-->

Chriss Mhenga Chimbuko Bongo Movie (Sehemu ya Kwanza)

UNAPOONGELEA tasnia ya filamu Bongo ni lazima uanzie kwenye michezo ya kuigiza kwani wanaong’ara na kufanya vizuri asilimia kubwa walikuwa ni waigizaji kutoka katika kundi la Kaole Sanaa Group, lakini si wengi ambao wanamtambua muasisi na mzalishaji wa vipaji hivyo huyu si mwingine ni Chrissant Mhenga.

CHRISS MHENGA Muasisi na muongozaji wa kundi la Kaole Sanaa Group.

Uncle Chriss kama wengi wanavyomjua ni Baba wa familia ya watoto watatu ambao ni Allen, Aneth na Asnat na mkewe Khadija King, aliingia rasmi katika utengenezaji wa filamu mwaka 1995 baada ya kupata mafunzo kutoka kwa walimu mahiri wa filamu katika kampuni Tanzania Filamu (Tanzania Film Company)

Anasema kuwa jinsi anavyoiangalia tasnia ya filamu hapa nchini imekuwa na mabadiliko tofauti tofauti, anakumbuka wakati yeye anaanza kufundishwa na kupewa maelekezo na wataalam kwa wakati huo tasnia ilikuwa ni fani ya kisomi zaidi kuliko sasa. Kwa hiyo watu walikuwa wanafanya kazi kiweledi zaidi.

Tanzania Film Company (TFC) ilikuwa shirika la Serikali hivyo ilikuwa ni lazima taluma itumike zaidi kwani ilikuwa kwa ajili ya kutengeneza filamu za kuelimishia kama Kilimo bora, mambo ya Afya na matukio ya kijamii na wafanyakazi wake walisomeshwa na Serikali na kuwa mahiri katika sekta hiyo.

Mhenga akiwa kazini kwa umakini kabisa

Hapa alikutana na magwiji wa utengenezaji wa filamu wa (TFC) na kumkubali kulingana na uwezo wake baada ya mafunzo ya mara kwa mara kutoka kwa Mwalimu Mzee Mlay na Hammie Rajab wote ni marehemu kwa sasa alionyesha kukomaa na kuanza utengenezaji wa filamu badala ya makala za kijamii zaidi.

“Hammie Rajab ndio aliyenivuta kwenda kukutana na watalam wa TFC na kunitia moyo naweza baada ya kuona kazi zangu nikiwa na Studio ndogo nikifanya kazi za Harusi akaniambia wewe unaweza kuwa Filmmaker,”

Mwaka 1995 alifanikiwa kufanya kazi na marehemu Hammie Rajab baada ya kufanikiwa kurekodi filamu kutoka katika hadithi ya kitabu cha Gubu la Wifi kitabu ambacho kilikuwa utunzi wa marehemu Hammie Rajabu mwenyewe na kufanikiwa kutoa hamasa kwa watanzania.

“Nikiwa na marehemu Hammie Rajabu nilitengeneza filamu ya Gubu la Wifi baadae nikaenda Tanga kukutana na Jimmy Master wakirekodi filamu ya Shamba kubwa ambapo baadae alikuja jiji Dar nikarekodi naye sinema yake ya Kifo Haramu,”alisema Uncle Chriss.

Hiyo ndio ilikuwa safari ya uncle Chriss na kuwa chanzo kikubwa cha uibua wa vipaji Tanzania kwani unapoongelea wasanii ambao ni watayarishaji mahiri au waongozaji ni zao lake kitaluma yeye ni mtayarishaji , muongozaji na mpiga picha mzuri wa Filamu na tamthilia Tanzania.

KAOLE ILIANZEJE?
Mwaka 1999 aliajiriwa na kituo cha Televisheni cha ITV akiwa mtayarishaji na kumuongozaji wa vipindi alinza kufanya kazi na waigizaji kama vile Mzee Pwagu marehemu, marehemu Rajab Hatia (Mzee Kipara), Mama Hambiliki wakitokea wakitokea Redio Tanzania enzi hizo ikiitwa RTD.

Kwa sababu siku zote anaamini sana kuhusu Weledi alianza kuwafundisha wasanii kama Mahsein Awadh (Dr. Cheni), Nina, Mashaka na baadae kuwaibua wasanii kama Vincent Kigosi (Ray), marehemu Steven Kanumba wakifanya mazoezi katika ukumbi wa Magomeni Annex.

Hapo ndio ilikuwa hatua ya kutengeneza vipaji kwani pamoja na kuwa na ufundishwaji sawa lakini kulikuwa na ushindani mkubwa ili msanii aweze kurekodi lazima awe na vigezo huku muhimu kuliko vyote ni suala la nidhamu na usikivu darasani hivyo viliweza kumbeba msanii.

“Wengi wanawaona tu wasanii hawa wakitamba lakini walipikwa kwa nguvu nyingi sana na kufika hapo walipo japo kuna wakati wanajisahau na kujikweza pengine hilo ndilo anguko lao,”

Kaole baada ya kuwa kundi mahiri katika utengenezaji wa tamthilia chini ya Uncle Chriss halikuiingia moja kwa moja katika utengenezaji wa filamu kwani walikuwa wakihofu wataweza kuonyesha kile ambacho wanapata katika Televisheni?

Hivi Mhenga anasema kwa haraka haraka kitu alichokiona kinaweza kuwafurahisha watu ni kuanza na urekodiji wa komedi ambazo hazikuwa na gharama katika utengenezaji kuliko filamu na ilikuwa katika harakati za kujikimu yaani kuongeza kipato kwa wasanii wake kwani kile kipato kilikuwa hakitoshelezi.

