Baba Uwoya amgomea Janjaro
MZEE kaamua kukausha tu, sio kwamba hasikii blabla zenu mnazochonga juu ya bintie Irene Uwoya. Lakini kubwa ni kwamba ameikataa ndoa ya bintie huyo dhidi ya mkali wa muziki wa kizazi kipya hasa ule wa kufokafoka, Abubakar Chende ‘Dogo Janja’ a.k.a Janjaro, akidai haitambui japo anatafuta nafasi ili ajue ukweli ulivyo.
Ndio, Baba mzazi wa nyota wa filamu nchini, Irene Uwoya, Mzee Pancras Uwoya amefichua amefikia hatua ya kuamua kuweka pamba masikioni ili asisikie namna bintiye anavyonangwa kila uchao na vyombo vya habari, hasa mitandao ya kijamii.
Mzee Uwoya amesema amefikia hatua hiyo kutokana na kukithiri tabia ya mtoto wake huyo kusemwa na kuandikwa kila uchao, jambo ambalo mwanzoni lilimpa shida kabla ya kuamua kukausha ili maisha yasonge mbele.
Baba Uwoya aliyasema hayo, wakati mtoto wake huyo akiwa bado midomoni mwa watu kutokana na stori yake ya hivi karibuni kuteka habari za burudani kwa kitendo chake cha kufunga ndoa na msanii Dogo Janja.
Habari hiyo imekuwa kubwa kutokana walivyotofautiana umri na Dogo akiwa na miaka 20 tu, huku mwenza wake huyo akiwa na zaidi ya miaka 30 ikiwa ni tofauti ya wastani wa miaka kumi.
Akizungumza na Mwanaspoti, Mzee Pancras alisema awali kama mzazi ilikuwa inamuuma sana kila akiona mtoto wake huyo kipenzi akiwa anaandikwa vibaya kwenye media, lakini ikafika mahali akazoea na sasa hivi wala haangaiki.
“Nimejifunza ukiwa na mtoto msanii kama mzazi unatakiwa uwe na roho ngumu la sivyo unaweza kupata magonjwa ya shinikizo la damu na mengine kila mara, kwani
inaongeza presha, ila nashukuru kwa sasa nimekomaa na hilo na kwa kuwa ndio kazi aliyoichagua mwanangu sina budi kuwa mvumilivu,” alisema baba huyo.
Kuhusu sakata la mtoto wake kufunga ndoa na Janjaro, alisema ndoa hiyo kama mzazi haitambui na kwa kuwa suala hilo lilifanyika akiwa nje ya Dar es Salaam kikazi.
Hata hivyo, alisema ana mpango akikutana na mwanae uso kwa uso na atamuuliza kuhusu ukweli wa jambo hilo, huku akisisitiza mkwe aliyekuwa anamjua kuwa amemuoa mwanae kihalali marehemu Hamad Ndikumana ‘Kataut’, aliyekuwa akisakata soka na mzaliwa wa Rwanda.
Ndikumana alifariki dunia mwishoni mwa mwaka jana na Irene alienda kuhani msiba mara baada ya mumewe huyo aliyekuwa ametangana naye kuzikwa siku moja baada ya kifo chake cha ghafla.
“Siwezi kuamini yasemwayo na mitandao ya kijamii au vyombo vya habari bila kupata ukweli kutoka kwake kazi ambayo natarajia kuifanya pindi nitakapokutana naye ana kwa ana kwani mpaka sasa hivi pamoja na kwamba tunawasiliana kwenye simu hajawahi kuniambia jambo hilo na mimi kama baba sioni haja ya kumuuliza,” alisema Mzee Pancras.
Irene na janjaro walishtukiza mashabiki wao mwishoni mwa Oktoba mwaka jana baada ya kuzagaa picha zao wakiwa wanafunga ndoa nyumbani kwa mmoja wa Meneja wa Diamond, Hamis Taletale ‘Babu Tale’ na baadaye kufahamika kuwa wawili hao hawakuwa wanaigiza ila ni kweli waliamua kufunga pingu ya maisha na wasanii wa Tip Top Connection anakotokea Janjaro ndio walioshiriki sambamba na wasanii wengine wachache walioshtukiza ishu nzima.
Hata hivyo, mpaka sasa bado kuna baadhi ya mashabiki hawaamini kama ni kweli wenzao hao wamefunga ndoa kikwelikweli kutokana na kushindwa kuonekana pamoja kama ambavyo Shilole na mumewe Uchebe wanavyokuwa kama kumbikumbi.
Mwanaspoti