Jide, Mwarabu Wazua Utata
MKONGWE wa Bongo Fleva, Judith Wambura ‘Jide’ na Mwarabu mmoja ambaye jina lake halikuweza kupatikana mara moja, wamezua utata wa aina yake kufuatia msanii huyo ‘kumposti’ mara kwa mara kwenye mtandao wake wa Instagram.
Risasi Jumamosi lilianza kumfuatilia Jide baada ya kutonywa na chanzo kuwa msanii huyo amekuwa akimposti Mwarabu huyo na kwamba kuna kila dalili ni mtu wake aliyerithi mikoba ya aliyekuwa mumewe, Gardner Habash.
“Nyie kama vipi fuatilieni kwa makini kwenye Instagram yake, mtagundua tu ukweli, kuna kitu maana hata akimposti huyo jamaa huwa anaweka maneno yenye utata, hataki kufunguka moja kwa moja kama ni mpenzi wake au vipi,” kilisema chanzo hicho.
Baada ya chanzo hicho kulitonya Risasi Jumamosi, mwanahabari wetu aliingia kwenye ukurasa wa Jide na kuziona picha tofauti zikimuonesha akiwa amekaa na Mwarabu huyo huku akisindikiza na ujumbe ambao hautoi majibu ya moja kwa moja kama ni mtu wake au la.
Alipotafutwa mrembo huyo kupitia simu yake ya mkononi, iliita bila kupokelewa lakini mmoja wa mameneja wake alisema mwanaume huyo ni rafiki wa karibu wa Jide na kama kutakuwa na lolote, atafafanua baadaye.
“Ni rafiki yake tu na nisingependa kumtaja jina lake maana sidhani kama ni jambo zuri, nyie msiwe na wasiwasi, kila kitu kitakuwa wazi tu muda muafaka utakapowadia, najua watu wengi mnataka kumjua shemeji mpya, wawe wavumilivu tu watamjua,” alisema meneja huyo huku akiomba hifadhi ya jina.
Chanzo:GPL