Mzee Chillo Alia na Wataalamu wa Afya Muhimbili
MSANII nguli wa Filamu za Kibongo, Ahmed Olotu, ‘Mzee Chillo’ jana aliwafungukia baadhi ya wataalamu wa afya wa Chuo Kikuu cha Muhimbili (University of Health and Allied Sciences), jijini Dar, kuachana na mambo ya rushwa ili kuwafanya wananchi kuwa na imani nao.
Mzee Chillo alisema hayo kwenye Warsha ya Kilangi For Youth Academic Social Premier, iliyoandaliwa na Mfamasia, Archman Kilangi iliyofanyika jana kwenye Ukumbi wa Semina wa Environment uliopo chuoni hapo, ambapo aliwasisitiza kuisafisha sekta hiyo kutoka na kuchafuka kwa rushwa.
“Niwasihi kama mzazi wenu, kama mgeni rasmi, mnapomaliza chuo mnapaswa mkaitumikie vyema jamii yenu, kazi yenu ni wito, kataeni rushwa ya ngono, rushwa ya pesa, kujuana, wizi wa dawa na nyinginezo. Mkifanya hivyo mtaifanya jamii iendelee kuwaamini tena, kwani rushwa inawaharibia,’’ alisema Mzee Chillo.
Warsha hiyo iliwakutanishwa wahudhuriaji zaidi ya hamsini wakiwemo wataalamu wa afya mbalimbali kama wafamasia, wauguzi, madaktari na wadau kutoka sekta tofauti.
Na Gabriel Ng’osha/GPL