Pasha Ateseka na Penzi la Snura
Msanii wa Bongo Fleva, Khaji Mtepa ‘Pasha’ aliyewahi kutamba na Nyimbo za Thamani ya Penzi, Umeniweza, Hidaya, Ni Soo na nyingine kibao amefungukia mateso makubwa anayoyapata juu ya penzi la msanii mwenzake, Snura Mushi.
Akizungumza na safu hii katika mahojiano maalum, Pasha alifunguka kuhusu maisha yake ya muziki, kawaida, uhusiano na mikakati yake mipya kimuziki.
HADI SASA UMETOA NYIMBO NGAPI?
Tangu mwaka 2006 hadi leo nimetoa nyimbo nyingi sana, mwaka 2008 nilitoa albamu moja yenye nyimbo 14, baada ya hapo, nimekuwa nikitoa single hadi sasa.
NINI KILIKUPOTEZA KWENYE GEMU?
Sijapotea, bado ninaendelea kurekodi nyimbo, nafanya shoo, pengine ukimya ni kwa sababu sijatoa ‘hit song’ kwa muda mrefu.
KUNA WAKATI ULIUNGANA NA H.BABA, MLIFIKIA WAPI?
Ni kweli, tuliungana kufanya baadhi ya nyimbo zetu ila si kwa kuunda kundi la pamoja. Tulitengana baada ya H.Baba kupata menejimenti mpya. UNA MKE AU WATOTO? Nina mtoto mmoja. Anaitwa Ipa, bado sijao ila Inshaallah muda ukifika Mungu atanipatia mke.
WAPI UNAPOHISI BIASHARA YA MUZIKI INA UPUNGUFU KWA BONGO?
Upungufu upo, lakini mimi naamini biashara ya muziki ndiyo kwanza imeanza kushika kasi miaka ya hivi karibuni. Miaka ya nyuma ubora wa kazi haukuwa mzuri kutokana na vifaa duni. Pia hatukuwa na wasambazaji nje ya Bongo. Ingawa mimi nje ya muziki ninafanya biashara tofauti.
NI MSANII GANI WA KIKE NA KIUME UNAYEMKUBALI?
Wapo wengi, kila msanii namkubali kwa kigezo chake, mwingine kwa uimbaji wake mzuri, msanii kama Dyna Nyange namsheshimu sana kwa kukomaa kwenye gemu muda mrefu tofauti na wengine. Kwa upande wa msanii wa kiume ninajikubali mwenyewe.
PENZI LA MSANII GANI WA KIKE WA FILAMU AU MUZIKI HUWEZI KULISAHAU?
Kutoka moyoni, penzi la msanii Snura Mushi, siwezi kulisahau.
SNURA WA CHURA AU MWINGINE?
Yaah. Ni huyuhuyu. NINI HASA CHA TOFAUTI KINACHOKUFANYA USIM-SAHAU? Anajua ‘kucare,’ ni mwaminifu, anajua sana mapenzi, mtoto amefundwa yule, akafundika.
IKITOKEA SNURA AKAKUBALI KUISHI NAYE YUKO TAYARI?
Hapana, imeshapita miaka mingi zaidi ya saba, ni kitambo sana. Kila mtu amesha-move on na maisha yake, mengine yamebaki stori.
MLIDUMU KWENYE UHUSIANO NA SNURA KWA MUDA GANI?
Mwaka mmoja na tuliachana bila sababu zaidi ya kila mtu kuwa bize na kazi zake.
UNAMAANISHA WAKATI UKIWA NAYE HAKUWA NA MTOTO?
Ndiyo, zamani sana, hata muziki alikuwa hajaanza, ni enzi za Jumba la Dhahabu ingawa na mimi pia niliigiza naye filamu mbili ikiwemo Kisasi cha Mzimu na Uungwana.
UMESHAWAHI KUVUTA AU KUDILI NA MADAWA YA KULEVYA?
Hapana, sijawahi kuvuta, kutumia hata pombe pia situmii. Vita ya madawa naiona ni hatua nzuri, waendelee kupigana nayo, isiwe kwa wasanii pekee, iwe kwa jamii nzima.
UNA MIKAKATI YA KURUDI KWENYE SANAA MWAKA HUU?
Nazidi kujipanga na nitarudi kwa kishindo, mashabiki waendelee kusubiri
Chanzo:GPL