-->

Kwaheri mwaka 2017 karibu 2018

MWAKA 2017 ulikuwa mpya, sasa umekatika tukisubiria mwaka mwingine mpya 2018 zikiwa zimebaki siku nne tasnia ya filamu kama ilivyo sekta nyingine ambazo zilikuwa na matukio ya kukumbukwa na kuagwa kwa kuukaribisha mwaka 2018 kwa matukio mapya katika ukuzaji wa tasnia ya filamu Swahilihood kwa waliojifunza wamejifunza na wale waliopoteza ni vema kujipanga kwa mwaka 2018.

Kulikuwa na mengi yaliyotokea si rahisi kuyaandika yote kwani muda hautatosha na kuyamaliza, bali tutaweza kuandika baadhi yake tu ili kujikumbusha na kuwa nafasi ya kuanza mwaka 2018 kwa matumaini na nguvu mpya kama ilivyozoeleka kwa wengi.

SOKO

Soko la filamu limeshuka sana kama si kupotea huku lawama zikiwa ni kutokana na uzalishwaji na uingizwaji wa tamthiliya kutoka nchi kama za Ufilipino, India, Korea na sehemu nyinginezo tena zikiwa zimetafsriwa kwa Lugha ya Kiswahili na kuziua filamu za ndani kilio ambacho kimekuwa kikubwa.

Kufuatia sakata hilo mamlaka ya mapato Tanzania (TRA) hivi karibuni iliendesha oparesheni kwa kushirikiana na Alex Msama katika kuwakamata wale waliokuwa wakiuza sinema bila kuweka stempu bila kujali zinatoka nje au ndani zoezi hilo limefanikiwa kwani nao sasa wanaweka stempu kazi za nje.

Kwa wauzaji wa filamu za nje kupata fursa ya kupata stempu na kuwa ni bidhaa halali hapo hali ya soko kwetu inakuwa ngumu zaidi kwani wasanii wenyewe wanakubali kuwa kazi za nje zina ubora kuliko za ndani kuanzia matayarisho na hata maudhui. Watengenezaji wamefanikiwa na kuwa na kazi bora zaidi.

WASANII NA SIASA

Ikiwa hali ya upepo wa kisiasa haujatulia wasanii nao wamejikuta wakiwa ni sehemu ya kuyumba katika uamuzi wao, pale Wema Sepetu ‘Madam’ akitangaza kurudi CCM akitokea Chadema alikohamia akiwa na kesi yake ya matumizi ya madawa ya kulevya. Kupitia mitandao ya kijamii na mmoja wa kiongozi wa chama hicho akipinga njia hiyo.

Huku tasnia ya filamu ikihitaji njia zaidi ya kujinasua na kufikisha ndoto za wadau wake kupitia umoja wao naye Rais wa Shirikisho la Filamu (TAFF), Simon Mwakifwamba anajiingiza kwenye siasa na kuibuka mshindi nafasi ya Katibu Mwenezi Mkoa wa Dar es Salaam.

NDOA

Mwaka huu si haba kwa wasanii wa filamu walipata bahati ya kufunga ndoa zao aliyefungua dimba alikuwa ni Irene Uwoya akiolewa na kijana mdogo kabisa wa muziki wa kizazi kipya, Dogo Janja ingawaje hadi leo kuna sintofahamu kama wasanii hao ndoa yao ni kweli au la, lakini bado wapo pamoja.

Mwanadada machachari katika sanaa Zuwena Mohamed ‘Shilole’ naye hakuwa nyuma pale alipofanikisha ndoa yake na mpenzi wake, Asharaf Uchebe, baada ya uhusiano wao kuvuma katika mitandao ya kijamii na kuwa tetesi kuwa Shilole ataolewa baada ya kuachana Nuh Mziwanda.

