-->

King Majuto: Mastaa Wamenikaushia Bwana!

TANGA. JANA Alhamisi tulianza makala yaliyotokana na mahojiano maalumu na mwigizaji na mchekeshaji mkongwe nchini, Amir Athuman ‘Mzee Majuto’ ambaye alivumishiwa kifo, siku chache baada ya kuanza kuugua.

Amir Athuman ‘Mzee Majuto’

Mwanaspoti lilimwibukia mwigizaji huyo nyumbani kwake Donge, jijini Tanga na kumkuta katika hali inayotia tumaini na ndio maana aliweza kufanya mazungumzo yaliyozaa makala haya.

Mzee Majuto aliweka bayana namna alivyoanza kuugua na jinsi wazushi bila ya aibu walipomzushia kufa, ikiwa ni mara yao ya nne kitu alichodai kinamhuzunisha kuona wanadamu wanawaombea wenzao vifo badala ya uzima.

Je, Majuto anamfahamu aliyemzushia kifo safari hii na kama anamjua hatua zipi ambazo amezichukua dhidi ya mtu huyo na nini mtazamo wake kuhusu uwepo wa mitandao ya kijamii inayotumiwa vibaya na baadhi ya watu? Endelea naye…!

ALIYEMZUSHIA HUYU HAPA

Mzee Majuto anasema licha ya kuwa anaendelea kujiuguza na familia yake kuwa karibu naye kwa muda wote tangu kuugua kwake, lakini hakuacha kumsaka aliyevumisha taarifa za kifo chake na kuleta mkanganyiko.

Anasema tofauti na mara tatu za awali alivyovumishiwa kifo, safari hii zilifanyika jitihada za kumng’amua mhusika na kwa bahati walifanikiwa kumnasa kupitia mtandao wa facebook.

Anasema mzushi huyo ‘aliyemuua’ safari hii anafahamika kwa jina la Said Mbuzi, jina analotumia katika akaunti hiyo iliyobainika kutoa taarifa hizo.

“Watu wangu wa karibu na familia yangu, walifanikiwa kuona jina la Saidi Mbuzi ndio aliyeanzisha habari za kifo na aliposti katika mtandao wa Facebook alituma picha zangu za hospitali nikiwa nimefanyiwa operesheni na pembeni ameweka kaburi tena kaburi hilo ni la marehemu Sharo Milionea.”

HATUA GANI WALIZOMCHUKULIA?

Pamoja na kupitapita katika mitandao ya kijamii na kumgundua mtu huyo aliyezusha kifo cha Majuto, lakini mwigizaji huyo anasema wameshindwa kumchukulia hatua zozote za kisheria mpaka sasa kwa sababu ya kuumwa kwake.

Hata hivyo, anasema kazi hii ya uchunguzi na maamuzi ya kumchukulia hatua za kisheria ni kazi ya polisi, hivyo anaamini kama wanavyoshughulikiwa watu wengine wanaoenda kinyume na sheria za mitandao naye atashughulikiwa.

“Kama wale wanaofikishwa mahakamani kwa madai ya kuvunja sheria ya matumizi ya mitandao, mhusika huyo naye anapaswa kushughulikiwa na siyo yeye tu bali wote wenye tabia za kuwazushia watu vifo na kuleta usumbufu kwa familia zao.”

MITANDAO NI JANGA

Kutokana na taarifa za uzushi wa kifo kila wakati kwa watu tofauti kuenezwa katika mitandao ya kijamii, Mzee Majuto ameiomba Serikali kama ingewezekana mitandao hiyo ingefutwa kama hakuna udhibiti wa matumizi yake.

“Mimi naiomba Serikali kama inawezekana hii mitandao ya WhatsApp, Facebook, Instagram na mengine ingefutwa tu kama hakuna udhibiti, maana watu wanaitumia sivyo, Serikali inakaa kimya tu jamii inazidi kuangamia,” anasema.

“Kama watu wanafikia hatua ya kumuediti Rais na watu wengine wenye heshima zao, nini maana yake, lazima hivi vitu vidhibitiwe kwani tunaonekana tumeingia kwenye utandawazi tukiwa hatujajiandaa, hata kama ina faida zake,” anasema.

AWATOA HOFU MASHABIKI

Mkongwe huyo, amewatoa hofu mashabiki wake kuwa, wasiwe na wasiwasi juu ya hali yake ya ugonjwa, kwani anaendelea vyema.

“Pia wasidhani tatizo nililonalo ni gonjwa lisilotibika, hapana unatibika na ninaendelea vyema na In sha allah Mungu akipenda nitarejea tena kuwapa raha mara nitakapopona,” anasema.

MASTAA WENZAKE WAMKAUSHIA

Mzee Majuto anayeongoza kwa kucheza filamu nyingi nchini, anasema tangu ameanza kuumwa na hata alipozushiwa kifo ni wasanii wachache wenye majina ambao wamemjulia hali.

Anasema ni Mboto na Nisha pamoja na wasanii wengine wasio na majina ndio wamekuwa wakimtembelea ama kumpigia simu kujua hali yake, japo hamlaumu mtu.

“Nilijua swali hili ungeniuliza tu, ila ukweli wasanii waliofika hapa na wengine kunipigia simu tangu nianze kuumwa ni, Mboto ambaye alifika siku aliposikia taarifa za kifo, alikuwa wa kwanza kufika asubuhi asubuhi na wengine waliofika ni Nisha, Tausi, Manjonjo, Mizengwe walinipigia simu, wengine ni Korongo, Jengua na Ndimbo, nawashukuru kwa kunijali.” Licha ya kufahamika Mzee Majuto yupo karibu sana na mwigizaji Jacob Stephen ‘JB’ akiwa ameshirikiana naye filamu nyingi, lakini anasema ni kati ya waliomkaushia. “Sijawahi kujuliwa hali kwa kutembelewa ama kupigiwa simu japo ya salamu au pole na JB mpaka sasa,” anasema.

“Unajua siwalaumu sana hawa wasanii wanaojiita mastaa, kwani sijui wamepatwa na nini? Hata JB huenda ameghafirika tu, wakati mwingine hizi kazi za filamu zinakufanya uwe bize sana na bahati mbaya kwa sasa maisha kwao yamekuwa magumu, siwasemi vibaya ndio maana siwezi kuwalaumu sana,” anasema.

Pia anaongeza inawezekana JB amemkaushia ili wajiandae kumfanyia sapraizi kwa kumpelekea keki kwani mastaa wanapenda sana mambo ya kustukizana kama bethidei.

Je, unajua kuwa Mzee Majuto licha ya kuonekana mtu wa masihara, lakini ni shabiki mkubwa wa soka. Anashabikia timu zipi na sanaa yake ilianzia wapi mpaka kufika alipo? Ungana naye kesho Jumamosi kuhitimisha mahojiano yake.

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364