Ray Kigosi Afunguka Kutokuwa na Wivu kwa Irene Uwoya na Dogo Janja
Msanii Vicent Kigosi maarufu kama Ray ambaye ndiye aliyemfungulia milango ya kuingia kwenye sanaa muigizaji Irene Uwoya, amesema hawezi kuwa na wivu kwa kuolewa na Dogo Janja.
Akiongea kwenye kipindi cha Planet Bongo ya East Africa Radio, Ray amesema yeye alianza kumuona Irene kabla ya Dogo Janja, lakini hakuvutiwa kumuoa, hivyo hawezi kuwa na hisia za wivu kwa yeye kumuoa muigizaji huyo mwenye mvuto wa kipekee.
“Mimi siwezi kuwa na wivu nilianza kumuona Irene kabla ya Dogo Janja, Dogo Janja ni mdogo wangu na namuheshimu kwa maamuzi ya kumuoa Irene Uwoya, mimi yule ni dada yangu ambaye nimetoka naye mbali kwenye sanaa, na mimi ndiye nilimu-introduce kwenye sanaa na marehemu Kanumba, kama ningekuwa nimemuona ningetamani kuwa naye basi ningekuwa nae lakini niliamua kufanya naye kazi tu, wengine wamemuona wamemchukua, ni jambo zuri hata Mungu anafurahia”, amesema Ray.
Ray ameendelea kusema kwamba yuko tayari kumuita Dogo Janja shemeji kwa sababu ameshamuoa dada yao Irene Uwoya, na kuhusu suala la umri halijalishi sana kwani kikubwa ni upendo.
“Mapenzi ni kipenda roho, na kipenda roho hula nyama mbichi, kama wamependana wenyewe inatosha, niko tayari kumuita shemeji kwa kuwa kashamuoa dada yangu”, amesema Ray.
Hivi karibuni Dogo Janja na Irene Uwoya wamefunga ndoa jambo ambalo limewashtua watu wengi, kwa kuwa kuna tofauti kubwa ya umri kati ya wawili hao.
Eatv.tv