-->

Mtanzania Ashinda Tuzo ya Filamu za Kigeni Marekani

SOKO la filamu za Tanzania limezidi kujitangaza nje ya nchi baada ya Filamu ya ‘Daddy’s Wedding’ iliyoongozwa na Mtanzania, Honeymoon Aljabri, kushinda tuzo ya filamu bora ya kigeni katika tamasha la filamu za kimataifa lililofanyika juzi katika Hoteli ya Double Tree mjini Houston Marekani.

Honeymoon ambaye pia ndiye prodyuza wa filamu hiyo, alisema furaha yake kubwa ilikuwa ni kuitangaza vema tasnia ya filamu nje ya nchi jambo ambalo anaona amefanikiwa katika tuzo hiyo muhimu itakayosaidia kukuza tasnia ya filamu kwa kuongeza chachu kwa waongozaji na maprodyuza wengine kufanyakazi bora na kuzishindanisha katika matamasha mbalimbali ndani na nje ya nchi.

Muongozaji-bora-wa-filamu-Honeymoon

Katika tamasha hilo filamu zaidi ya 5,000 zilishirikishwa lakini filamu 74 tu ndizo zilizofanikiwa kuonyeshwa kwenye tamasha hilo lililokamilika Jumapili.

Tamasha hilo lilianzishwa miaka 49 iliyopita katika umri huo mkubwa kuliko matamasha yote ya Marekani, baadhi ya waongozaji wenye majina makubwa wa filamu duniani waliowahi kushinda tuzo katika tamasha hilo ni George Lukas, Steven Spielberg, Ang Lee na Jonathan Damme.

Filamu hiyo iliyochezwa katika mbuga ya wanyama ya Saadani na kuandaliwa na kampuni ya True vision & motion art production ya Texas, Marekani, washiriki wake ni pamoja na mwandishi mkongwe na mchambuzi wa masuala ya siasa, Jenerali Ulimwengu, mwanamuziki Banana Zorro, mchora katuni, Nathan Mpangala, mkurugenzi wa kampuni ya PR Tabasam Lucy Ngongoseke, waigizaji, Mama Abdul, Natasha na binti yake, Monalisa pamoja na waigizaji wengine wasio na majina makubwa.

Tasnia hiyo pia imejitangaza vema nje ya nchi kupitia kwa filamu mbalimbali zilizoshirikishwa katika baadhi ya matamasha hayo na kushinda ambapo mwigizaji, prodyuza na mwongozaji wa filamu nchini, Omary Clayton, aliibuka kidedea katika kipengele cha msanii bora wa kiume kwenye tuzo za California Online Viewers Choice Awards (COVCA) zilizotolewa nchini Marekani.

Pia waigizaji, Elizabeth Michael (Lulu) alishinda tuzo kupitia filamu yake ya ‘Mapenzi ya Mungu’ kipengele cha Filamu bora Afrika Mashariki ‘Best Movie- Eastern Africa’ na Single Mtambalike ‘Richie’ kushinda tuzo ya filamu bora ya Kiswahili, ‘Best Indigenous Language Movie/Tv Series-Swahili’ kupitia filamu yake ya ‘Kitendawili’.

Mtanzania

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364