Kundi lilikuwa kubwa sana kiasi cha kuhitaji mapato zaidi hivyo baadhi ya wasanii walitengwa na kuwa na kundi lao la uigizaji katika kundi la Mizengwe ililowakutanisha wasanii kama vile marehemu Max, Zembwela na wengineo, kama ni njia ya majaribio Komedi zilirekodiwa.

Baada ya mafanikio na kumpata mtu wa kufanya nao ambaye alikuwa ni Mtitu Game walianza na filamu ya kwanza ya Johari ambayo ndio pengine ilichangia kufifia kwa kundi la Kaole Sanaa Group kwani baada ya hapo Mhenga anasema kati ya wasanii waliotoka ni marehemu Kanumba tu ndio alikuwa ushirikiano.

“Katika tamthilia nilikuwa nikiweka vichekesho kutoka kwa marehemu Max na Zembwela ITV wakanishauri nitengeneze kundi lao pekee hapa ndio ilipozaliwa Mizengwe ambayo ipo hadi leo,”

NINI SABABU YA KUYUMBA KAOLE SANAA GROUP?
Mwaka 2005 kundi la Kaole Sanaa Group lilikuwa na umaarufu mkubwa sana wakiwepo wasanii kama vile marehemu Kanumba, Ray na wasanii wengine wengi hivyo mwaka 2006 kundi hilo likaondoka kuonyesha michezo yake katika televisheni ya ITV na hapo ndio ikawa mwanzo wa kusambaratika.

Baada ya mkataba kumalizika takribani miaka saba ya kufanya kazi na kituo hicho cha runinga, Mhenga anasema ilikuwa ni changamoto tu katika ukuaji wasanii na pengine ilikuwa katika wasanii kujitambua na kuona wanahitaji kujitegemea au kuwa huru katika kutengeneza maslahi zaidi.
“Baada ya mkataba kumalizika ndio yaliyotokea hayo may be labda ndio wasanii walikuwa wamejitambua na kuona ni wakati wao kufanyakazi zao kwa wale waliokuwa wamejiweka vizuri wakaanza,”

“Na bado mimi nilikuwa bado mfanyakazi wa ITV hivyo nikabaki na kuendelea na kazi haikuwa rahisi kwani huwezi kumzuia mtu asiondoke na tayari keshapata ujuzi wake,”

Na hiyo ndio ilikuwa mwanzo wa mgawanyiko mkubwa kabisa kutokea kwani kwa wale waliokuwa wamejiandaa walianza rasmi kujikita katika filamu badala ya tamthilia kutoka na malipo kuwa makubwa zaidi kuliko tamthilia ambayo walifaidika na umaarufu tu.

Mhenga akiwa kazini kwa umakini kabisa

ANAONGELEAJE KUHUSU NIDHAMU KATIKA VIKUNDI NA WASANII BINAFSI?
Siku za nyuma kulikuwa na ushindani wa uwepo wa makundi ya uigizaji ambayo yaliundwa katika mfumo wa nidhamu ambayo kulikuwa na kundi kama Nyota Ensemble (Mambo hayo), Kidedea, Msanii Afrika, Kamanda Family na mengineyo ambayo yaliweza kujenga wasanii.

Mhenga anasema kuwa kwa sasa kumekuwa na mabadiliko makubwa sana katika tasnia nzima kwa ujumla wake huku suala la nidhamu ikiwa ni changamoto kubwa nap engine anasema kuwa labda inatokana na hali ya wasanii kufanya kazi ndogo na kupata fedha nyingi

Siku za nyuma ilikuwa wasanii kama wanajitolea na kuambulia umaarufu ambao wenye uelewa waliweza kuutumia vizuri na kuweza kutengeneza ajira au kuwatengenezea maisha mazuri ambayo kama wasingekuwa waigizaji wasingepata nafasi hizo bila kujulikana.

“Filamu ya leo si kesho unajua siku za nyuma watu wengi walikuwa hawana cha kufany hivyo ilikuwa lazima wafanye tamthilia ili wajulikane lakini unafanya ili uwe pesa,”

Anahisi kukosekana wasanii kufika sehemu moja na kufanya mazoezi kwa pamoja na kufundishwa mambo mbalimbali imesababisha ukosefu wa nidhamu kwa wasanii kwani siku hizi ni sura ya msanii na si uwezo wake katika kuigiza na kuheshimu taluma.

Wasanii wanajihisi wanapata fedha nyingi na kuona hakuna sababu ya kwenda shule kwani ukiwa na fedha tu unaweza kukusanya waigizaji na kutengeneza filamu, lakini kitu kingine kilichofanya tasnia idorore ni wasambazaji kununua sinema bila kujua kazi bora.

Siku za nyuma watu walifanya kazi kwa nguvu sana wakitaka vipaji vyao vionekane au wawe maarufu kwani kipata ambacho kilikuwa kikilipwa kilikuwa chini kwa maana ya ukubwa wa kundi kwani badala ya kugawana ilikuwa fedha zikitumika katika kubororesha tamthilia iwe bora.

“Kutokana na malezi bora kwa wasanii waliokuwa pamoja waliweza kuwa wastamilifu na kuipenda kazi yao pamoja na kuwa na malipo kidogo na watu walichukulia baada ya hapa wanaweza kupata pesa katika shughuli zao nyingine,”

Mhenga anaamini kuwa kuwa na makundi Fulani Fulani na yakakaa pamoja na kujifunza ni jambo muhimu sana kwani toka kuondoka kwa makundi hayo ya yaliyotamba kumeyumbisha tasnia ya filamu na kuwa ilivyo sasa, ni vigumu kumjengea nidhamu mtu wanayekutana naye katika kazi tu.
itaendelea jumanne USIKOSE!

Chanzo:FilamuCentral

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364