-->

Mboto Afungukia Kuhusu Kutoka na Aunt Ezekiel

KAMA kawa Mtu Kati ipo ‘live’ leo tena, ambapo baada wiki iliyopita kukuletea mwanadada mkongwe anayefanya vizuri kwenye Tasnia ya Filamu Bongo, Halima Yahaya ‘Davina’ wiki hii inakusogezea mvunja mbavu mwenye jina kubwa katika ardhi ya JPM, Haji Salum ‘Mboto.’

mboto043

Mboto akiwa na Aunt Ezekiel

Huyu ni mchekeshaji mkongwe kidogo aliyeanzia sanaa yake katika Kundi la Kaole Sanaa Group mwishoni mwa miaka ya tisini, akiigiza na kina Max (marehemu), Zembwela, Bambo na wengine wengi.
Kuhusu mafanikio, maisha binafsi, anatoka na staa na demu wa aina gani pamoja na mengine mengi ambayo huyafahamu kutoka kwa mkali huyu, katika Mtu Kati ya leo anafunguka kila kitu, tena kwa kujiachia, ungana naye;

Mtu Kati: Mashabiki wako wangependa kufahamu matumizi yako ya pesa kwa siku yanakuaje? Unatumia kama shilingi ngapi?
Mboto: Siku hazilingani, inategemeana siku hiyo nitakuwa nahitaji kupata mahitaji gani. Kwa hiyo sina kiwango kamili ambacho naweza kusema huwa ninatumia, lakini kama unavyofahamu maisha ya Bongo ni ghali kwa hiyo mfuko huwa unatoboka sawasawa.

KUOA VEPEE?
Mtu Kati: Umeoa na una watoto wangapi?
Mboto: Ahhaaa haaa! Bado sijaoa, ila niko mbioni kufanya hivyo kuhusu mtoto ndiyo ninaye mmoja tu.
Mtu Kati: Miaka miwili nyuma umewahi kufanya mahojiano na sisi na ukadai kuwa uko mbioni kuoa lakini mpaka sasa bado upoupo, imekaaje hapo?
Mboto: Ni kweli lakini ndiyo kujipanga kwenyewe, miaka miwili nyuma si mingi, sihitaji kukurupuka juu ya hili ndiyo maana nafanya mambo taratibu.

FILAMU ZINAMLAZA NJAA!!
Mtu Kati: Vipi, kutokana na mdororo wa kiwanda cha filamu Bongo, pesa unayopata kwa kuuza filamu inajitosheleza kumudu mahitaji yako?
Mboto: Ndiyo inajitosheleza. Unajua japo soko limedorora inategemeana na muvi unatengenezaje, kwa hiyo kwa upande wangu ninatengeneza muvi bora ambazo zinapata soko na kuniingizia mkwanja.
Mtu Kati: Muvi gani ambayo imekuingizia mkwanja kuliko zote?
Mboto: Nampenda Mke Wangu, iliuza sana lakini siwezi kutaja iliniingizia shilingi ngapi.
Mtu Kati: Kwa muvi unaigiza kwa shilingi ngapi na kwenye nyimbo vepe?
Mboto: Kwenye muvi naanzia kuchukua shilingi milioni 3 na kwenye nyimbo naanzia laki tatu.

KUBANJUKA NA AUNT EZEKIEL JE?
Mtu Kati: Kuna madai kuwa huwa unatumia ukaribu wako na Aunt Ezekiel kubanjuka naye na si kuigiza hiyo vepe?
Mboto: Ha! Ha! Haaa! Hayo madai hayana ukweli, Aunt ni mtu wangu wa karibu, nampenda sana kwa sababu ni mtu ambaye tumefanya kazi nyingi na tunaelewana!
Mtu Kati: Huo ukaribu wenu vepe?
Mboto: Ni wa kazi tu, halafu kitu ambacho watu hawakijui, Aunt anafahamu udhaifu wangu wote na mimi ninafahamu tunapokuwa kwenye kazi. Kwa hiyo kuna muda unakuta tunapokuwa lokesheni naweza kusahau kitu yeye akanikumbushia katika mwendelezo bila mtu yeyote kufahamu, na mimi hivyohivyo.

KAPITIA WAREMBO KIBAO BONGO MUVI?
Mtu Kati: Inasemekana pia miongoni mwa wasanii viwembe, wewe pia umo. Kwamba umepitia warembo wengi Bongo Muvi!
Mboto: Si kweli. Sijawahi kuwa hata na mmoja wao. Mimi ni mtu ambaye sipendi kuwa na mpenzi sehemu ninapofanyia kazi, kwa hiyo madai hayo ni ya uongo.
Mtu Kati: Kwani mpenzi wako ni wa aina gani?
Mboto: Mwanamke wa kawaida tu ambaye hata hayupo kwenye sanaa, anapenda kuwa mtazamaji tu na anafanya ishu zake zinginezingine.

HEE! ANAIKUMBUKA IVETA?
Mtu Kati: Kati ya nyimbo nyingi ulizoigiza, wimbo gani unaukubali kazi uliyoifanya?
Mboto: Iveta ya Sajna. Unajua wakati ule teknolojia ilikuwa chini, lakini jambo la kufurahisha ile kazi ilikuwa bora na ilitokea kupendwa mno hapa Bongo na Afrika Mashariki kwa jumla. Hata hivyo, kazi nyingine ni kazi ya Tunda Man iitwayo Mama Kija.

WANAWAKE WANAMSHOBOKEA?
Mtu Kati: Wewe ni mtu maarufu, upande wa usumbufu kutoka kwa kina dada vepe?
Mboto: Usumbufu upo, hata hivyo nafahamu namna ya kukabiliana nao.
Mtu Kati: Ushawahi kutongozwa na mrembo yeyote Bongo Muvi?
Mboto: Mmmmh! Hapana!

MAFANIKIO NAYO?
Mtu Kati: Mpaka sasa umevuna nini kwenye sanaa?
Mboto: Mambo mengi. Umaarufu unaonisaidia kwenye biashara zangu. Nina vyombo vya usafiri barabarani vinavyopiga kazi ambavyo sidhani kama kuna umuhimu wa kuvitaja, naendesha maisha yangu na mambo mengine mengi.
Mtu Kati: Lolote kwa wapenzi wa kazi zako.
Mboto: Wazidi kunipa sapoti, sitawaangusha.

Chanzo:GPL

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364