-->

Sakata la Q-Chief, Qs Mhonda Nyuma Yake Kuna Wcb?

HAINA tofauti sana na zile tetesi za usajili tunazo zisikia kwenye ulimwengu wa soka, ila safari hii tunazisikia kwenye tasnia ya muziki kufuatia mkongwe wa Bongo Fleva, Abubakary Katwila ‘Q Chief’ kuhusishwa kutua pale Wasafi Classic Baby (WCB).

Uvumi huo umepata nguvu siku chache baada ya Q Chief kutangaza kuvunja mkataba na uongozi wake chini ya kampuni ya QS Mhonda J, kwa madai ya kutoridhishwa na mwenendo wa utekelezwaji wa mkataba huo wa maisha.

Chila anadai kuwa yeye ni msanii mkubwa hivyo anahitaji kubadilika kwenye kazi zake mpaka katika maisha ya kawaida kitu ambacho uongozi wake chini ya mtaalamu ya ujenzi, QS Mhonda J wameshindwa kuvitekeleza.

Wakati mvutano huo ukiendelea baina ya Q Chila na QS kuna picha zimesambaa kwenye mitandao ya kijamii zikimuonyesha yupo na Bosi wa WCB, Diamond Platnumz taswira inayojengeka hapo ni ile ya Q Chief kujiunga na lebo hiyo.

Swaggaz tukaona isiwe tabu, tukamtafuta Q Chief mwenyewe ili aliweke wazi suala hili ambalo kiukweli kitaani limezua gumzo na kuwaachia maswali yaliyokosa majibu.

PICHA YAKE NA DIAMOND VIPI?

Q Chila anasema ni kweli amekutana na Diamond Platnumz na kikubwa walichozungumza ni mwenendo wa muziki wake pamoja na kupata ushauri kutoka kwa mdogo wake huyo mwenye mafanikio.

“Kweli nimepata taarifa kuwa Q Chila nimevunja mkataba na QS Mhonda kwasababu nataka kusainiwa kwenye lebo ya WCB chini ya Diamond Platnumz.

“Taarifa hizo si za kweli, kuondoka kwangu kwa QS ni moja ya mipango niliyokuwa nayo katika kuboresha kazi, lakini pia Diamond aliniita nyumbani kwake kama kaka yake ili tuzungumze kuhusu mwenendo na hatima yangu kupitia kile ninachokifanya,” anasema Q Chila.

Anasema Diamond alikuwa na lengo zuri la kumuita nyumbani kwake na walitumia zaidi ya saa zisizopungua 18 kujadiliana namna ya kufikia malengo.

KWANINI AMEVUNJA MKATABA?

“Nieleweke kuwa nimeachana na QS Mhonda siyo kwasababu ya WCB, nimetoka kutokana na kuanza kuingizwa kwenye uwekezaji na watu ambao siwatambui, nilijaribu kufanya naye vikao vya ndani kuhusiana na jambo hilo kwa zaidi ya mwaka mmoja nikitaka tubadilishe mwenendo lakini hakuwa tayari,” anasema Q Chila.

Aliongeza kuwa kila msanii anayefanya muziki anataka mafanikio na hakuna anayetaka kufanya kazi za  hasara hivyo yupo tayari kufanya biashara na WCB kama watamwitaji.

QS MHONDA WAFUNGUKA

“Q Chila ndiye aliyesaini mkataba akiomba kujengewa nyumba ya kuishi na familia yake, bima na gari la shilingi milioni 35, unawezaje kuinyima bendi ya Jahazi inayoingiza mapato mengi umpe mtu ambaye ukienda kwenye shoo anapata Laki 2 haiwezekani,” anasema Obama Japai meneja kutoka kampuni ya QS.

KAULI TATA YA DIAMOND PLATNUMZ

Taarifa kutoka kwenye moja ya tovuti za kiburudani zimeonyesha video ya Diamond akisema kuwa ni yupo kwenye mazungumzo ya kikazi na mkongwe huyo.

“Unajua lengo langu kama kijana ni kujaribu kufanya kazi kwa ushirikiano, ‘so’ tuko kwenye maongezi na braza tunaangalia jinsi gani tunaweza kufanya kazi kwasababu ni mtu ambaye namkubali na kumuamini.

“Ni mtu ambaye najua kabisa akibonyeza ‘button’ tu basi mji mzima umechafuka. Kwa hiyo siwezi kuongea mengi sema watanzania watuombee dua tunachopanga kifanyike vizuri,” anasema Diamond Platnumz.

Mtanzania

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364