NDANI YA BOKSI: Shoo ya Milioni 10, Shingoni Cheni ya Milioni 100!
Hasira. Inatia hasira. Kuchukuliana poa poa maisha haya. Jay Z ni mtoto wa maskini tu, aliyelelewa na mama. Atake asitake ni mtoto wa maskini. Aliyekulia sehemu za kipumbavu. Kipuuzi na kila aina ya ushenzi. Wendawazimu uliotopea.
Ila binti yake Blue Ivy, atabaki kuwa mtoto wa tajiri na atakufa akijulikana kama mtoto wa tajiri.
Jay Z kabla ya kuingia kwenye muziki aliuza sana unga. Huu unga ambao hapa katikati ulivuruga nchi.
Aliingia kwenye muziki akiwa tayari akaunti yake inasoma pesa nyingi sana. Zaidi ya dola milioni 3. Muziki ukatunisha zaidi akaunti. Akili yake ikamuweka pale alipo. Mpaka kuingia kwenye biashara ya unga ni kutokana na maisha mabovu aliyokulia. Akawa na hasira na pesa. Mungu akamuongoza na kuingia kwenye muziki na kuachana na mchongo wa kuua vijana wenzake kwa unga.
Diamond Platinumz wetu ambaye aliuza mpaka mitumba, lakini hakupata pesa, akaamua kujiingiza kwenye muziki ili apate unafuu wa maisha.
Naye kakulia kwenye umaskini kama vijana wengi ambao muziki au soka limekuwa kimbilio lao.
Kaingia kwenye muziki akiwa hana kitu tofauti na Jay Z. Hivi sasa unapoongelea Diamond Platinumz, ni kijana mdogo mwenye pesa ya kufanya afanye analotaka kwenye maisha yake katika uso wa dunia hii.
Mungu kamjaalia. ‘Of coz’ bidii yake na kujielewa ni vyanzo na sababu ya kipato chake. Kuna kitu kimoja tuwekane sawa hapa. Muziki wa sasa hivi dunia nzima, kutokana na utandawazi una maisha mafupi kuliko funza.
Pesa ya muziki kama ya soka ukishindwa kuwekeza unapokuwa kwenye chati, siku si nyingi utachekwa na hawa wanaokuzunguka kwa sasa kama mfalme. Unapopata nafasi ya kupenya na kupiga pesa. Piga pesa kila inayokatiza mbele yako. Fanya muziki ukiwa na akili ya Mangi Mchaga wa Kibosho kwenye hela.
Kusanya fedha zote kuliko serikali ya Magufuli. Huku ukilinda heshima yako. Usiichekee pesa hata sekunde. Kamata.
Angalia wanamuziki wote wa kimataifa waliokuja kutumbuiza hapa Bongo. Ni wale ambao wanapatikana kirahisi. Kwa bei nafuu. Ndo maana humuoni Justin Bieber akija. Beyonce wala Rihanna.
Kwa sababu hao na wengineo wapo ila hawapatikani kirahisi. Jay Z alikuja Bongo miaka kumi iliyopita. Eleweni nyie kizazi cha Kikwete. Jay Z hakuja kufanya shoo. Ni kama Diamond apelekwe na Tamwa au Tasaf huko Mbamba Bay, kwenye shughuli ya kijamii halafu jamii ya huko imbembeleze atumbuize kidogo.
Jay Z alikuja kwa suala tofauti na muziki. Ndiyo maana hata shoo yake ilikuwa na ‘complimentary’ nyingi zaidi kupata kutokea.
Ingetangazwa kuwa ni bure usalama ungekuwa mdogo. Ndiyo maana kiingilio kilikuwa kidogo na ‘complimentary’ zikawa nyingi kuliko taksi za Dar es Salaam.
Mwanamuziki ambaye yuko juu ndani ya Amerika huwezi kumleta aje kushika maiki na kulala kwenye hotel za Dar es Salaam kirahisi rahisi atumbuize jukwaa moja na Man Fongo na Snura. Haiwezekani.
Kwa sababu wanakuwa na ratiba ngumu na ya fedha nyingi huko huko kwao Marekani.
Msanii ambaye yuko juu ndani ya Amerika hakamatiki kirahisi hata kwenye nchi za Ulaya. Kwa sababu Marekani yenyewe inajitegemea kwa kila kitu. Li nchi kubwa kama bara la Afrika. Kuna Tanzania 50 ndani yake. Dar es Salaam kama elfu tatu. Mpaka amalizane na Wamarekani wenzake siyo leo. Asikudanganye mtu.
Wengi wa wanamuziki wanaokuja Bongo wanakuwa wamekata ‘ringi’ kwao inakuwa rahisi kuja kuambulia chochote Afrika. Kutokana na muziki kuwa na maisha mafupi. Baadhi ya wanamuziki wameamua kujikita kwenye shughuli za filamu. 50 Cent na Ice Cube ni miongoni mwao.
Wanaendelea kupiga hela huko Hollywood. Muziki umekuwa bidhaa ya Kichina. Haudumu. Ukiwa juu piga hela kama vile kesho unakufa. Piga pesa. Kusanya pesa. Kisha itunze mpaka ishike adabu. Usicheke na kima utachekwa wewe keshokutwa.
Ukitambua kuwa umetoka kwenye umasikini, kuwa na adabu na kila senti inayoingia mfukoni. Unaweza kuwa siyo mtu wa club. Siyo mlevi wala mpenda starehe za kidunia. Lakini, ukawa na udhaifu fulani ambao unateketeza pesa katika daraja lile lile la mlevi au zaidi. Kama mzinzi na mpenda anasa za kila aina.
