Hemed ‘PhD’, Filamu Kali, Muziki Mzuri… Utamtaka?
NIKIMTAZAMA msanii mwenye makeke mengi akiwa na uwezo mkubwa wa kuvaa uhusika, Hemed Suleiman ‘PhD’, namkumbuka galacha wa Bongo Fleva Khaleed Mohamed ‘TID’.
TID yeye ni msanii wa Bongo Fleva akitamba zaidi kwenye RnB, ambaye aliweza kung’aa sana enzi zake na hadi sasa akiwa na bendi yake iitwayo Top Band.
Akiwa yupo kwenye kilele cha kukubalika kimuziki, TID alishiriki katika filamu ya kwanza ya Kiswahili iitwayo Girlfriend ambayo kisa chake kinahusu maisha na muziki.
Katika sinema hiyo ambayo TID alishiriki kama kinara, wamecheza wanamuziki wengine kama Gwamaka Kaihula ‘King Crazy GK’, Juma Mohamed ‘Jay Moe’ na Ambwene Yesaya ‘AY’. Wanamuziki hao walishirikiana na vinara wa Bongo Muvi wakati huo, Yvonne Cherry ‘Monalisa’ na Beatrice Morris ‘Nina’.
Mtunzi wake ni Sultan Tamba, huku mwongozaji akiwa marehemu George Tyson. Ilikuwa sinema nzuri, yenye kisa cha kusisimua sana. Baada ya filamu hiyo, TID hakujishughulisha tena na mambo ya filamu, badala yake akaendelea na muziki wake.
TURUDI KWA HEMED
Hemed yeye ni tofauti kabisa na TID, maana yeye alianza kwenye muziki baada ya kushiriki shindano la vipaji la Tusker Project Fame nchini Kenya. Aliporudi Bongo baada ya kumalizika kwa shindano hilo, aliingia moja kwa moja kwenye filamu.
Huko alifanya vizuri sana. Mpaka sasa jina la Hemed PhD ni kubwa zaidi kwenye filamu kuliko muziki ambao kimsingi ndiyo uliomtoa.
Ukiangalia sinema kama I Know You aliyocheza na Yusuf Mlela unaweza kuelewa nini namaanisha ninaposema Hemed ni msanii mkali sana kwenye filamu.
Filamu nyingine alizocheza ni pamoja na Saturday Morning, Hot Friday, Machozi Yangu, Red Cross, Ujinga Wangu, The Waiter, Matilda, Jini Tausi, Bad Girl, For My Child na nyingine nyingi.
Si ajabu, msanii kuwa na vipaji vingi au kutumia vipaji vyake kwa wakati mmoja. Hata wasanii wa nje wanafanya hivyo.
Mbali na Hemed, wapo wasanii wengine wa filamu waliojaribu kuingia kwenye muziki – wengi wamefeli. Kati ya waliofanya vizuri ni pamoja na msanii Snura Mushi ambaye alikuwa kwenye filamu kwa muda mrefu bila mafanikio makubwa.
Baada ya kujaribu tu muziki, akatoka jumla. Mwingine ni Zuwena Mohamed ‘Shilole’ ambaye naye alianza kwenye filamu bila mafanikio makubwa, lakini alipotia maguu kwenye muziki akatusua.
HEMED NA MUZIKI
Pamoja na kung’ara sana kwenye filamu, ni kama Hemed ameusahau muziki uliomtoa. Hatumii nguvu kubwa sana kwenye muziki.
Kwangu mimi, Hemed yupo kwenye Top 5 ya wasanii wa kiume wenye kujua kuvaa uhusika vizuri kwa sasa. Ingawa ni mzuri kwenye sinema, kila ninaposikiliza na kutazama video za muziki wake, naona ana kitu kikubwa zaidi kwenye muziki.
Inawezekana kwa sasa ameamua kufanya muziki kama burudani tu na filamu kama kazi, jambo ambalo nadhani anakosea kidogo.
Hemed anatakiwa kujua kuwa muziki upo ndani ya damu yake zaidi; hata unapoangalia video zake, utagundua kuwa ni msanii mkali ambaye kama akikaza kidogo, anaweza kuleta ushindani mkubwa kwenye muziki.
Angalia kibao kama Far Way utaelewa nazungumzia nini. Mashairi makali, video nzuri, anaimba vizuri, kazi yenye ubora wa hali ya juu kabisa.
Tafuta kazi zake nyingine za muziki kama On My Wedding Day, Rest of My Life na Imebaki Stori, utagundua kuwa Hemed ni mkali sana kwenye muziki.
MENEJIMENTI ZAIDI
Sina hakika kama anayo menejimenti, kama hana ni wakati wake, kama anayo inatakiwa kukaza zaidi. Mafanikio ya Diamond, pamoja na juhudi zake, nyuma kuna mameneja wakali waliogawana majukumu, wakiwa na lengo moja la kumfanya msanii huyo ang’ae zaidi.
Si rahisi kufanya kila kitu mwenyewe, akiwa na menejimenti imara, Hemed atazidi kuwa mkali kwenye filamu lakini pia ataendelea kuitendea haki fani yake ya muziki.
Akiwa na menejimenti ni rahisi kupata shoo zitakazokuwa zinamtangaza zaidi. Sina maana kuwa aachane na filamu, hapana… atapangiwa ratiba nzuri na kufanya majukumu yote kwa wakati mmoja.
Hemed ni mkali sana kwenye filamu, lakini namuona Hemed mkali zaidi kwenye Bongo Fleva! Kazi kwako kamanda Hemed. Cheza na miguu yote papaa!
Mtanzania