-->

Profesa Jay: Diamond, Kiba Wanaua Bongo Fleva

MKONGWE kwenye muziki wa Hip Hop Bongo, Joseph Haule ‘Profesa Jay’ ameibuka na kusema kuwa, wasanii  mahasimu wakubwa, Nasibu Abdul ‘Diamond’ na Ali Kiba ndiyo wanauoa muziki wa Bongo Fleva.

Mbunge wa jimbo la Mikumi na msanii wa Hip hop , Prof Jay

 

Profesa Jay ambaye ni Mbunge wa Mikumi, akiwa ameachia ngoma yake mpya ya Kibabe hivi karibuni  amefanya mahojiano na Polisi wa Swaggaz na kuzungumza mengi kuhusiana  na muziki wa Bongo na sanaa kwa jumla.

Fuatilia sehemu ya mahojiano hayo;

SWAGGAZ: Umeachia ngoma mpya Kibabe, nini kimo ndani ya ngoma hiyo? Kwanini umeiita Kibabe?

PROFESA JAY: Nimeuita Kibabe kwa sababu mimi ni msanii mkongwe na nimefanya mengi kwenye huu muziki… na kama nilivyosema humo ndani (ya wimbo), nimechonga barabara ambayo mafanikio hayo (ya muziki) wasanii wengi sasa hivi wanayapata.

Mimi ni msanii wa muziki wa juu yaani heavy weight Mc, nimeona kuna baadhi ya mapungufu yapo kwenye game yetu, yakiwemo uandishi, kiki ambazo hazina kichwa wala miguu na vitu vingi vilivyofanya sanaa yetu idorore au ipunguze ule uhalisia wake ambao tulikuwa tunautegemea kila siku.

Ndiyo maana nikasema niuite wimbo wa Kibabe, kwa sababu mimi ni msanii mbabe na kama unavyojua hii ni Hip Hop… Hip Hop imejaa majigambo… unajisikia nini moyoni mwako na kupeleka kwa hadhira ambayo ni jamii.

Muziki wa sasa hivi ni tofauti sana na zamani sababu mwanzo platforms zilikuwa chache, radio stations zilikuwa chache lakini pia TV zilikuwa chache, studio zilikuwa chache na hata sapoti haikuwa kama ya sasa, lakini sasa hivi kila mtu anasapoti muziki wetu, kuanzia viongozi mpaka mashabiki wa chini, wote wanajitahidi kuwa wazalendo na kusapoti muziki wetu.

SWAGGAZ: Unaonaje sanaa yetu na hasa muziki ambao wewe ni msanii wake. Vipi, kuna hatua tunapiga kwenye muziki au unaona tupo palepale?

PROFESA JAY: Muziki unakua, lakini wasanii hawapo serious kwenye utendaji wao wa kazi. Unaweza kuona wasanii wakubwa kama Diamond na Kiba ambao wana platform kubwa, lakini hawaongei, mashabiki wao hawasaidiani, hawashirikiani, inachangia sana kuufanya muziki wetu udorore.

Naamini kwa nguvu kubwa waliyonayo Kiba na Diamond, wangekuwa pamoja, mashabiki wao nao wangeungana, kama taifa tungeweza kwenda mbele kwa haraka zaidi.

Wenzetu Nigeria wameshirikiana sana, watu walikuwa walidhani kuna bifu kati ya WizKid na Davido au D Banj na P Square, lakini baadaye unawakuta pamoja wanakunywa kahawa.

Naamini siku moja Diamond na Kiba watamaliza bifu zao na kutengeneza taifa lililo bora na wao kama kioo, kama wasanii ambao tunawaangalia sana, wanaweza kufanya kitu kizuri zaidi. Ushindani ubaki wa kimuziki na siyo wa kishabiki na chuki.

SWAGGAZ: Tangu umekuwa mbunge kuna mchango gani mkubwa ulioleta katika sanaa kwa ujumla?

PROFESA JAY: Nimefanya mambo mengi ya kuwasaidia wasanii lakini zaidi ni kupaza sauti ya wasanii ndani ya Bunge kutetea haki yetu. Changamoto za wasanii sasa zinajulikana na namna gani ya kubana ili jasho lao liwafikie moja kwa moja.

SWAGGAZ: Nje ya bunge, hakuna kitu cha moja kwa moja ulichofanya kwa wasanii?

PROFESA JAY: Kama nilivyosema, kazi kubwa nimeifanya kwa kushirikiana na wenzangu, lakini pia studio yangu ya Mwanalizombe nimeihamishia Mikumi na sasa matengenezo yanaendelea ikiwa kwenye hatua za mwisho kabisa.

Hii studio itawasaidia wasanii wa Mikumi na hasa wa vijijini kurekodi kazi zao katika quality ya juu. Naamini itakuwa msaada mkubwa sana kwa wasanii wa Morogoro kwa ujumla na wasanii wengine walio katika mikoa ya  karibu kama Dodoma na Iringa na kufanya kazi zao katika viwango bora.

SWAGGAZ: Mwelekeo wa muziki wa Tanzania unauonaje kwa sasa hasa katika ushindani wa kimataifa?

PROFESA JAY: Mwelekezo ni mzuri, na naamini Kiswahili kinazidi kupasua anga na sisi tunaeleweka. Unaweza kuona sasa hivi wasanii zaidi ya kumi, nyimbo zao zinapigwa kwenye stations kubwa za kimataifa kama Trace, MTV, Channel O nk.

Hata Blogs za kimataifa zinaripoti habari zetu, naamini tukiwa wengi, tutazidi kuwa na mafanikio makubwa zaidi. Nayaona mafanikio makubwa mbele yetu. Tukiwa wasanii wengi na channels zikafunguka zaidi, naamini tutazidi kufanya vema kwenye tuzo za kimataifa kama nchi nyingine.

Mfano Nigeria unakuta kwenye tuzo nyingi wao wanakuwa 25, Mtanzania mmoja au wawili ndiyo maana wanatushinda, naamini wasanii tukiongezeka tutasaidia zaidi kupasua kimataifa.

SWAGGAZ: Unatengaje muda wa muziki na kuwatumikia wananchi bila kuathiri upande wowote?

PROFESA JAY: Nasema kila siku, mimi ni mtu wa kutumikia Jimbo la Mikumi kwa asilimia zote. Hii talent nipo nayo, na ninayo kila siku. Nalala nayo, naamka nayo, naoga nayo, nakunywa nayo chai, natembea nayo.

Kwahiyo hainizuii hata kidogo kutimiza majukumu yangu jimboni. Muziki ni kipaji, kipo ndani, ninacho siku zote.

SWAGGAZ: Vipi kuhusu ndoa yako, baada ya kumvisha mpenzi wako wa muda mrefu pete ya uchumba?

PROFESA JAY: Ni kweli Desemba 31, mwaka jana nilimvalisha pete mchumba wangu wa muda mrefu, mama Lissa, anaitwa Grace ambaye nimezaa naye mtoto mmoja Lissa mwenye miaka 11 na Mungu akipenda mwezi wa saba mwaka huu, nitafunga naye ndoa. Naombeni sana baraka zenu, naombeni mniombee ili niweze kulikamilisha jambo hili mbele za Mungu.

Mtanzania

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364