sina Mpango Na Diva… Ni Mpenzi Wangu Tu!
UNAIKUMBUKA East Coast Team chini ya kiongozi wao Gwamaka Kaihula a.k.a King Crazy GK? Enzi za Ama Zangu, Ama Zao utawataka?
Kule alisimama Mwana FA, pale AY, usiwasahau O Ten, Snare, Buff G na wengine kibao kutoka maskani yao Upanga Mashariki.
Kundi hili ambalo lilitesa zaidi miaka ya 2000 wakichuana vikali na Kundi la TMK Wanaume lilisambaratika baadaye baada ya wasanii wake kuamua kufanya kazi zao binafsi nje ya kundi huku wengine wakiamua kwenda shule kupiga kitabu.
You know what? Rais wa East Coast Team, King Crazy GK ameibuka na kutema cheche kuhusiana na ujio mpya wa kundi hilo.
Katika interview na Polisi wa Swaggaz iliyofanyika juzi jijini Dar es Salaam, GK alifunguka mengi, lakini baada ya kudodoswa na mwandishi wetu alifunguka pia kuhusiana na uhusiano wake.
Kwanza alizungumzia uhusiano wake na mtangazaji nyota wa Radio Clouds FM ya jijini Dar es Salaam, Loveness Malinzi ‘Diva’ ambapo alisema kwa sasa hana mpango wowote na mpenzi wake huyo zaidi ya kuwa wapenzi tu, baasi.
“Sina mpango naye wowote ule zaidi ya kuwa mpenzi wangu tu. Hakuna zaidi ya hivyo,” alisema GK.
SWAGGAZ: Lakini nimesikia kuwa mpo karibu kufunga ndoa?
Crazy GK: Siyo kweli kwa sababu mimi sijatangaza habari hizo na bado hata sijamvalisha pete… Diva ni mpenzi na siyo mchumba wangu naomba tuelewane.
SWAGGAZ: Mbona mpenzi wako anaitumia vibaya mitandao ya kijamii kwa kutuma picha ambazo hazina maadili ya Kitanzania?
Crazy GK: Kila mtu na uhuru wa kutumia mitandao vile apendavyo yeye na kuhusu picha anazotuma ni maamuzi yake na mimi sioni ubaya au tatizo lolote.
SWAGGAZ: Lakini vipi kuhusu kufunga ndoa, maana naona umri unakwenda kiongozi.
Crazy GK: Jibu langu ni moja tu, bado niponipo sana, sijawaza kuoa kwa sasa.
SWAGGAZ: Hebu tugeukie sasa muziki. Ilisemekana East Coast imekufa, lakini wewe umeibuka na kusema kuwa kundi bado lipo hai na mpo mbioni kuibuka na cheche za muziki, imekaaje hiyo?
Crazy GK: East Coast ni kampuni ambayo inatengeneza fedha hadi leo hii, ingawa wasanii wa kundi hilo tulitengana kutokana na majukumu ya hapa na pale, baadhi yetu tulikwenda shule kusoma na wengine walikuwa na majukumu yao ya kifamilia.
East Coast haijawahi kufa kwani bado inafanya kazi zake kama kawaida na kuna kazi ambazo zipo njiani zinakuja, zilizofanywa na wasanii wetu. Pia kuna wasanii wapya ambao siku si nyingi tutawatambulisha.
SWAGGAZ: Kwa nini unasema East Coast sio kundi kama Watanzania tulivyokuwa tumezoea kuliita na kusema ni kampuni?
Crazy GK: East Coast ni kampuni inayofanya kazi mbalimbali kama kukuza vipaji vipya vya wasanii wanaochipukia katika tasnia na kutoa ushauri ili kuzidi kukuza muziki wetu wa Tanzania.
SWAGGAZ: Watanzania wategemee nini kutoka kwa kampuni yenu?
Crazy GK: Wategemee kazi ambayo ipo jikoni iliyofanywa na wasanii wa zamani wa kampuni hii.
SWAGGAZ: Wimbo wako mpya wa ‘Mzuri Pesa’ unamaanisha nini hasa?
Crazy GK: Mzuri Pesa ni wimbo ambao unaeleza kuwa pesa ndiyo kila kitu katika maisha ya sasa, bila ya kuwa na pesa huwezi kufanya lolote au unaweza kusema kuwa mzuri pesa, urembo na ubishoo ni mapambo ya pesa.
SWAGGAZ: Mwisho kabisa… ukipanda jukwanii kwa ajili ya shoo, unavuta mkwanja kiasi gani?
Crazy GK: Sifanyi shoo ya chini ya Tsh. Milioni 30. Hiyo ndiyo pesa ninayolipwa mara nyingi.
SWAGGAZ: Mbona kama ni pesa nyingi sana?
Crazy GK: Hata kazi yangu ninayoifanya nikiwa jukwaani si ya kitoto, lakini mbona wasanii wa nje ya nchi wakija kufanya shoo hapa nyumbani wanalipwa zaidi ya fedha hizo? Wapo wanavuta hadi Tsh. Milioni 100, sasa msanii wa ndani nikilipwa hizo 30 kuna tatizo gani?
Mtanzania