-->

Hakimiliki Itawanufaisha Wasanii, Mapato ya Serikali

Ili kukidhi mahitaji ya kila siku, jitihada zinahitajika. Kila mtu anayo namna yake halali ya kumuingizia kipato.

Katika harakati hizo wapo wasanii wa uigizaji, muziki au uimbaji, uchoraji, uandishi, utunzi na ubunifu tofauti.

Hakimiliki ni sheria ambayo inampa msanii haki ya kumiliki kitu alichotengeneza au kubuni. Kinaweza kuwa kwenye mfumo au muonekano wa mchoro, picha, shairi au kitabu. Kwa kuwa tu kimetengenezwa au kimebuniwa, hakimiliki inampa msanii haki ya kuwa chake.

Sheria hii inampa msanii haki ya kuzalisha, kuandaa, kusambaza, kutanganza na kuonyesha ubunifu wake kwa jamii. Hizi ni haki za msanii na ni zake peke yake.

Kwa ridhaa yake msanii anaweza kuhamisha au kuuza haki au sehemu ya haki kwa mtu au watu wengine bila kufanya hivyo ni kosa kisheria kwa mtu au watu wengine kutumika kazi iliyobuniwa au kuzalishwa bila ridhaa ya aliyeibuni.

Sanaa kama zilivyo kazi nyingine inatoa elimu na burudani ambapo hutatua changamoto ya ajira, huzalisha na kisha kuchangia uchumi wa nchi.

Shirika la Hakimili Duniani (Wipo) na Chama cha Hakilimili Marekani (IIPA) na washirika wengine kushirikiana na Serikali ya Marekani ilianza kazi ya kufuatilia na kusimamia utekelezaji wa sheria ya hakimiliki kwa wasanii wa Marekani tangu mwaka 1984.

Mafanikio ya kazi yao yameendelea kuonekana, ripoti ya IIPA ya mwaka 2016 inaonyesha kuwa mchango wa hakimiliki kwa uchumi wa Marekani umekuwa ukiongezeka mwaka hadi mwaka.

Mwaka 2015 hakimiliki zimechangia zaidi ya Dola 1.2 trilioni sawa na asilimia 6.88 ya Pato la Taifa (GDP). Katika upande wa ajira hakimiliki imechangia watu kupata kazi zenye hadhi na zinazolipa vizuri.

Zaidi ya watu milioni 5.5 wameajiriwa katika sekta ya sanaa sawa na asilimia 3.87 ya ajira zote nchini humo. Kuanzia mwaka 2012 mpaka 2015 sekta hiyo imekuwa ikikua kwa wastani wa asimilia 4.81 wakati uchumi wa Marekani ukikua kwa asilimia 2.11.

Mauzo ya hakimiliki za wasanii wa Marekani nje ya nchi yao ilifikia Dola 177 bilioni mwaka 2015. Mauzo hayo yanajumuisha muziki, filamu, tamthilia, haki za masafa ya luninga na video, vitabu, majarida pamoja na software za aina zote.

Mchango huo ni mkubwa kuliko mauzo ya bidhaa za kilimo ambazo ziliwaingizia Dola 62.9 bilioni na dawa Dola 58.3 bilioni. Kwa mwaka 2015, mapato ya sanaa hasa kutokana na hakimiliki yalichangia Dola 2.1 trilioni sawa na asilimia 11.69 kwenye uchumi wa Marekani.

Ukiona takwimu hizi utapenda kufahamu hali ilivyo nchini. Tanzania ina sheria ya hakimiliki kwa kazi za sanaa ila malalamiko makubwa yamekuwa ni namna sheria hiyo isivyo na makali kwa wezi wa kazi za sanaa. Kuwepo kwa sheria ni jambo moja, usimamizi ni jambo jingine.

Ni vyema Serikali ikatambua kuwa hakimiliki kwa kazi za sanaa ni chanzo cha uhakika cha mapato. Marekani ni mfano mzuri wa mchango wa sanaa kwenye uchumi wa nchi endapo kutakuwa na mifumo na mazingira mazuri.

Mwaka 2012 Wipo ilifanya utafiti juu ya hakimiliki nchini lakini ripoti yake haifahamiki ilipo huenda ni Serikali pekee ndiyo inafahamu. Wengi wa wasanii wa Tanzania wana majina makubwa na wanafanya kazi nzuri lakini kazi zao na kipato kinachotokana nazo ni vitu viwili tofauti.

Ni wasanii wachache Tanzania wanaoweza kumudu kuendesha maisha yao ya kila siku kwa kutumia sanaa wanayoifanya pekee. Aliwahi kuimba msanii mmoja kuwa, ‘sanaa isiwe daraja la kutengeneza masikini wenye majina makubwa.’

Ni wakati kwa Serikali kupitia na kuangalia upya mifumo yote inayotumiwa na wasanii kuanzia kubuni, kuzalisha, kutangaza na kusambaza kazi zao na kuziba mianya ya upotevu wa mapato.

Itengenezwe sheria mpya ya hakimiliki za kazi za sanaa ambayo itakuwa dawa na uponyaji kwa sanaa ya Tanzania. Si jambo la kufurahia kupata elimu na burudani kutoka kwa wasanii masikini ambao wangestahili kuwa matajiri na kuchangia mapato ya Serikali.

Hakuna utafiti uliofanyika kuthibitisha ila inahisiwa kuwa moja ya sababu za wasanii kujiingiza katika utumiaji wa dawa za kulevya ni msongo wa mawazo unaotokana na ugumu wa maisha wakati huo kazi zao zikiwatajirisha wengine.

Kwa kuanza tununue kazi za sanaa zilizohalali ‘original’ ili msanii apate kipato na Serikali ikusanye kodi. Na Serikali itunge Sheria yenye makali kwani faida zitakuwa pande zote kwa msanii na Serikali.

Kutoisimamia ipasavyo sekta hii si tu kunapoteza kipato halali cha wasanii bali kunachelewesha mapambano dhidi ya umaskini. Kila mdau akiweka nia ya kumaliza udanganyifu unaofanywa kuwanyonya wasanii matunda yake yataonekana.

Kampuni zinazofanya kazi na wasanii kwenye uhamasishaji wa miradi ya aina tofauti, iboreshe maslahi na kusaidia harakati za kurasimishwa kwa sekta hii ili manufaa yanayotokana na kazi zao yawe na mgawo sawa kwa pande zote mbili. Thamani ya wasanii ikipanda, sanaa yetu itakua.

Mwananchi

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364