-->

Mafanikio ya Wema Sepetu Miaka 10 ya Ustaa

SHINDANO lenye umri wa miongo miwili na tayari limeshatoa warembo kibao, lakini ukweli usio na shaka ni lile shindano la mwaka 2006 lililokuwa na mvuto wenye ladha iliyobeba msisimko wa kipekee.

Wema Sepetu mwaka 2008

Ni fainali zilizompa Wema Sepetu heshima ya kuwa Miss Tanzania. Lakini pia ni mwaka ambao umewatoa mastaa wengi wa Bongo. Mbali na Wema, wapo Jokate Mwegelo, Lisa Jensen na Irene Uwoya.

Kipimo cha ukubwa wa jina na hadhi yake unaweza kupimwa kwa mambo mengi ila wingi wa mashabiki wanaomfuata katika mitandao ya kijamii inaweza kuwa ni kipimo sahihi.

Instagram pekee ana watu zaidi ya Milioni 2.5 idadi ambayo hakuna staa yeyote wa kike Bongo ameifikia.

Katika kipindi hiki cha miaka kumi ya ustaa wa Wema, amefanya mengi makubwa na ya kujivunia. Ukiacha kutunza ustaa wake, jambo ambalo wengi wameshindwa, hapa chini Swaggaz inakuchambulia mafanikio yake akiwa staa wa Bongo katika fani mbalimbali ndani na nje ya urembo.

 FILAMU

Baada ya kupata ushindi mnono kutoka kwenye shindano la Miss Tanzania, Wema Sepetu aliitazama fursa iliyopo kwenye kiwanda cha filamu Bongo.

Wema Akiwa Kwenye Moja ya Filamu Alizocheza

Kipaji kilichomuwezesha kuvaa uhusika wa kile kilichopo kwenye script kiliifanya Kampuni ya Game 1st Quality ya jijini Dar es Salaam, ikampa nafasi ya kucheza filamu yake ya kwanza iitwayo A Point of No Return, ambapo mhusika mkuu alikuwa ni marehemu Steven Kanumba, hiyo ilikuwa mwaka 2007.

Kazi hiyo ilimtambulisha vyema kwenye ulimwengu wa filamu. Zikafuata nyingine kama Family Tears (2008) Red Valentine, White Maria na nyinginezo zilizotolewa na Game, chini ya Mtitu Game.

Baadaye wadau wengine wakamshirikisha kwenye sinema zao, akiwemo staa wa Bongo Muvi, Jacob Stephen ‘JB’ kwenye 14 Days, Dj Ben, Chungu cha Tatu, Lerato, Basilisa, House Boy, It Was Not Me, Mapenzi Yamerogwa, Saa Mbovu na nyingine nyingi.

Idadi ya sinema alizoshiriki ni kubwa na kwa sehemu kubwa amefanya vizuri, akishirikiana na washiriki wengine, ambapo mara nyingi hucheza kama mhusika mkuu au mhusika mkuu msaidizi.

 AZINDUA ENDLESS FAME FILMS

Hakuishia kucheza filamu za watu pekee, bali alikuwa na kiu kubwa ya kuzalisha filamu zake mwenyewe.

Februari, 2013 mrembo huyu alifungua Kampuni ya Endless Fame Films, akiwa na dhumuni la kuzalisha filamu zake na za wasanii wenzake, kuibua na kukuza vipaji vipya na kuongeza ubora kwenye kazi za sanaa kwa ujumla.

Kupitia kampuni hiyo aliweza kulitikisa soko la filamu pale alipoachia filamu yake ya kwanza iitwayo Madame.

Filamu hiyo ilimpa nguvu ya kuvuka mipaka ya Tanzania na kutua Accra, Ghana kukutana na staa wa filamu mwenye heshima kubwa Afrika, Van Vicker.

Lengo la kumsaka Van Vicker ni kulitanua soko la filamu Tanzania hasa pale filamu yao inayoitwa Day After Death itakapoingia kitaa.

Hakuishia kwenye filamu pekee bali amewahi kumiliki wasanii wa Bongo Fleva, Mirror na Jordan waliokuwa wanaunda Kundi la Danger Vuu lililokuwa linapewa sapoti na marehemu Albert Mangwea.

‘IN MY SHOES’ YAMPA HESHIMA

Mwaka 2014  ulikuwa na neema kwake kwani aliamua kuweka hadharani kila hatua anayoipiga kwenye maisha yake. Alimua kutuletea In My Shoes, kipindi cha runinga kinachoonyesha maisha yake kama staa.

Watu wengi walipata kumfahamu zaidi na kiukweli alijiweka karibu zaidi na mashabiki hasa wale ambao walikuwa wanapenda kazi zake.

 ‘KISS BY WEMA’ NI BALAA KITAA

Wema si mwepesi wa kukubali kushindwa licha ya ukweli kwamba maadui anao wa kutosha, Novemba Mosi, 2015 kwa mara nyingine alionyesha jinsi anavyoweza kunyumbulika, hapa sasa alitutupa kwenye ujasiriamali.

Aliingiza mzigo wa lip stick zenye jina la ‘Kiss by Wema’ na kwa muda mfupi zilisambaa kitaa kufuatiwa kugombaniwa na warembo wenye mapenzi ya dhati na mnyange huyu.

AJISONGEZA ZAIDI KWA MASHABIKI

Mei 22, mwaka jana alijiongeza kibiashara ili kuwa karibu na mashabiki ambao mara kwa mara wamekuwa wakipokea taarifa zilizopotoshwa juu yake.

Akawaletea mashabiki huduma ya kupata habari zake kupitia simu za mkinoni inayoitwa ‘Wema Sepetu Mobile Application’.

MAFANIKIO NI YAKE

Hivi sasa ana miaka kumi kwenye tasnia ya burudani. Hakuna aliyeweza kuvunja rekodi ya kuubeba ustaa kwa muda wote huo bila kupungua.

Kwa maana hiyo, Wema bado ana nafasi kubwa ya kuendelea kutengeneza fedha zitakazomfanya aishi kistaa kulingana na hadhi yake ilivyo.

Bado ana nafasi zaidi, ni suala la ubunifu zaidi na kutambua thamani yake kama staa mwenye heshima Bongo. Kazi ni kwake.

Wiki ijayo tutawaletea maoni ya wadau mbalimbali wa sanaa Bongo, wanavyozungumzia mafanikio yake.

Na Christopher Msekena-Mtanzania

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364