NDANI YA BOKSI: Mchawi wa Bongo Movie ni Bongo Movie…
Kim Kardashian anaweza kuwa na mpango wa kupiga picha za utupu katika jarida maarufu la PlayBoy. Ameshafanya hivyo mara kadhaa.
Na zaidi dunia nzima iliwahi kumuona akifanya ngono na Ray J, kupitia mkanda wa video waliojirekodi pamoja. Lakini haijawahi kumyumbusha akili yake na kushindwa kuendelea na mambo yake na zaidi umaarufu ukaongezeka zaidi. Biashara zake zikaendelea kubamba.
Tanzania na Marekani ni mbingu na ardhi. Hatufanani kwa kila kitu. Kuanzia maadili, uchumi na utamaduni. Katika mpango wake huo wa kupiga picha za utupu meneja wake atamuunga mkono. Atamsisitiza. Atampa mbinu zaidi za namna ya kukamata akili za watu. Na zaidi yeye ndiye aatayesimamia shughuli nzima ya namna na kiasi cha fedha watakacholipwa. Unamfahamu meneja wake?
Ni mama yake mzazi. Marekani akili zao wanazijua wenyewe. Ndiyo utofauti wetu Tanzania na Marekani. Wakati huko mama mtu anamuunga mkono mwanaye kupiga picha za utupu, huku Tanzania mama yake Wema analumbana na waandishi wa udaku. Kwa habari yenye kichwa cha habari kisemacho “Wema, Diamond wana kwichi kwichi kisiri”.
Tuko tofauti sana na Wamarekani. Wazungu wote wako hivyo, naitaja Marekani kwa sababu sisi tunawaiga zaidi wao kuliko Wapoland au Wahispania. Kwa utofauti huo tunawaacha na utamaduni wao sisi tufanye yetu.
Msanii wa Tanzania ni tofauti na wa Marekani. Kiuchumi aina ya maisha yao na kila kitu. Kuna kitu kimoja tu tulichowazidi. Aibu ya utu.
Video ya Ndindindi ya Jide inaweza kutazamwa popote duniani. Lakini Morocco wanaweza kupiga marufuku nchi kwao video ya Rude Boy ya Rihanna. Iko hivyo. Msanii wa Kitanzania inabidi aitazame jamii yake kwanza kabla ya kuingia ‘location’ au studio kufanya yake.
Kuna wendawazimu umewaangia wasanii wetu sijui ni ushamba au kuyojitambua.
Katika ardhi ya Tanzania kutaka kufanya kile anachofanya Kardashian utachekesha watu. Utawakera. Utawapoteza. Na watakutenga.
Leo hii tunawaona wasanii wetu wakipiga picha za utupu mitandaoni. Wakiacha miili yao wazi ili tuone tattoo walizojichora mpaka sehemu nyeti.
Na hawaoni kama ni kosa kubwa kwa siku za usoni. Ila wanachoona wao ni ushamba na ubwege wa kiboya wa sisi tunaoshangaa wanachofanya. Wanawaiga kina Kim Kardashian wakati wako katika ardhi tofauti kwa kila kitu. Kardashian anaangalia jamii yake inataka nini. Ndo maana Jarida la PlayBoy linauzwa ndani ya nchi yake bila vikwazo. Huku PlayBoy zetu zimekuwa Instagram.
Wasanii wa Bongo Movie hivi sasa wana haha. Soko lao limetoweka kama ‘kaseti’ za Marehemu Lufufu. Hawatazamwi tena kwa kazi zao. Wanatazamwa kama midoli ya kwenye maduka ya nguo. Watu watanunuaje filamu zao. Kama vituko vyao watu wanavyoviona kwenye vipindi vya Shilawadu ni filamu tosha? Wasanii wa filamu wametengeneza mazingira mabovu ya soko lao wao wenyewe.
Wamewalazimisha watu wafuatilie maisha yao zaidi badala ya kazi yao. Maisha ya mitandaoni kwa wasanii wetu ni filamu tosha. Wataenda vipi kunua movie ya elfu tano wakati matukio ya kwenye filamu yapo Instagram. Unazama mitandaoni unakutana na video ya Jack Wolper akiigiza kulia chozi linamtoka anajirekodi anapost Instagram kisha anawaomba watu wampe pole kafiwa sijui na shost yake huku mtaani anakojua yeye.
Kila siku unasikia fulani ana kwichi kwichi na fulani. Habari zao zinaanzia mitandaoni redioni mpaka magazetini. Na kibaya zaidi habari zao zina mvuto kwa watu kuliko filamu zao. Habari zao za mapenzi zinasambaa kuliko filamu zao. Na stori zao ni za ukweli na zinavutia kusoma na kusikiliza kuliko stori zao za kwenye filamu ambazo ni za uongo halafu mbaya.
Watu hawawezi kununua stori za uongo ambazo hazina mvuto kwenye filamu, wakati wakitega sikio kwenye Shilawadu na kuperuzi mitandaoni wanakutana na stori zao za ukweli halafu zinavutia kwa kuzisikiliza na kutazama. Maisha yao wameyageuza kama filamu halafu filamu wamegeuza kama mikanda ya Kipaimara. Komonio. Harusi au Birthday.