HARAKATI ZA SOKO LA FILAMU

Mwaka huu kuliibuka harakati mbalimbali wasanii na wadau wakijaribu kupigania hali ya soko la filamu za ndani, lakini hali ni tete kwani tangu Waziri Nape Nnauye aondoke mwaka uliopita filamu za nje zimeendelea kushika soko na kuzifanya filamu za ndani kusuasua sokoni, jambo ambalo limewafanya wasanii wengine kuzimika.

Hivi sasa soko limekwama kwani wasambazaji wa filamu za nje nao wameingia katika ulipaji wa kodi jambo linalowafanya wawe wauzaji rasmi kwani nao wamepewa stempu za TRA na kuwa ni kazi halali kuuzwa, kitu ambacho awali hakikuwepo.

Kitu cha msingi ni kwa wasanii wa ndani sasa kujipanga na kutoa kazi ambazo zinaweza kuishawishi jamii kuamini kazi za ndani na kuachana na zile za nje. Hiyo siyo kazi ngumu kama kweli wasanii hao wanataka kupigania soko lao na kuendelea kutawala katika kazi hiyo.

Wasambazaji wa ndani wanajaribu kujipanga kwa mwaka 2018 kuja na njia mpya ambayo ni kutengeneza katika ubora wa juu na kuwafikia wanunuzi walipo pengine ndio itakuwa mbinu ya kuua soko la kazi za nje kutoka Korea na Ulaya.

Kuna wale wenye imani kuwa soko la filamu linarudi kwani wamegundua moja ya sababu kuwa makini katika utengenezaji wa filamu kwani matatizo yaliyokuwepo awali hayatakuwepo tena watatengeneza sinema nzuri zenye uhalisia na kushindana na kazi za nje.

MATATIZO KESI

Matatizo yaliyoikumba tasnia ya filamu mwaka 2017 ni mengi mbali na nyota wa Bongo, Wema kuhusishwa na utumiaji wa madawa ya kulevya na kufunguliwa kesi ambayo hadi leo hii haijaisha, kwa upande mwingine, Nyota wa tasnia hiyo, Elizabeth Michael Lulu mambo hayakwenda sawa pale kesi yake ilipochukua sura mpya baada ya kusikilizwa kwa muda kidogo kisha kutolewa hukumu ya kesi ya kuua bila kukusudia iliyomtia hatiani na kufungwa kifungo cha miaka miwili jela.

Lulu anaacha simanzi kwa wapenzi wa kazi zake kutokana na kesi iliyomhusisha na kifo cha nguli wa uigizaji katika tasnia ya Filamu Bongo Steven Kanumba, hilo lilikuwa ni tukio la kushtua kwa wadau wa filamu Bongo, pia mwaka huu mwigizaji wa kimataifa Ramsey Noah alifika katika kaburi la msanii huyu na kuhani.

UZINDUZI

kwa mwaka huu uzinduzi wa filamu umechukua kasi, pale ambapo hata majina yamekuwa yakibadilika kama tulivyozoea katika uzinduzi, wasanii wakipita katika zuria Jekundu (Red Carpet) lakini wasanii wetu wamekuwa wakipita katika Zuria la Dhahabu na kuitwa (Golden Carpet).

Pamoja na ubunifu huo lakini hali imekuwa tofauti sana kwa mfumo huu ambao kwa wenzetu mara nyingi hufanya Premiere siku moja kabla ya sinema kuingia katika majumba ya sinema kama ni njia ya kufungua onyesho rasmi na kuendelea kuonyeshwa sinema katika majumba ya sinema.

Kuna jambo la kujifunza mwaka 2018 kwa kuhakikishia filamu zetu haziishii kuruka tu katika majumba ya sinema kisha kurudi katika Dvd au kukaa nazo ndani tu bila kuisambaza kwa watazamaji, mwaka huu watayarishaji watajipanga.

Mwaka 2017 tumeumaliza salama na tujipange kwa ajili ya mwaka 2018 tukiwana afya furaha kwa ajili ya kufanya vizuri na kuikuza tasania ya filamu Swahilihood.

Mungu Ibariki Tanzania, Mungu Ibariki Afrika.

Chanzo:Mwanaspoti

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364