Khadija Kopa Afungukia Kifo cha Taarab
Mkongwe wa muziki wa taarab, Bi. Khadija Omar Kopa amedai muziki wa wao unaonekana kama umepoteza ladha kwa sababu ya nyimbo zao kupigwa sana sehemu ya kuuza vilevi na kupotezewa katika vyombo vya habari.
Khadija amezungumza hayo akiwa kwenye uzinduzi wa video ya Saida Karoli ‘Orugambo na kusema kwamba muziki wa taarabu umeshushwa na watu wachache walioruhusu nyimbo zao kuchezwa ‘bar’ kitu kinachopelekea hata wapenzi wa muziki kususia matamasha yao yakiandaliwa.
“Muziki wetu umekosa thamani baada ya kuanza kupigwa kwenye ma- bar, unakuta nyimbo zinapigwa bar muda wote mtu ananua maji yake ya 1500 anasikiliza nyimbo anarudi nyumbani, saa ngapi atakuja kwenye show wakati bar anapata bure, lakini watu wa media nao wametupotezea sana kiasi kwamba wamefanya taarabu ni ya kipindi maalumu siyo kama bongo fleva au hip hop wao nyimbo zao zinapigwa kila muda, Wao ndio waliotufanya tujulikane lakini pia wao ndiyo wanatupoteza”, Khadija alisema.
Akizungumzia ujio wa Saida Karoli tena kwenye ‘game’ Khadija amesema sanaa ilimkosa mtu mwenye ladha ya asili kwa muda mrefu na ujio wake ni burudani kwa wasanii na wapenda muziki mzuri.
“Tulim-miss sana Saida sema wasanii tunajijua matatizo yetu, Uongozi ukiwa mbovu utakufanya upotee lakini ni vizuri amerudi tena na sisi tunamkaribisha, hapa tayari nimeshaweka mazingira ya kuweza kufanya kolabo. Naomba tumpe ushirikiano ule tuliokuwa tunamuonyesha zamani maana kipaji na uwezo wake unajionesha”, Khadija aliongeza