Mwana FA Awataja Hawa Ndiyo Wasanii Wake Bora wa Hip Hop Bongo
Mwanamuziki Mwana FA amefunguka na kuwataja wasanii wawili ambao yeye siku zote amekuwa akiwakubali kutokana na uwezo wao na kazi kubwa waliyoifanya katika muziki wa Hip Hop Tanzania kiasi cha kuwafanya watu waamini muziki huo siyo uhuni bali ni kazi.
Mwana FA kupitia kipindi cha Friday Night Live (FNL) kinachorushwa na EATV alisema Professor Jay pamoja na marehemu Albert Mangwea ndiyo wasanii wake wawili bora wa siku zote katika muziki wa Hip hop Tanzania.
“Wasanii wangu bora kwa kipindi chote kwenye muziki wa Hip hop ni marehemu Albert Mangwea pamoja na Professor Jay hiyo nasema na kuna siku nilishawahi kuandika hilo, mpka Professor alinipigia simu na kuniuliza mzee una nini unataka kufa nini?. Watu hawajui tu huyu Professor Jay kwanza ndiyo mtu aliyefanya muziki wetu huu kwanza uanze kuheshimiwa, mwanzoni nyimbo zilikuwa na ujumbe wa fujo fujo fulani, kwa hiyo muziki wetu ulikuwa hauchukuliwi ‘serious’ lakini baada ya chemsha bongo kila kitu kikabadilika” alisema Mwana FA
Mbali na hilo Mwana FA alisema kuwa Professor Jay ni msanii ambaye alifanya yeye kidogo aache muziki sababu Mwana FA alikuwa anataka kufanya muziki bora lakini alipokuwa anasikiliza kazi za Professor Jay akaona hawezi kufanya kazi bora kama hizo.
“Unajua mimi siku zote huwa nataka kuwa best kwa kile nachofanya sijui kwa wasanii wengine, sasa baada ya kusikia ngoma ya Professor Jay ‘Chemsha bongo’ mimi nina nyimbo zangu nilikuwa nimeandika nikarudi nyuma nakajiuliza sasa mimi nawezaje kuwa ‘best’ kwa ngoma hizi? Yaani alinikatisha tamaa lakini nikarudi na kuanza kujipanga upya” alisema Mwana FA