Mambo 10 ya Kukumbukwa 2016
ZIMEBAKI takribani siku saba kabla ya mwaka huu kufikia ukingoni na kuukaribisha mwaka mpya wa 2017. Kwa hakika mwaka 2016 umekuwa wa matukio mbalimbali kwenye tasnia ya burudani Bongo.
Kwa wiki tatu sasa mfululizo tumekuwa tukikuletea matukio tofautitofauti yaliyopata kutokea tangu kuanza kwa mwaka huu. Tayari tumeshaona mastaa waliofunga ndoa, ndoa zilizovunjika na mabifu yaliyotingisha.
Leo ikiwa ni toleo maalum la kufungia mwaka kwa Swaggaz ya Mtanzania, tunakuletea matukio muhimu zaidi kumi yaliyopata kutingisha kwa mwaka huu katika maeneo mbalimbali katika burudani.
WASTARA, SADIFA
Mastaa kadhaa walifunga ndoa (kama tulivyoona kwenye mfululizo wa matukio haya ya kukumbukwa) akiwemo mwigizaji Wastara Juma aliyefunga ndoa na Mbunge wa Donge, Sadifa Khamisi Juma lakini ndoa hiyo ilivunjika miezi michache baadaye.
Si ndoa ya Wastara pekee iliyovunjika mwaka huu, lakini ni kati ya ndoa iliyozungumzwa zaidi kuvunjika kwake kwenye mitandao mbalimbali ya kijamii na magazetini.
MZEE YUSUF KUSTAAFU MUZIKI
Aliyekuwa mfalme wa muziki wa Taarab Bongo, Mzee Yusuf mwaka huu aliamua kuacha kufanya muziki na kumrudia Mwenyezi Mungu.
Alifikia uamuzi huo Agosti 12, mwaka huu kabla ya kwenda kuhij Makka ili kutimiza moja kati ya Nguzo Kuu za Kiislam. Pia Mzee alimtaka mkwe Leila Rashida, naye kuacha kufanya muziki ikiwa ni pamoja na kuzuia vituo vya redio na televisheni visipige nyimbo zake.
SANAA KURASIMISHWA
Mwaka 2016 umekuwa mwaka wa neema kwa tasnia ya sanaa nchini ambapo Rais Dk. John Magufuli, Desemba 10, 2015 aliamua kuiingiza sanaa katika Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo, hivyo kuirasimisha kama kazi inayotambulika.
Wizara hiyo ipo chini ya Nape Nnauye, ambayo licha kurasimishwa mwaka jana lakini kwa kiasi kikubwa imeanza kufanya kazi mwaka huu. Rais Magufuli, aliwaalika wasanii Ikulu jijini Dar es Salaam na kujadilina nao masuala mbalimbali kuhusu sanaa nchini.
NDOA YA MASANJA
Ndoa nyingi za wasanii zilifungwa mwaka huu lakini ndoa ya komediani maarufu katika Kundi la Origino Komedi, Emmanuel Mgaya ‘Masanja Mkandamizaji’ imekuwa ndoa ya mwaka hasa kutokana na kuzungumzwa na kuandikwa zaidi.
Upekee wa Masanja unatokana na hatua yake ya kuvaa suti tatu tofauti siku ya ndoa yake. Kanisani alivaa nyingine, wakati wa kupiga picha na baadaye ukumbini katika hafla iliyohudhuriwa na viongozi mbalimbali wa vyama na serikali wakiongozwa na Naibu Spika, Dk. Tulia Ackson.
Katika hatua nyingine, wasanii wa Origino Komedi – Joti, Seki, na Wakuvanga walikamatwa na kuhojiwa na Jeshi la Polisi, Kanda Maalum ya Dar es Salaam kwa kosa la kuvaa sare za jeshi hilo bila kibali katika harusi hiyo.
MWAKA WA DARASSA
Umekuwa mwaka wenye mafanikio makubwa katika tasnia ya muziki wa Bongo Fleva nchini, huku wakiwaacha mbali sana wasanii wa Bongo Muvi ambao walikuwa kileleni kimafanikio kwa muda mrefu.
Wasanii chipukizi walipata nafasi, wakongwe wakafurukuta kutaka kurudi kwenye nafasi zao, huku wale vinara wakionyeshana kazi.
Lakini mwisho wa siku mkali Darassa akafunga kazi. Dalili za Darassa kufanya vizuri zilianza kuonekana tangu mwanzoni mwa mwaka alipoachia Kama Utanipenda na baadaye Heya Haye, kisha Too Much. Lakini mwisho wa yote ni pale alipotoka na Muziki a.k.a Wimbo wa Taifa unaotingisha kila kona.
Unaitwa ‘Wimbo wa Taifa’ kutokana na namna ulivyokiki kila kona ya nchi na kuwa wimbo unaopigwa zaidi hivi sasa.