Lazima soko liyumbe. Na mwenye akili ni ngumu kushangaa Monalisa na Rose Ndauka kuwa watangazaji maarufu badala ya waigizaji maarufu. Kwa sababu soko la filamu limepauka kama ukuta wa uwanja wa Kaunda pale Jangwani.
Bongo Movie punguzeni ‘vicheche’ kwenye tasnia yenu. Ondoeni wauza sura wanaotaka kulelewa kwa umaarufu. Ingizeni wasanii bora na siyo bora wasanii kwenye tasnia ya filamu.
Namna ya kupunguza siyo kuwatimua waliopo bali jiwekeeni miiko maadili taratibu na kanuni zitakazowabana wasanii ambao hawana lengo zuri na tasnia yenu.
Hakuna sababu ya kulalamikia filamu za kutoka nje ya nchi kwamba zinaharibu soko lenu. Huo utakuwa uvivu wa kufikiri na kutenda. Ukweli ni kwamba mazingira haya ya ubovu wa soko mmeyatengeneza na kuyatukuza wenyewe. Na bado mnayalea kwa kuyapalilia na kuyamwagilia kama mazao mashambani.
Kanumba waliingia kwenye game filamu za Kinaijeria zikiwa juu nchini. Ilikuwa ngumu sana watu kuwahamisha kwenye filamu za Kinijeria. Kwa sababu hizo ndizo zilizoua hata soko ka tamthiliya zetu.
Taratibu kwa ubora wa kazi za hapa nyumbani Wanigeria wakaondolewa kwenye soko. Wakabaki kina Kanumba. Wakasomba watu. Wakawateka ‘Wadosi’ kisha wakapiga fedha nyingi sana.
Kwa nini ishindikane leo? Ondoeni magugu maji. Achaneni na maisha ya siasa. Kulalamikia filamu za nje ni maneno ya kisiasa.
Unataka kuondoka kitu bora kinachopendwa na watu ili kuwalazimisha waangalie mikanda ya Vipaimara na Komonio mnazoita movie? Kinachowaponza Bongo Movie ni maisha ya kwenye filamu kuyaleta mtaani.
Kila kitu wanaigiza. Wanaigiza kuvaa nguo. Wanaigiza kulia hata kwenye misiba inayowahusu kwa damu kabisa. Wanaigiza kuishi kana kwamba wana kipato kikubwa sana. Na wanaigiza mpaka kwenye mapenzi. Bongo Movie vigumu sana kumuamini kwenye uhusiano wa mapenzi kwa sababu wanaigiza sana. Naamini huigiza hata kuoga na kwenda msalani.
Maisha yao ya filamu wameyaweka mitandaoni. Msanii wa Bongo Movie siyo bidhaa adimu tena. Wanapatikana sana kama mabasi ya mwendokasi. Kila dakika utamsikia redioni. Utamuona mitandaoni. Gazetini au runingani akihojiwa siyo kwa kazi yake mpya au iliyopo. Bali kwa kituko alichofanya. Mahojiano ya mastaa wetu hivi sasa ni ya nani anatoka na nani. Nani kamtema nani. Nani kaingilia penzi la nani.
Iko hivyo lakini suala la kazi yao huwezi kulisikia. Na mashabiki nao wanaenda vile unavyotaka wewe nao wanafuatilia zaidi vituko vyao kuliko kazi zao. Akiandikwa gazetini anaenda kujibu mitandaoni. Hivi hamjiulizi kwamba watu bado wanawapenda ndiyo maana wanafuatilia kila kitu mnachopost mitandaoni na kuandikwa magazetini?
Sasa kwa nini hawafuatilii wala kununua kazi zenu? Manaake ni kwamba matukio yenu ya kila siku ni rafiki kwa macho na masikio ya mashabiki wenu kuliko uongo wenu wa kwenye filamu. Shitukeni.
Ni vigumu watu kuwa na hamu na wewe au kazi yako. Wanajisifia kuwa magazeti ya udaku siku hizi hayana soko kwa sababu kila kitu kipo Instagram. Sawa ni kweli ila Instagram inakusaidia nini? Kama una wafuasi milioni mbili halafu kazi yako ya filamu huwezi kuuza hata kopi mia tano mtaani? Si kichaa hicho? Unafurahia likes na comments tu. Una wafuasi mamilioni mitandaoni ukurasa wako hauna tangazo hata moja la biashara ambalo linakuingizia pesa.
Watu wenye akili zetu tulishituka mapema sana baada ya kuona Steve Nyerere anapewa madaraka ya kumuongoza JB na Ray kwenye kikundi cha Bongo Movie. Siasa ikateka akili zao wakawaza posho za kampeni kuliko kile kilichowapa heshima na pesa kwa miaka mingi.
Kichaa kinatofautiana ila hiki nacho ni kichaa mtambuka.
Makala By Dk Levy.
Mwananchi