Aunt, Mke wa Iyobo Wapatana
DAR ES SALAAM: Yamekwisha! Baada ya kudumu ndani ya bifu kwa muda mrefu huku wakituhumiana uchawi, hatimaye mwigizaji Aunt Ezekiel na mzazi mwenzie na Moses Iyobo, Mwengi Ally wamekutana na kumaliza tofauti zao.
Mapema mwaka jana, wawili hao waligombana kufuatia Iyobo ambaye ni dansa wa staa wa Bongo Fleva, Nasibu Abdul ‘Diamond Platnumz’ kummwaga Mwengi kisha kuanzisha uhusiano na Aunt ambapo uhusiano huo ulijibu na wakafanikiwa kupata mtoto.
Aunt ndiye aliyeamua kufuta ‘kinyongo chao’ ambapo alisema hakuona sababu ya wao kuendeleza bifu lisilokuwa na msingi wowote na kuwa wao ni wazazi na watoto wao ni ndugu wa damu moja, alimshauri Iyobo awakutanishe, wamalize tofauti zao.
Baada ya kukubaliana, Aunt na Mwengi walikutana katika Hoteli ya Girrafe iliyopo Mbezi Beach, jijini Dar wakiwa na Iyobo ambaye alisimamia zoezi zima la mapatano kwa wawili hao kuzungumza, wakaelewana, ‘wakazika’ tofauti zao na kila mmoja kubeba mtoto wa mwenzake kisha kula na kunywa pamoja.
Akizungumzia tukio hilo la kiungwana baada ya Risasi Jumamosi kumtafuta, Aunt alisema:“Unajua sisi ni wazazi na tuna watoto kwa baba mmoja (Iyobo), kuendeleza mabifu ambayo hayana msingi siyo kitu kizuri tunatakiwa kuwafundisha watoto wetu upendo siku zote, ndiyo maana tumeyamaliza,” alisema Aunt.
Kwa upande wa Mwengi, alisema:
“Hakuna jambo lisilokuwa na mwisho vitu vingine ni vya kupita katika maisha ya sasa hivyo ni bora kuweka mabifu pembeni ili kuruhusu baraka,” alisema Mwengi.
Wawili hao walikubaliana kuwa muda wowote Mwengi atakuwa akimpeleka mtoto wake nyumbani kwa Iyobo (baba’ke) na baadaye atakapofikisha umri wa kuanza masomo, atamhamishia nyumbani anakoishi Iyobo na Aunt ili wamlee pamoja na mtoto wa Aunt.
Kabla ya kupatana huko, Mwengi alimtuhumu Aunt kuwa ni mchawi.
Chanzo: GPL