Kama mambo ambayo mtoto wa maskini unatakiwa kuyakwepa ili kujenga baadaye yako. Hasa kwa ajili ya watoto wako. Baraka ya 40 ya mtoto kutumia mamilioni ya pesa kana kwamba ni tukio la kitaifa. Fanya kitu kingine cha kutunisha akaunti yako.
Inahitaji moyo wa kiwendawazimu kidogo. Hata kama wapo wadhamini wa shughuli kama hiyo ya 40 komonio au birthday kama siyo kipaimara. Unaweza kufanya shughuli ya kuingiza pesa zaidi na wadhamini hao hao wakadhamini na wakajitangaza.
Siri ya utajiri ni kuingiza kingi na kutumia kwa kiasi. Hakuna uchawi zaidi ya huo. Kuna shughuli za kujionesha kwa watu ambazo hazifanani na mtoto aliyekulia katika umasikini. Haya mambo yatafanywa na watoto wako ambao kwa wakati huo wataitwa watoto wa matajiri kutokana na namna ulivyowatengenezea maisha kabla.
Huu ni wakati wa kupiga pesa, siyo kuteketeza pesa. Kuna wanamuziki wengine wanataka kuwa sehemu alipo Diamond, bila kupitia njia alizopita. Wanapata matajiri wawezeshaji wanaomba pesa za video ya soko la Afrika.
Wakati hata Tandale hajajulikana bado. Matokeo yake video ya milioni 50 inaenda kuingiza Sh3 milioni kwa shoo za Fiesta. Kutaka tu awe na video sawa na Diamond, ambaye soko lake limesambaa mpaka Sierra Leone.
Wasanii mlio nyuma ya Diamond pigeni kazi kwanza hapa Tanzania. Kamata pesa mashabiki wa hapa kabla ya kuwawaza kina Davido.
Kabla ya kuwaza kuwa na video kama ya Diamond, tengeneza himaya yako nyumbani. Kuwa na wafuasi wako unakotoka kabla ya kutafuta wafuasi kwa majirani.
Diamond hakuanza ghafla. Aliiteka Bongo, akaiteka Afrika Mashariki. Kabla hajaanza kuwakalisha kina Davido kwenye vibaraza vya mama zao huko Abuja na Lagos. Jenga himaya yako nyumbani kwanza.
Hili tatizo analo Shetta. Ni mhanga wa kutaka kuwa Diamond kabla ya kupambana kuwa Daz Baba.
Shetta alikuwa na haraka sana, na haraka hiyo imemponza. Hivi leo wawezeshaji ni ngumu kutoa mamilioni ya pesa kwa mtu ambaye hata Arusha hawezi kufanya shoo ya milioni sita peke yake. Alisahau kuwekeza mtaani kwao akataka kuwekeza kwa jirani kama Diamond.
Haraka ya matumizi makubwa ya pesa bila mipango.
Pesa za kwenda kutengenezea video Afrika Kusini, tumieni kujijenga Tanzania kwanza.
Wakati una mshangaa Shetta hata anayemuiga naye anataka kuishi dunia ya kina Mike Tyson. Anakataa shoo ya milioni 10 huku akinunua cheni ya milioni 100.
Ni pesa yake. Ni haki yake anavyotaka kuitumia. Ila tunataka kuzalisha kina Mo Dewji kupitia muziki huu.
Na hawawezi kupatikana kama wanaopata wanataka kuvaa na kuishi kama Myweither. Pigeni pesa. Wekeza vya kutosha haya maisha unayotaka kuishi watakuja kuyaishi watoto wetu.
Hasira za kuishi kwenye maisha duni lipiza kwa watoto wako. Sisi hata tutajirike vipi bado tutatambulika kama watoto wa masikini mpaka tunakata roho.
Na wadau wa muziki nchini wanahitaji kubadilika kifikra. Huu siyo muda wa kukandamizana ili wapate kikubwa kuliko wavuja jasho ambao ni wanamuziki.
Kama rahisi hivyo waambieni watoto wenu waingie studio. Wafanye kile wanachofanya kina Dimpoz, kisha wafanyisheni shoo za kujitolea kwenu.
Ni wakati wa kuwaeleza ukweli waandaaji wa shoo za nyumbani. Kwamba kabla ya kumuita Diamond kwanza ujue ukumbi gani wa kumfanyisha shoo ya kuzidi Milioni 100.
Na wasaidizi wake (Mameneja) si busara kufanya mazungumzo na mtu ambaye anataka kufanya shoo Mbagala.
Unafanya mazungumzo na mtu anayetaka kufanya shoo Vingunguti kwa ukumbi gani wa kumpeleka Diamond? Mnapotezeana muda mreefu wakati mnajua siyo tu Mbagala, Dar es Salaam hii hakuna ukumbi wa kufanya shoo ya milioni 100 kumlipa mwanamuziki tu. ‘Mapromota’ kokote mliko Bongo hii. Akili zenu zijilazimishe kuamini kuwa Diamond siyo wa nchi hii.
Hamtaki? Unafanya mazungumzo na meneja wa mtu ambaye shingoni ana cheni ya milioni 100, wewe ukatake kumpa milioni 10 kwa shoo? Wakati miaka mitatu iliyopita alimzawadia Wema gari ya milioni 40? Mnachekesha.
By Dk Levy
salaamzao@gmail.com
Simu no 0744053111
Mwananchi