-->

Bongo Movie Tengenezeni Sababu ya Filamu Zenu Kupendwa

UNAWEZA kumpeleka ng’ombe mtoni kwa kutumia nguvu nyingi, ila ukashindwa kutumia nguvu hiyo hiyo kumfanya anywe maji ya mto, kwa kuwa uamuzi wa kunywa au kutokunywa ni wake.

Aunt Ezekiel, JB na  Kajala, wasanii wa bongo movie

Mapema wiki hii jijini Dar es Salaam baadhi ya wasanii wa filamu walifanya maandamano ya kupinga uuzwaji wa filamu za nje zisizofuata utaratibu kwa kile walichodai zinashusha soko la filamu za ndani.

Hapo ndipo gumzo lilipoanzia. Kuna kundi kubwa la watu waliounga mkono tukio hilo na wengine wengi, wakiwamo mastaa walipinga kitendo hicho.

Ninachokiona

Kuna ufa mkubwa kwenye tasnia ya filamu na endapo usipozibwa tutashuhudia tasnia hii ikikosa mwelekeo na kupoteza ajira za vijana wengi wanaotegemea sanaa kuendesha maisha yao.

Umoja wa wasanii umebaki kwenye vyama pekee na siyo ndani ya mioyo ya wanachama, yaani wasanii. Iweje wasanii waliopo kwenye chama kimoja wagawanyike kwenye hili lililobeba taswira ya kuijenga sanaa.

Iweje JB, Ray, Richie Richie, Wolper, Kajala na wengine waandamane na punde aibuke Steve Nyerere na kupinga kwa hoja walichokifanya wenzake.

Tujikumbushe hii

Kipindi cha nyuma kabla hatujaanza kutengeneza filamu zetu, tulikuwa tukipata uhondo wa filamu za Marekani, Uingireza, China, India na kwingineko.

Hakika tulifaidi utamu wa sanaa ya kina Arnold Schwarzenegger, Rambo, Jet Li, Donnie Yen, Bruce Lee, Steven Seagal, Amitabh Bachchan, Sunny Deol na wengine wengi kwenye vibanda umiza kule mtaani.

Baadaye zikaja filamu za Nigeria ambazo zilipoteza umaarufu wake Tanzania ilipoanza kutengeneza michezo ya kuigiza katika runinga (Tamthilia) na hatimaye zikazaliwa filamu zilizofanya vizuri sokoni na kutuletea mastaa hawa tunaowaona.

Unaweza kuona ni namna gani filamu kutoka nje zilivyoamsha akili zetu na sisi tukathubutu kuingia kwenye utengenezaji na kufanikiwa kutamba mpaka nje ya mipaka yetu, sasa iweje leo tuseme filamu kutoka nje zinaua soko la ndani.

Kilichoikumba tasnia

Baada ya kupata ustaa na kujizolea mashabiki wengi, wasanii wetu wamekuwa wakifanya kazi zao kwa mazoea, wakijua kabisa ni lazima mashabiki watanunua siyo kwa kupenda maudhui ya kazi, bali kwa ajili ya ukubwa wa majina yao.

Mfano mdogo ni huu, hebu linganisha kava za filamu zetu na zile za nje, utaona filamu zetu zikipambwa na mastaa wakubwa na warembo wenye maumbo ya kuvutia wakati wenzetu hawategemei hayo kuuza filamu zao.

Weledi wa kazi umepungua, filamu zetu hazina ubora unaokidhi, hakuna uwekezaji unaofanyika, hakuna mawazo mapya kwenye tasnia, ndiyo maana lokesheni kila siku ni zile zile kiasi kwamba mashabiki wamechoka na kuamua kutazama filamu za Kikorea zenye ladha waliyoikosa nyumbani.

Ukweli filamu za nje

Siungi mkono uuzwaji usio halali wa CD zenye maudhui ya picha jongevu kutoka nje kwa sababu serikali inapoteza mapato. Kinachofanyika ni kwamba, mtu anapakua filamu ya nje kwenye mtandao, anaiweka kwenye CD, anatengeneza kava zuri na kuiingiza mtaani kwa bei isiyozidi elfu 2 na ndani yake zitapatikana nyongeza ya filamu zaidi ya tano.

Kwa kuwa maudhui yanavutia, shabiki anaacha kununua filamu ya kibongo inayouzwa elfu 5 yenye maudhui aliyoyazoea na kununua ya Adaan, filamu itakayokata kiu yake kwa bei rahisi.

Wasanii fanyeni haya machache

Kwanza kuweni wamoja ili mpiganie na mpate sheria mpya ya filamu itakayowalinda nyinyi na kazi zenu, pili jiulizeni kitu gani kimekosekana kwenye filamu zenu mpaka mapenzi ya mashabiki yamehamia ughaibuni.

Mkifanikisha hayo, hamtakuwa na haja ya kuandamana wala kumuona Mkorea kama nuksi kwenu, kumbukeni mashabiki wanataka ladha mpya, fanyeni kazi na muache kuchezea sanaa yenu, nadhani nimeeleweka.

Mtanzania

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364