WATANGAZAJI WAPANDA BEI
Ulikuwa mwaka wa neema kwa watangazaji nchini. Kwa muda mrefu ilielezwa kuwa tasnia ya utangazaji Bongo imekuwa ikichukuliwa poa kwa watangazaji kulipwa kiduchu huku wakitegemea madili yao mengine, lakini mwaka huu tumeshuhudia mapinduzi makubwa.
Kufunguliwa vituo vya Azam TV, TV 1 na Radio E FM kulileta changamoto kubwa ya kunyang’anyana watangazaji na hivyo kuipaisha tasnia hiyo.
Usajili ulikuwa na mvutano mkubwa, lakini matukio makubwa zaidi ni Gardner Habash kung’olewa E FM alipokuwa akiendesha Kipindi cha Ubaoni na kurejea Clouds FM kwenye Kipindi cha Jahazi ambazo alikiasisi yeye miaka kadhaa iliyopita.
Kabla ya Gardner kwenda Clouds, walianza watangazaji nyota wa Power Breakfast, Gerald Hando, Paul James ‘PJ’ na Abel Onesmo kuvutwa Radio E FM ambapo waliingia kwenye Kipindi cha Joto la Asubuhi.
Hata hivyo baadaye Clouds walifanikiwa kumrejesha tena nyumbani, mchambuzi mahiri wa magazeti PJ kuungana na Barbara Hassan, Fred Fidelis na Masoud Kipanya aliyerejea Clouds.
MWAKA WA WCB
Tumeshuhudia ongezeko kubwa la mastaa wakianzisha lebo za muziki, lakini ubora wa Wasafi Classic Baby (WCB) umeendelea kudhihirika siku baada ya siku.
Mwaka 2016, umekuwa mwaka wa mafanikio kwao. Matukio mengi ya kiburudani yaliyojiri yamekuwa yakiuhusisha WCB kwa namna moja ama nyingine.
Juni pili, mwaka huu haiwezi kusahaulika kabisa. Uzinduzi mkubwa wa lebo hii ulifanyika kwa mara ya kwanza na kutambulishwa kwa msanii Rich Mavoko sambamba na ngoma iliyoambatana na video matata ya Ibaki Story.
Mpaka hivi sasa ina wasanii wanne – ni Rayvanny, Harmonize, Queen Darleen, Rich Mavoko na Diamond Platnumz mwenyewe ambao wote mafanikio yao yanaonekana.
WCB imemrudisha kwenye ramani Dully Sykes kupitia Inde, ngoma iliyosimamiwa na Harmonze. Chid Benz pia hawezi kusahau msaada aliopewa na WCB japokuwa haukufua dafu kuweza kumtoa kwenye dimbwi la utumiaji madawa ya kulevya.
Mafanikio ya nyimbo za wasanii wake ndani na nje ya nchi yanaonekana. Chati mbalimbali za muziki barani Afrika zimepambwa na nyimbo za wasanii wa lebo hii.
KIBA KURUDISHIWA TUZO
Haikuwahi kutokea tangu Bongo Fleva ianze kupata mashiko kwenye jamii. Novemba 10, haiwezi kusahaulika pale uongozi wa Tuzo za MTV EMA zilizofanyika huko Rotterdam, Uholanzi kutangaza kuitoa kimakosa Tuzo ya Msanii Bora Afrika iliyokwenda kwa Wizkid.
Tuzo ikarudishwa Tanzania, Ali Kiba ndiye aliyestahili kuipata kwa kuwa ndiye aliyeongoza kwa kupigiwa kura nyingi kuliko msanii yoyote yule. Ilikuwa shangwe na kelele za kutosha kwenye mitandao ya kijamii ambapo Team Kiba walikinukisha baada ya msanii wao kunyimwa tuzo yake.
Ilikuwa heshima kwa taifa pia katika anga za burudani.
RUBY ACHOMOA DILI LA FIESTA
Mwezi Agosti, staa wa singo ya Na Yule, Ruby alitikisa vyombo vya habari mara baada ya kutangaza kutotumbuiza kwenye matamasha ya Fiesta kwa madai ya malipo kiduchu.
Kitu kilichovuta hisia zaidi za watu ni pale alipoanza kuonekana kwenye matamasha yanayoandaliwa na wapinzani kibiashara na watu waliomuibua yaani Clouds Media Group kupitia Shindano la Super Nyota.
SINGELI YATUSUA
Ngoma kali kama Hainaga Ushemeji, Ghetto na nyingine nyingi za wasanii wa Singeli mwaka huu ndiyo zimefanikiwa kupeta kitaa, kuanzia uswazi mpaka ushuwani.
Heshima ya wasanii wa Singeli imepanda maradufu, muziki wao ni bidhaa tamu kwenye masikio ya mashabiki, imefika hatua ya mkongwe wa Hip Hop, Profesa Jay kuamua kuchanganya ladha na kupata Hip Hop Singeli, siyo mchezo aisee. Hiyo ni dalili nzuri kwao kwa mwaka ujao.
Chanzo:Mtanzania