Ningekuwa Kibaka au Sheikh-Dogo Janja
Rapa Dogo Janja mwenye hit ya Ngarenaro amefunguka kama asingekuwa mwanamuziki na kupata mafanikio basi angekuwa mwizi au sheikh kutokana na maisha aliyoishi huko awali.
Akizungumza kwenye Top 20 ya East Africa Radio, ndani ya Back stage, Dogo Janja amesema kuwa kama asingefanikiwa kwenye muziki basi kwenye maisha yake angeendelea na kuiba au angebadilika na kuwa Sheikh kwa sababu baba yake alikuwa akijitahidi kumbana sana ili aweze kusoma chuo (Madrasa)
“Nilikua kibaka kweli, Mjanja mjanja sana, lakini Mzee naye alikuwa akinikamata ananibana sana niende madrasa. Msikiti wa Ngarenaro nilikuwa napiga adhana , hicho ni kitu ambacho kilikuwa kinanipelekea hata nisiache kwenda Madrasa a nilikuwa vizuri kwenye dini sema utundu na maisha ndivyo vilivyonifanya niingie kwenye muziki” amesema.
Katika hatua nyingine Janjaro amesema kwamba anamshukuru Mungu kwa hatua aliyofikia kwani amebadilika na sasa amekuwa kijana anayeishi kwa kufuata misingi ya nchi na dini bado hajaiacha.
Aidha Dogo Janja amesema kwamba kuhusu albamu watu wakae tayari kwani hivi karibuni yeye na msanii Madee wataachia albamu waliofanya pamoja.
“Mimi ndiyo Dogo wa kwanza kupeleka albam kwa Mamu. Nina albamu moja inaitwa mtoto wa uswazi na ya pili tumeshafanya na Madee ipo tayari siku siyo nyingi tunaachia mzigo” – Dogo Janja.