Chilwa Kutoa Upapa Kula Dagaa Katika Tasnia ya Filamu
TUPO katika mchakato wa uchaguzi wa vyama vinavyounda shirikisho la filamu Tanzania (TAFF) tukiangazia uchaguzi wa chama cha waigizaji Taifa TDFAA huku kila mgombea akijinadi kwa madaha na leo hii FC iliongea na Salum Hussein Chilwa akiitaka nafasi hiyo na kumwaga sera zake kwa wapiga kura wake.
Chilwa ambaye alikuwa makamu mwenyekiti wa chama cha Waigizaji Kinondoni anasema anatosha kugombea uenyekiti Taifa kwania ana uzoefu mkubwa na anakuja kwa ajili ya kuhakikisha kuwa ule mfumo wa Samaki mkubwa Papa kula Dagaa anaumaliza na kuwa na tasnia yenye usawa kwa wote kimaslahi na si kama ilivyo sasa.
“Hali ya tasnia ya filamu kwa sasa haipo sawa kabisa kwani wasanii chipukizi wanajikuta wakitumikishwa katika filamu za wasanii wenye majina pasipo malipo stahili wakiwa na imani ya kutoka na kutoka hawatoki, na wanapopeleka kazi zao sokoni kuna changamoto nyingi,”anasema Chilwa.
“Nina uwezo mkubwa sana katika masuala ya uongozi nafikiri wakati umefika kuisaidia tasnia ya filamu ya Tanzania kwa sasa naamini ninatosha kabisa na nitfanya maajabu makubwa katika kuhakikisha Waigizaji wanapata maslahi halisi,”anasema .
Chilwa anasema anawaahidi waigizaji kuwa atafanya makubwa sana na kama hatafanya yale ambayo yanawasumbua na kuwanyima maslahi basi ahukumiwe kwa hilo hivyo anataka awe mfano wa kiongozi makini ambaye atahakikisha makundi yanakufa na kuwa wote sawa bila kufanya ubaguzi.
Huyu ni Salum Hussein Chilwa kwa ufupi ni nafasi yako kumpigia kura ili awapoteze Mapapa yanayokula Dagaa katika tasnia ya Filamu
FC