Muna Afungukia Madai ya Kumuingiza Wema Kwenye Madawa ya Kulevya
Mrembo aliyewahi kufanya vyema kwenye tasnia ya maigizo Bongo, Rose Alphonce ‘Muna’, amefungukia madai ya watu kumtuhumu kuwa amemwingiza shosti wake Wema Sepetu ‘Madam’ kwenye matumizi ya madawa ya kulevya kwa kusema madai hayo hayana ukweli.
Akizungumza na paparazi wetu, Oktoba 5, mwaka huu, Muna alisema mbali na kumhusisha kumwingiza Wema kwenye madawa hayo, amekuwa pia akituhumiwa kuwa yupo kwenye orodha ya wabeba unga jambo ambalo halina ukweli wowote na kwamba watu wanajaribu kumharibia sifa yake kwa kuwa tu yupo karibu na Madam.
“Sijamuingiza Wema kwenye matumizi ya madawa ya kulevya kama watu wanavyosema, mimi mwenyewe sijawahi kujihusisha na biashara hiyo wala kuwa kwenye matumizi ya dawa hizo.
“Wasifikirie ukaribu wangu na Wema ndiyo eti naweza kumfundisha vitu vya ajabu, kwanza Wema hajawahi kutumia wala kujihusisha na matumizi ya aina yoyote ile ya madawa ya kulevya na kama angekuwa anatumia dawa hizo, angekuwa ameshaharibikiwa.
“Mimi nina kampuni yangu (hakuitaja jina) najitahidi kuikuza kila siku ili tuweze kusonga mbele. Hata ninaposafiri mara nyingi ni kwa ajili ya kampuni yangu.
“Halafu kwanza Wema nimefahamiana naye akiwa mtu mzima na wala hakuwa mtoto hivyo suala la mimi kumuingiza kwenye mambo maovu siwezi zaidi najitahidi kumfanya awe mfanyabiashara mzuri ndiyo maana utaona siku hizi kila kukicha tunajitahidi kubuni shoo mbalimbali za kutuingizia kipato,” alisema Muna.
Kwa muda mrefu Muna amekuwa akitajwa kwenye biashara ya madawa ya kulevya huku madai hayo yakichagizwa na safari zake za mara kwa mara nje ya nchi zisizofahamika kwa haraka na kama haitoshi, mrembo huyo amekuwa akidaiwa kumfundisha Wema kuvuta ‘unga’ jambo ambalo Muna amesema halina ukweli wowote.
Chanzo:GPL