Nisha: Mastaa Wasahau Penzi Langu
SALMA Jabu maarufu kwa jina la ‘Nisha’, siyo geni masikioni mwa wapenzi wa filamu za Kitanzania ambapo watu wengi walianza kumfahamu kupitia kipaji chake cha uchekeshaji.
Nisha amewahi kufanya vizuri kwenye baadhi ya filamu kama Simu Sikioni, Because of Facebook, Chumba cha Siri, Mchana wa Kiza, Bado Niko Hai, Pusi na Paku na nyingine nyingi.
Swaggaz imepata nafasi ya kupiga naye stori ambapo amezungumza mengi yanayohusu maisha yake ndani na nje ya sanaa.
Anasema akiwa mdogo hakuwahi kutamani kuigiza lakini alipokuwa anasoma sekondari aliangalia filamu waliyocheza Johari (Blandina Chagula) na Uwonya (Irene) iitwayo Peace of Mind, ikamvutia kuanza kuigiza.
“Filamu hiyo ilinishawishi kuanza kuwatafuta ili wanisaidie na mwaka 2012 nikaanza rasmi, licha ya kupitia mabonde mengi niliweza kufanya kazi na RJ Company ambapo nilipewa sehemu moja katika filamu ya My Dream.
“Mpaka nakuja kuwa Nisha anayefahamika na watu wengi nchini nimepitia changamoto nyingi sana lakini naweza kusema kwamba nimezikabili na sasa ni Mkurugenzi wa Nisha Entertainment Company,” anasema Nisha.
Wiki kadhaa zilizopita kwenye mitandao ya kijamii, kulifukuta bifu kali dhidi ya Nisha na msanii mwenzake Jacquline Wolper.
Akizungumzia hilo, Nisha anasema: “Hakuna bifu lolote linaloendelea labda mashabiki zangu walichukulia tofauti baada ya mimi kuweka picha ya Nuh Mziwanda akiwa na Raymond, Rich Mavoko na mwingine nimemsahau na kuandika mmoja wao ‘He is my Babee’ alichocomment Wolper ndicho walichochukulia tofauti mashabiki,” anasema.
Katika maoni yake, Wolper aliandika: “Hebu wataje walionyakuliwa tuwajue @nishabebeee yani ulikuwa umewamiliki na wakanyakuliwa, maana kunyakuliwa mtu awe official siyo mpita njia halafu ulalamike umenyakuliwa nikimanisha wewe na yeye mlishawahi kutangazana wa karibu wataje tuwakanye.”
Hata hivyo, Nisha anasisitiza: “Sina bifu kabisa na Wolper. Ni amani tu.”
Mbali na sanaa, Nisha amekuwa akifanya harakati za kujitoa kuwa sauti ya watoto wanaoishi kwenye mazingira magumu, yatima na walemavu ambapo ni Balozi wa Kikundi cha New Hope Family cha Kigamboni jijini Dar es Salaam.
“Kuwasaidia watoto ni moja ya maisha yangu na siyo kwamba nawasimamia New Hope Family pekee, nasaidia watoto wote nchini, sibagui. Nawatengenezea watoto mazingira mazuri ya kuishi. Nashukuru naendelea vizuri,” anasema.
Iliwahi kuvuma kuwa anatoka kimapenzi na msanii Baraka Da Prince, lakini Nisha anasema hizo ni fununu tu, ambazo hazina ukweli wowote ndani yake.
“Sijawahi kutoka na huyo mtu na haitakuja kutokea, tena siyo yeye tu bali sina mpango wa kutoka na msanii yeyote hapa Bongo. Nafanya hivi kwa sababu sitaki kuchanganya mapenzi na kazi na sitaki kufanya utani na mipango yangu,” anasema kwa kujiamini.
Akizungumzia kuhusu kuwasaidia wasanii chipukizi, Nisha anasema ni kati ya programu zake, maana hata yeye alikuwa chipukizi na alipata watu wa kumsaidia ndiyo maana akafanikiwa kutoka.
“Nisha ni mama wa wasanii wote chipukizi Tanzania hivyo kila mmoja yupo chini yangu na wengi wamekuwa wakinipigia simu, nawasaidia ndiyo maana niliamua kuweka namba yangu maalumu ya kuchati nao kwa WhatsApp ili kujadiliana nao namna ya kuwasaidia.
“Lakini pia kampuni yangu tukiwa na filamu, washiriki asilimia 80 huwa ni chipukizi, mastaa huwa hiyo asimilia 20 iliyobaki,” anasema Nisha.
Aidha anasema katika upande wa wasanii wa muziki yeye kwa kushirikiana na HK wanamsimamia msanii mmoja wa muziki wa Singeli aitwaye S Kide na tayari ameshatoa wimbo mmoja ‘Ushemeji Upo’ akionekana kumjibu Man Fongo aliyetoa ‘Hainaga Ushemeji’.
Mtanzania