Nyimbo nyingine zaidi kufungiwa
Siku tano baada ya Mamlaka ya Mawasiliano Tanzania (TCRA) kusitisha kuchezwa kwa nyimbo 15 zisizokuwa na maadili, zikiwemo mbili za msanii Nassib Abdul maarufu Diamond, Baraza la Sanaa la Taifa (Basata) limesema hivi karibuni litatoa orodha ya nyimbo nyingine zitakazofungiwa.
Akizungumza na MCL Digital leo Machi 5, 2018 katibu mtendaji wa Basata, Godfrey Mngereza, amesema orodha hiyo itatolewa kwa kuwa bado kuna nyimbo zinaendelea kuchezwa licha ya kutokuwa na maadili, kwamba Basata imedhamiria kumaliza nyimbo hizo.
“Tumeshawakanya wasanii wetu vya kutosha lakini
wengine wamekuwa wanafanya kusudi. Tunaona njia ni moja tu kuzifungia kabisa na hii ni baada ya kupata ushirikiano wa TCRA. Wenye mpango wa kutengeneza nyimbo zilizo kinyume na maadili watakula hasara, wajitahidi kuzuia hasara,” amesema.
Kuhusu malalamiko ya wasanii kwamba hawakuitwa kuelezwa makosa yaliyopo katika nyimbo zao, amesema kwa sasa wamebadili utaratibu kwa maelezo kuwa walipokuwa wakiwaita wasanii hao kujieleza, walitumia nafasi hiyo kuzinadi nyimbo zao.
“Yaani tumejikuta wakati tukitangaza kuzifungia nyimbo watu ndio huzidi kuzisaka nyimbo hizo. Ili kuepuka hili wasanii wanapaswa kuleta nyimbo zao Basata zihaririwe kabla ya kuzitoa. Wapo wanaofanya dharau na kuzitoa bila kutushirikisha maana wanaona zinachezwa,” amesema.
Nyimbo zilizofungiwa na TCRA ni Hallelujah na Wakawaka (Diamond), Kibamia (Roma Mkatoliki), Pale kati patamu na Maku makuz (Ney wa Mitego), Hainaga ushemeji wa Manifongo, I am Sorry JK (Nikki Mbishi).
Nyingine ni Chura na Nimevurugwa (Snura), Tema mate tumchape(Madee), Uzuri wako (Jux), Nampa papa (Gigy Money) na Nampaga (Barnaba), Mikono juu (Ney wa Mitego) na Bongo bahati mbaya wa Young Dee.
Kuhusu wimbo wa Chura kufungiwa mara ya pili, amesema hiyo imetokana na wanawake wenye maumbo makubwa kulalamika kuwa wanaitwa chura kila wanapokatiza mitaani, jina ambalo limekuwa likitumika kuwadhalilisha wanawake.
Pia, amezungumzia nyimbo za Ney wa Mitego kwamba matendo yanayofanyika katika video zake pamoja na lugha anayotumia si nzuri na inajulikana wazi alilenga kusema nini, jambo ambalo si sahihi.
Mwananchi