-->

Fid Q: Mapenzi Yamenitesa Sana Jamani!

AGOSTI 13, mwaka huu ilikuwa ni kumbukumbu ya kuzaliwa kwa Mwanahip Hop, Fid Q na kwa furaha aliyonayo kwa kutimiza miaka kadhaa, siku hiyo aliamua kuachia ngoma mbili kama zawadi kwa mashabiki wake.

Fid-q

Wimbo wa kwanza unaoitwa Sumu aliutoa usiku wa kuamkia Jumamosi iliyopita, baadaye jioni akaachia video ya ngoma nyingine ya Roho aliyomshirikisha Christian Bella.

Licha ya uzuri wa video na ujumbe, lakini Fid Q ambaye jina lake halisi ni Fareed Kubanda anakiri wimbo wa Roho umegusa kisa cha kweli cha mapenzi kilichomtokea miaka iliyopita na ndiyo maana anaonekana na kusikika akiimba akiwa na hisia kali.

“Mapenzi ni matamu, nahofia kuumizwa moyo, nashindwa kujaribu roho inaniuma sana, roho inaniuma roho inaumaaa…’’

Hiyo ni sehemu ya mashairi ya Bella katika wimbo huo. Fid Q naye kuna sehemu anaimba:

“Haki ya Mungu tena chuki humchoma anayeihifadhi, kumsahau sana siwezi… mapenzi yalifanya nikaumbuka ninachoshukuru hayakuniua.”

Championi Ijumaa limezungumza na Fid ikiwemo uamuzi wa kwenda kutengeneza video ya Roho nchini Sweden:

“Ingawa ni muda mrefu sana tangu nilipokutwa na mkasa huo wa kimapenzi lakini nimeamua ‘ku-share’ na jamii katika kipindi hiki. Nimeamua hivyo kwa kuwa kilichotokea nimeshasamehe na nimeanza kusahau,” anasema Fid kisha mahojiano yanaendelea:

Beat ya Roho ilitumika katika wimbo wa Haki mwaka 2014, imekuwaje umesikika tena kwako?

“Ni kweli, tena ilitumiwa na wasanii wengi wa Hip Hop katika ule wimbo ambao January Makamba naye alifanya ‘intro’. Kilichotokea ni hivi, tayari nilikuwa nimeshaitumia hiyo beat katika wimbo huohuo wa Roho ila nilikuwa sijautoa.

“Sasa ilipokuja ishu ya kuimba Haki, P-Funk akahitaji kuitumia beat hiyohiyo. Kwa kuwa ‘idea’ za ujumbe zilikuwa tofauti nikaona siyo mbaya, kwa hiyo akaibadili kidogo, tukafanya ngoma na hakuna tatizo lolote.

Ilikuwaje ukamshirikisha Bella?

“Nilihitaji kufanya kitu cha tofauti tu ambacho nahisi nimefanikiwa. Haikuwa shida kumpata Bella, nilipomshtua akakubali maana ni shabiki wa ngoma zangu pia, nashukuru alinipa ushirikiano mkubwa kukamilisha hii kitu ndiyo maana hata mimi nilipomuandikia script (mwongozo) ya video yake ya Nishike nilifanya kwa roho moja.

Script ya Roho nani aliandika?

“Niliandika mimi lakini nilipoenda Sweden madairekta wakairekebisha kidogo kwa kuwa wao ndiyo wanafahamu zaidi mazingira na mitaa ya Sweden kuliko mimi. Sababu ya kwenda huko ni kubadili upepo na kuwa na kitu cha tofauti.

Kuna sehemu umevaa ‘hood’ (nguo nzito) inaone-kana kama imeanza kuchoka na kuchanika, ilikuwaje?

“Ile ni staili tu kama ilivyo kwa Kanye West anavyovaa zile nguo kama za watu wa zamani. Hii staili niliyoifanya inaitwa Rough, Rugged & Raw, ni ishu ya kuwakilisha zaidi kitaa ila naona kama imekuwa gumzo hivi, hivyo naweza kuanzisha nguo zangu za dizaini hiyo.

Tofauti na Bella kuna sauti inasikika, ni nani huyo?

“Yule anaitwa Paul Ndunguru, anatoka Wa Hapahapa Band, ni mchoraji mzuri, anaandaa vitabu na anapinga ukatili wa mauaji ya tembo, naye haikuwa shida kumpata, nikafanya naye kazi vizuri tu.

Gharama nzima ya video ni kiasi gani?

“Mzoefu anaweza kukisia ni kiasi gani kwa maana ya nauli ya kwenda kule, kugharamia mamodo na kila kitu, japokuwa naona kimsingi tuangalie zaidi ubora wa kazi iliyotoka kuliko gharama, maana hata nchi za wenzetu hawazingatii sana gharama zaidi ya kazi iliyofanyika.

Vipi kuhusu video ya Sumu?

“Video ya Sumu ndiyo ipo kwenye maandalizi, Roho itaangaliwa na Sumu itaendelea kusikilizwa kwenye redio kwa kuwa hata meseji ni mbili tofauti.”

Vipi kuhusu kolabo za kimataifa?

“Hizo zipo lakini siwezi kuongeza chochote hapo kwa kuwa mwenye mamlaka ya kuzungumzia hizo ishu ni Cheusi Dawa, maana ndiyo wasimamizi wa kazi zangu.”

Chanzo:GPL

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364