-->

Nay wa Mitego Afungiwa na Kupigwa Faini

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limemfungia kwa kipindi kisichojulikana msanii wa muziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki maarufu kwa jina la Nay wa Mitego.

nay987

Nay wa Mitego

Baraza la Sanaa la Taifa (BASATA) limemfungia kwa kipindi kisichojulikana msanii wa muziki wa kizazi kipya Emmanuel Elibariki maarufu kwa jina la Nay wa Mitego hadi hapo litakapojiridhisha kwamba ametekeleza maagizo yote aliyopewa na Baraza sambamba na yeye kubadilika katika kubuni kazi zenye maadili na zisizo dhalilisha watu wa kada mbalimbali.

Maagizo aliyopewa Msanii Nay ni pamoja na kulipa faini (adhabu) ya kiasi cha Shilingi milioni 1, kufanya marekebisho ya mashairi ya wimbo wake wa ‘Pale Kati’, kufuata sheria, kanuni na taratibu za urasmishaji sekta ya sanaa kwa maana ya kusajiliwa na BASATA na kuhakikisha wimbo wake umefuata taratibu zote.

Aidha, msanii Nay ameagizwa kuwaomba radhi watanzania kwa kutoa kazi ya muziki yenye kuvunja maadili na kudhalilisha watu wa kada mbalimbali hususan wanawake.

Taarifa iliyotolea leo na Katibu Mtendaji wa BASATA Godfrey Mngereza imesema kuwa maamuzi haya yamefanyika kwa mujibu wa kifungu cha 4(2) cha sheria nambari 23 ya mwaka 1984, ikisomwa pamoja na kifungu cha 30(1)(2) na waraka wa Wizara ya Habari, Utamaduni na Michezo wa tarehe 16/7/2009 ambayo kwa sasa inafahamika kama Wizara ya Habari, Utamaduni, Sanaa na Michezo.

Mngereza amesema hizo zimetolewa kufuatia BASATA kufanya kikao cha pamoja na Msanii huyu jana siku ya Jumanne tarehe 26/07/2016 kwenye Ukumbi wa Baraza na yeye kukiri makosa na kuahidi kubadilika.

Makosa aliyosomewa na yeye kuyakiri kwa maandishi ni pamoja na;

1. Kujihusisha na shughuli za Sanaa pasipo kusajiliwa na BASATA.

2. Kutoa wimbo wa “Pale Kati” na kuupakia katika mitandao ya kijamii bila kuuleta kufanyiwa uhakiki wa maudhui yake.

3. Maudhui ya wimbo wa ‘Pale Kati’ kwa sehemu kubwa hayafai kwa matumizi ya wazi na ni kinyume cha sheria za nchi na maadili ya mtanzania.

Ikumbukwe kwamba mnamo tarehe 16/07/2016 BASATA lilitoa taarifa kwa umma ya kuufungia wimbo wa Pale Kati kufuatia kubeba maudhui yaliyotajwa kuwa ni yenye uvunjifu mkubwa wa maadili na kupambwa na picha dhalilishi kwa wanawake.

Aidha, tarehe 12/02/2016 BASATA liliufungia wimbo wa Shika Adabu Yako wa Msanii huyuhuyu kwa makosa yanayofanana na haya.

Mngereza amesema kuwa adhabu hii imetolewa ili kumpa muda wa kujifunza, kujitathimi na kujirekebisha kama kweli ana nia ya kuendelea kufanya kazi ya muziki.

eatv.tv

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364