Mastaa wa Kike Kutoka Familia za Mboga Saba
NAIJUA familia ya mboga saba? Wengine wanapenda kuwaita watoto wa kishua ama familia bora. Hii ikiwawakilisha watoto wanaozaliwa kwenye familia yenye uwezo mkubwa wa kiuchumi, kiasi cha kutumia mlo mmoja ukiwa na mboga tofauti na zinazobadilishwa kila uchao. Ndio, kuna familia nyingine bhana mlo unakuwa na mboga moja na huwa ni hiyo hiyo deile mpaka inachosha.
Ingawa kuna dhana kuwa watoto wa kishua huwa wavivu kujitafutia kwa sababu kila anachokotaka hukipata tu nyumbani, lakini ukweli sio wote. Kuna wengine wanaamua kuchakarika kutafuta maisha yao wenyewe, hata hawalingani na wale waliotokea familia za watu duni ambao walikatisha masomo ili kusaka noti wakiwa kwenye umri mdogo kabisa.
Mwanaspoti inakuletea baadhi ya mastaa wa kike waliozaliwa kwenye familia ya mboga saba, lakini wanakomaa kivyao vyao ile mbaya wakijichanganya na wenzao kusaka noto kwa jasho na damu.
VANESSA MDEE
Vanessa Mdee maarufu kama Vee Money alizaliwa mjini Arusha mwaka 1988. Vanessa anatokea familia bora ya Sammy Mdee ambaye kwa sasa ni marehemu. Enzi za uhai wake, baba ya Mzee alikuwa mtu mzito kwenye nchi hii akiwa mume wa Sophia.
Akiwa na umri mdogo Vanessa aliweza kusafiri nchi mbalimbali duniani. Vanessa Mdee alikulia miji ya New York , Paris, Nairobi na Arusha, lakini kwa sasa jamaa anatisha mbaya kwenye fani ya muziki akitamba ndani na nje ya Afrika.
JOKATE MWENGELO
Huyu unaweza kumuita mtoto wa Oysterbay kwani ndio alipokulia huku baba yake akifanya kazi serikalini.
Kumbuka Jokate alizaliwa Washington DC, Marekani ambapo wazazi wake walikua wakifanya kazi huko. Alipomaliza masomo ya juu ya Sekondari pale Loyola ndipo alipoanza kujichanganya kwa kuwania taji la Miss Tanzania mwaka 2006 na kushika nafasi ya 2 nyuma ya Wema Sepetu, kisha kuhamia kwenye fani ya muziki, utangazaji, mitindo na ubunifu na sasa akipiga fedha.
WEMA SEPETU
Wema Sepetu ni msichana anayetoka kwenye familia ya kibalozi akiwa ni mtoto wa mwisho katika familia ya wasichana wanne wa marehemu Balozi Isaac Sepetu.
Wema alizaliwa mwaka 1988 katika hospitali ya St. Andrew ya Dar es Salaam na amesoma elimu yake ya awali mpaka sekondari kwenye Shule ya Academic International iliyopo Dar es Salaam kabla ya kwenda Malaysia kusomea mambo ya biashara za kimataifa katka Chuo Kikuu cha Limkokwing.
Alianzia shindano la urembo akitwaa mataji kadhaa ikiwamo la Miss Tanzania 2006 kisha kuhamia kwenye filamu na sasa anaendelea kukimbiza akimiliki kampuni yake na akizalisha bidhaa zenye jina lake. Achana kabisa, ila ukiamua kubisha we bisha tu.
Mwanaspoti