Siwalaumu Wanaopenda Skendo – JB
Msanii wa filamu nchini Jacob Stephen maarufu kama JB amefunguka na kusema kuwa yeye hawalaumu wasanii ambao wamekuwa wakiendesha maisha yao ya sanaa kwa kutafuta ‘kiki’ au kufanya skendo.
Amesema kwa upande wake yeye hawezi kufanya hivyo kwani anaamini kuwa maisha ya skendo huwafanya wasanii waonekane wahuni, washindwe kuaminiwa na kudharauliwa na baadhi ya watu.
JB alisema hayo kupitia kipindi cha eNewz ya East Africa TV na kudai kuwa yeye amekuwa akiaminiwa sana kwenye kazi yake hiyo ya sanaa kutokana na kuwa na nidhamu na kuziepuka skendo siziso na msingi.
“Siwalaumu wanaopenda skendo sababu ni maisha yao wao ila kwangu mimi najisikia vibaya nikiambiwa nimefanya hiki hiki na hiki sijisikii vizuri kutokana na jinsi ambavyo nimelelewa na Mungu jinsi alivyoniumba. Sasa jeshini ni uvumilivu na kujitambua ndiyo tulivyofundishwa na hii imenisaidia kujenga ‘image’ nzuri mbele za watu, mbele ya jamii hata kwenye location”.
Ameendelea kusema “… kwa mfano mimi nikienda kuomba location sehemu yoyote baba mwenye mke wake, mke wake mpaka watoto wote, mabinti wanajua wapo salama sababu JB nimezaliwa upya wanajua siwezi kuongea ujinga, au hakuna kitu kibaya ambacho kinaweza kutokea kwa hiyo ukiniangalia mimi tu hapa unaona kristo ndani yangu hauoni uhuni” alisema Jb
Mbali na hilo JB amedai tabia yake hiyo imemfanya kuaminiwa hata na makampuni makubwa kwani wanaona kuwa huyu mtu ni mtu sahihi si mtu ambaye wanaweza kusikia amefumaniwa na kutimuliwa na mapanga huko bali wanakuwa na imani kuwa atafanya vyema katika jukumu atakalopewa.
eatv.tv