Sijapigwa ‘stop’ na Baraka – Naj
Msanii wa bongo fleva na mpenzi wake Baraka the Price, Najdattani amefunguka kwa kukanusha kuwa hajawahi pigwa marufuku na mwenzake wake kuwatumia ‘model’ wa kiume katika video yake mpya ya wimbo wa utanielewa kama watu wengine wanavyodai.
Naj amebainisha hayo kupitia kipindi cha eNewz kutoka EATV baada ya kuwepo minong’ono mingi inayodai kuhusisha wivu wa kimapenzi katika kazi mpaka kupelekea mwanadada huyo kukataa kuwaweka wanaume katika video yake kwa kuwa watamshika shika mwili wake.
“Hanibani kwenye kazi zangu kiukweli na hata hajawahi kuniambia oonh sitaki uweke ma-model sijui nini na nini hata hatujawahi kufikilia mazungumzo hayo lakini nilivyomwambia kuhusiana na ‘idea’ hata mwenyewe pia alichangia kwenye hilo akasema hiyo ni nzuri itakuwa kitu cha utofauti kabisa hatujawahi kuwa na tatizo”, amesema Naj.
Pamoja na hayo, Naj amesema siyo lazima mwanaume aonekane katika video ya wimbo wake japokuwa maudhui ya wimbo hiyo ni mapenzi.
“Ujumbe ukiuangalia vizuri utaona ni mwanamke ambaye anampenda mwanaume fulani hivi lakini yeye hajamkubali kwa kipindi hicho na endapo pale unapoamua ku-move on, yeye ndiyo anaanza kuja yaani mnapishana ‘so’ ndiyo maana siyo lazima hata mtu mwenyewe aonekane”, amesisitiza Naj.
Kwa upande mwingine, Naj amewataka watu na mashabiki zake waziondoe hizo fikra katika vichwa vyao ya kwamba wivu wa mpenzi wake ndiyo umesababisha kutoonekana video model wa kiume katika wimbo wake.