-->

Rose Muhando, Hii Ni Fedheha Kubwa Kwako!

NI jambo lisilohitaji mjadala, kukubaliana kwamba Rose Muhando, ni mmoja wa watu ambao Muziki wa Injili Tanzania, una damu yake, hasa unapozungumzia kile kitendo cha kuutoa ndani ya nyumba za ibada na kuuleta nje, tena kwenye majukwaa.

Rose Muhando

Ndiyo, Gospo ni muziki wa ndani ya nyumba za ibada, ukipigwa na wanakwaya kwa miaka mingi hapa kwetu na ilipolazimika kutoka nje, basi ni kwenye matamasha ya shughuli za kidini na hakukuwahi kuwa na mtu mmoja aliyeweza kusimama peke yake kuimba.
Lakini Rose Muhando ni miongoni mwa waimbaji wa kwaya walioamini wanaweza kufanya vitu viwili kwa wakati mmoja, kuimba kwa kumsifu Mungu, lakini wakati huo huo wakajiingizia kipato.
Alifanya hivyo na akakubalika sana, kwani mashabiki wa nyimbo zake hawakuwa watu wa kanisani tu, hata watu wa imani nyingine walivutiwa na nyimbo zake.

Ndiye aliyekuwa kioo cha waimbaji wengine kujitokeza na kuonyesha uwezo wao, kiasi kwamba wengi wakaanza kumtumia kama chanzo cha mapato, akiitwa huku na kule kutumbuiza katika matamasha na zinduzi mbalimbali za albamu na nyimbo za wanakwaya wenzake.
Ukubwa wa jina na kazi yake ukawavutia hadi watu wa Sony Music ambao waliweza kuingia naye mkataba wa kumsimamia katika shughuli zake za muziki.
Kuwavutia watu kama Sony siyo jambo dogo, maana hawa jamaa wanafanya kazi kimataifa na wako na wasanii wengi dunia nzima. Achana na tuhuma za utumiaji wa madawa ya kulevya, acha ile ya maneno kuwa anazaa nje ya ndoa, maana hivi vitu ni kwa faida yake, afanye, asifanye shauri yake na maisha yake.
Lakini kuna hili jambo ambalo mwanzo lilianza kama tetesi, baadaye ikaja kujulikana kuwa ni kweli. Binafsi nimeshawahi kuzungumza naye juu ya hili jambo, akakataa kabisa, akitoa madai kuwa kuna watu wamejipanga kumchafua na anawajua. Ni hili la utapeli katika shoo zake.
Tuhuma zinasema Rose anachukua hela kwa ajili ya kushiriki matamasha ya nyimbo, lakini hatokei. Nimekutana na watu wengi wanaomlalamikia kuhusu tabia yake hii, ambayo tofauti na yale mawili ya mwanzo, hili ni jinai, linaweza kumfunga jela.

Alianza Alex Msama, aliyewahi kuwa meneja wake, akilalamika kuwa dada huyo siku hizi amekuwa haeleweki, anachukua hela halafu hatokei eneo la tukio, hali imekwenda hivi kwa watu kuongezeka wakimtuhumu kwa suala hilo, lakini amekuwa mbishi kukubali, hadi hivi majuzi polisi mkoani Singida walipothibitisha kumkamata kwa madai hayo.
Kwa mtu wa aina yake, ambaye amepata sifa kubwa kwa nyimbo zake zinazoonyesha utii kwa Mwenyezi Mungu, akiwafundisha watu kuwa na tabia njema, kuepuka zinaa, vishawishi na tamaa ya mali ya dunia, hii ni fedheha kubwa. Ameacha kumtumikia Mungu na sasa ameamua kuwa mfuasi wa shetani maana anajua wazi kuwa anachukua hela za watu lakini hatatokea.
Ni vibaya kumuita tapeli, bali ana jina zuri zaidi analopaswa kuwa nalo zaidi ya hili. Ameshindwa kuridhika kwa alichokipata kwa miaka yote ya utumishi wake na sasa ameamua bila haya, kuwa mtenda dhambi za dhahiri. Dada, ninajua haya ni mapito, hizi ni dalili za kuwepo kwa mapungufu katika mapato yako. Kuna eneo umekosea kwa sababu wewe siyo mtu wa kutapeli laki tisa au milioni.

Na kama mapato yako yamepungua kiasi cha kukulazimu kuwa hivyo, ni wazi kuwa ulisahau kuwekeza, kwa sababu mtu wa kulipwa hadi milioni tatu, nne, tano kwa shoo, kwa muda ambao umefanya Muziki wa Injili, leo hii huwezi kujivunjia heshima kwa kiwango hicho cha hela.
Yawezekana ulikosea, badili tabia. Bado unayo nafasi ya kurekebisha makosa ya kushindwa kuwekeza vizuri fedha nyingi ulizotengeneza kwa muda mrefu na moja ya njia nzuri ya kuweza kufanikiwa, ni kuacha matumizi makubwa yasiyo ya lazima

Chanzo:GPL

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364