-->

Mzee Majuto: Nataka Nikifa Nizikwe Kama Steven Kanumba

Wiki hii, Mpaka Home ilifunga safari mpaka mkoani Tanga, nyumbani kwa mchekeshaji maarufu wa siku nyingi,  mzee Amri Athumani (68) ‘Mzee Majuto’ kwa lengo la kuyajua maisha halisi ya mchekeshaji huyu.

majuto00

Mzee Majuto akiwa na mjukuu (kushoto) pamoja na mtoto wake

Mzee Majuto anaishi eneo linaloitwa Donge, mkoani humo ambapo anaishi na familia yake nzima akiwepo mkewe kipenzi; Asha, watoto wake pamoja na wajukuu wake. Mcheshaji huyu ameyaweka wazi  maisha  yake halisi  kama ifuatavyo:

Mpaka Home: Kwa nini umeamua kuishi mkoani wakati mastaa wengi wanapenda kuishi Dar es Salaam?

Majuto: Mimi sipendi fujo kabisa, napenda kutuliza akili yangu sasa huko Dar ni vurugu tupu. Siwezi kukaa huko bora niishi hukuhuku atakayeniona mimi mshamba shauri yake.

Mpaka Home: Nimemuona mtoto mdogo hapa nimesikia akikuita baba kumbe bado unazaa?

Majuto: Kwa nini nisizae bado nina nguvu lakini kwa mke wangu si kwa mwanamke mwingine na wala siwezi kumkufuru Mungu kwa kukatiza kufanya hivyo.

Mpaka Home: Ulienda kuhiji Makha ni tofauti gani uliyonayo kabla hujaenda huko na baada ya kurejea?

Majuto: Tofauti ni kubwa sana kwa sababu nyumba yetu imekuwa ni nyumba ya ibada wakati wote na tunaishi kwa amani, ugomvi hakuna kama zamani.

Mpaka Home: Unapokuwa nyumbani unapenda mama akutayarishie nini?

Majuto: Napenda sana ugali wa muhogo na samaki ndiyo chakula changu kikubwa na ninakifurahia.

Mpaka Home: Kila mtu ana kitu chake kinachomvutia anapokuwa nyumbani kwake, wewe unavutiwa na nini?

Majuto: Napenda sana nikiwa nyumbani nikae jikoni na mke wangu tunapika na kupiga stori huku chakula kinaiva.

Mpaka Home: Hapana nyumbani nawaona watoto wengi sana wote ni watoto wako?

Majuto: Hapana wengine ni wajukuu zangu tena nawapenda sana.

Mpaka Home: Mara nyingi kumekuwa na tuhuma kuwa unapenda kuoa dogodogo angali una mke wako, vipi hilo?

Majuto: Jamani mimi wengine ni mashabiki zangu tu umri wangu huu natafuta nini tena jamani, siwezi maana unakuta wengine wanataka kupiga picha hivyo siwezi kukataa kupiga picha na mashabiki hata mara moja maana nataka siku nikizikwa na mimi nizikwe kama  Kanumba lakini hakuna kingine.

Mpaka Home: Nimeona umevuna mahindi, mihogo umeviweka hapa nyumbani vipi bado unalima?

Majuto: Kwanza mara nyingi mimi siishi hapa mjini naishi zangu shamba huko Kiruku, nje kidogo ya jiji kuna kila aina ya vitu ufugaji na bado nalima na pia nimejenga msikiti hukohuko shamba kwa ajili ya kuswali.

Mpaka Home: Ni kitu gani umefaidika katika kipindi chote cha uigizaji wako?

Majuto: Unajua mimi nimefanya mambo mengi kupitia jitihada zangu inawezekana ningekuwa mbali sana lakini watu wengi wamenidhulumu jasho langu ila kwa vile sipendi kumdai mtu nimemuachia Mungu maana ningeweza hata kuwa msanii wa kwanza kwa utajiri hapa Tanzania. Hivi nilivyonavyo, nyumba na mambo mengine ni vitu vidogo tu.

Mpaka Home: Nini kinakufurahisha unapokuwa nyumbani kwako?

Majuto: Ni familia yangu na kuwa karibu na mke wangu.

Mpaka Home: Ni kitu gani  unatamani kiwe hapa nyumbani kwako na hakipo?

Majuto: Natamani sana nyumba yote iwe imezungukwa na miti  maana napenda sehemu yenye hewa safi na nzuri. Nitapanda.

Chanzo:GPL

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364