-->

Darassa Afunga Mwaka Kwa Kishindo,Diamond Bado Yupo Juu!

TUMEZOEA kusikia nyimbo za mapenzi zikipendwa zaidi kuliko zile zenye ujumbe wa masuala mengine muhimu kwa jamii. Mara nyingi ngoma zenye meseji ni zile zinazohusisha mtindo wa kofokafoka yaani Rap.

Kwenye historia ya Bongo Fleva, nyimbo za Rap hazikuwahi kuzizidi zile za mapenzi. Ngoma zenye jumbe za mapenzi zinapendwa zaidi sokoni na ndiyo  zinazochezwa zaidi.

Sasa inakuwaje pale ambapo rapa anavunja rekodi nyingi kwa wakati mmoja ambazo kwa miaka mingi marapa wengine wameshindwa kuzivunja?

Hapo ndipo Swaggaz linapomkumbuka Ramadhan Sharif  ‘Darassa’ ambaye ni bosi wa Lebo ya Classic Music Group (CMG), ambaye anafunga mwaka kwa historia ya aina yake akiwa na ‘Wimbo wa Taifa’ Muziki.

 

‘SIKATI TAMAA’ MPAKA ‘HEYA HAYA’

Hakuna aliyewahi kumuelewa Darassa kabla, labla watu wake wa karibu ila Watanzania wakampenda pale alipochomoka na Sikati Tamaa, ngoma aliyomshirikisha Ben Pol mwaka 2011.

Baada ya hapo aliachia nyimbo kama Nishike Mkono, Siyo Mbaya  na akaufunga mwaka 2015 kwa kolabo na Ney wa Mitego (Tunaishi) pamoja na ile ya Mr Blue (Heya Haya).

 

AIFUNGIA KAZI 2016

Mwaka ulipoanza Darassa alitupa karata yake ya kwanza kupitia Kama Utanipenda, aliyomshirikisha Rich Mavoko.

Juni 30, akakutana na waandishi wa habari kutambulisha lebo yake ya CMG, staili yake ya kucheza anayoiita Zombie Walk na kuwaweka tayari mashabiki kwa Too Much, wimbo uliotoka Julai 12.

Grafu ya muziki wa Darassa ilizidi kupanda Novemba 23, alipotambulisha ngoma yake mpya, Muziki. Wimbo unaokua siku baada ya siku – wimbo ulioibua vituko mtaani na kupenya mpaka kwa viongozi wakubwa wa Serikali.

Hii ndiyo ngoma yenye mzunguko mkubwa kwa sasa kwenye redio, runinga mpaka kitaa. Usipousikia kwenye nyumba/chumba cha jirani yako basi utausikia kwenye baa iliyo karibu na wewe.

Ni ngumu kuukwepa labla uwe na matatizo ya usikivu ingawa utauona kwenye runinga hata ukiwa una uono hafifu basi utausikia kwenye Bajaj na bodaboda hapo mtaani.

 

MUZIKI YAVUNJA REKODI

Kama nilivyosema hapo mwanzoni kuwa ni ngumu msanii anayerapu kupata usikivu kama anaopata Darassa kipindi hiki.

Desemba 8, ikiwa ni wiki mbili tu tangu Muziki iwekwe YouTube iligusa watazamaji milioni moja, mpaka sasa imetazamwa mara milioni 2.5, kitu ambacho ni nadra kutokea kwa marapa.

Rekodi nyingine ni ile ya kuzificha nyimbo kali zilizotoka sambamba na Muziki. Hakuna ngoma kali kama Dume Suruali ya Mwana FA, Feel Good ya Navy Kenzo, Kokoro ya Rich Mavoko, Kajiandae ya Ommy Dimpoz, Kijuso ya Queen Darleen na nyingine nyingi mpya zimefichwa, habari kubwa ni kuacha maneno na kuweka Muziki.

Kuna kibao kikali kama Salome ya Diamond na Rayvanny? Lakini Darassa kaiweka pembeni. Ni mkali, mbabe, mwenye uwezo na nyota ya ajabu.

Imekuwa ni kawaida kwa wasanii kuwahimiza mashabiki kujirekodi video fupi wakicheza nyimbo zao lakini kwa Darassa imekuwa tofauti kwani mashabiki wenyewe ndiyo wanajirekodi wakiucheza kwa staili mbalimbali wimbo huu.

Bila shaka utakuwa umekutana na video hizo kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii.

 

ANATIA MGUU KWA DIAMOND PLATNUMZ?

Kitaa kumekuwa na ubishani mkubwa. Kuna kundi la watu wanaosema Darassa amechukua nafasi ya Diamond Platnumz hali kadhalika kuna watu wanaopinga kwa kusema hakuna kitu kama hicho.

Ukweli ni kwamba bado ni mapema kumuweka Darassa kwenye uzani mmoja na Diamond Platnumz, tumpe muda kwanza ajijenge. Muziki ndiyo ngoma ya kwanza kwa Darassa kumfanyia maajabu haya tunayoyaona.

Chibu ameshafanya yote kwenye muziki huu, kama leo akisema anaacha muziki basi atakuwa na uwezo wa kuishi na kuingiza fedha kupitia lebo, dili za matangazo na mirabaha.

Je, Darassa akiacha muziki hivi leo ataweza kuishi? Jibu ni hapana. Darassa hajawahi kuwa nominated kwenye tuzo yoyote ya kimataifa. Muziki imemfungulia dunia ndiyo maana juzi imeshika namba moja kwenye Top 10 ya nyimbo za Hip Hop, Trace TV maeneo ambayo Diamond Platnumz tayari ana heshima kubwa.

Diamond Platnumz ndiyo msanii wa kwanza Tanzania kutajwa kwenye Tuzo za BET. Hiyo ni rekodi ambayo Darassa hajaivunja.

Uwekezaji alioufanya kwenye Lebo ya WCB siyo wa kitoto. Hakuna ubishi kuwa Darassa amefunga mwaka kwa nguvu ya aina yake, na bila shaka akiendelea kukaza, mwakani ataleta ushindani mkubwa kwenye soko la Bongo Fleva.

Ni imani yangu kuwa, hata kwenye tuzo mbalimbali za kimataifa mwakani, listi ya wasanii wetu kuwa nominated na pengine kuondoka na tuzo hizo itaongezeka.

Hongera sana Darassa, heshima kwako pia Chibu.

Mtanzania

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364