Mpoto Atoa Dili Tano kwa Vijana Wasio na Mtaji
Msanii wa mashairi na kughani Mrisho Mpoto ametoa somo kwa vijana wa watanzania kwa kuwapa njia mbalimbali ambazo zinaweza kuwafanya kujikwamua kiuchumi endapo watazitumia kuanzisha biashara ya kutumia mtaji mdogo au bila ya kuwa na mtaji kabisa.
Mrisho Mpoto ametumia ukurasa wake wa facebook kutoa fursa tano ambazo anaona kama vijana watazitumia zinaweza kuwa na tija katika maisha yao.
Biashara hizo alizozitaja Mpoto ni kama ifuatavyo:_
“1. Toa huduma.
Kama huna mtaji wa fedha, basi nina uhakika una mtaji wa muda. Sasa tumia muda wako kutoa huduma ambayo wengine wanaihitaji. Toa huduma kulingana na utaalamu wako, uzoefu wako au ujuzi ulionao. Angalia ni namna gani unaweza kutumia muda wako kuongeza thamani zaidi kwenye maisha ya wengine.
Kwa mfano kama wewe ni mwalimu, basi unaweza kutenga muda wako wa ziada kutoa huduma ya kufundisha watoto shuleni au hata majumbani mwao. Kama wewe unaweza kufanya kitu fulani, basi tafuta wenye uhitaji wa kitu hiko na wasaidie kwa muda ulionao. Unaweza kuwasaidia watu kwa kazi zao za nguvu au hata kazi zao za kitaalamu. Unaweza kuwasaidia watu wanaofanya tafiti mbalimbali kwa muda wako na utaalamu wako kwenye tafiti.
2. Biashara ya mtandao (network marketing).
Najua wengi mkisikia hii huwa mnakunja sura na kuona kama mnapotezwa. Bado naendelea kusisitiza kama unataka kuingia kwenye biashara na hujui wapi uanzie, basi ingia kwenye biashara ya mtandao. Hii ni biashara ambapo unatumia bidhaa au huduma fulani, kisha unawashawishi wengine nao watumie na unalipwa kamisheni kwa manunuzi wanayofanya.
3. Biashara ya taarifa na maarifa.
Unaweza kuingia kwenye biashara ya kutoa taarifa na maarifa. Kwa dunia ya sasa ambapo watu wengi wanatumia mtandao wa intaneti, unaweza kutumia mtandao huu kutoa taarifa na maarifa na kuweza kutengeneza kipato.
4. Kilimo biashara.
Kuna fursa kubwa sana kwenye kilimo cha kibiashara, hasa kwa kilimo cha muda mfupi cha mboga mboga na matunda. Kilimo hiki unaweza kuingia kwa mtaji kidogo na kama una muda wa kutosha kukifuatilia kwa makini basi unaweza kuanza kidogo na kukua kadiri muda unavyokwenda. Angalia kilimo kipi unaweza kuanza nacho na ukaribu wako ili uweze kupata matokeo mazuri.
5. Biashara yoyote unayotaka kuanza, ila anza kidogo.
Unaweza kuanza biashara yoyote unayopenda kuanza, hata kama ina uhitaji wa mtaji mkubwa, wewe anza kidogo. Anza kwa hatua ya chini kabisa, weka juhudi kubwa na endelea kuikuza.
Ukishaanza kuona matokeo mazuri, yaani faida kwa hatua hiyo ndogo unayopiga, ni rahisi kuwakaribisha watu wengine na wakakuchangia mtaji. Au hata kwenda kwenye taasisi za kifedha na kuchukua mkopo.”
Hiyo ni kwa mujibu wa Mrisho Mpoto