Video ya Kala Jeremiah Yamkutanisha Mama na Mtoto
Video ya msanii Kala Jeremiah ‘Wanandoto’ imeweza kumkutanisha mtoto na mama yake mzazi baada ya mtoto huyo kupotea nyumbani kwao tangu mwaka jana mwenzi wa tisa.
Mama mzazi wa mtoto huyo amessimulia alivyoteseka kumtafuta mtoto huyo ambapo anasema alikwenda wa waganga, amehangaika kwenye maombi, na njia nyingine za kumpata mtoto wake huyo lakini haikuwezekana mpaka alipokuja kumuona kwenye video ya Kala Jeremiah.
Kala Jeremiah anasema siku mbili zilizopita alipigiwa simu na moja ya mtangazaji wa kipindi cha Radio na kumueleza kuwa kuna mzazi amemuona mtoto wake kwenye video yake ya ‘Wanandoto’ na mtoto huyo alikuwa amepotea toka mwaka jana.
“Kama siku tatu zilizopita nilipokea simu kutoka kwa mtangazaji wa Radio flani akanieleza kuwa kuna mama alimpigia simu akamwambia kuwa amemuona mtoto wake aliyepotea tokea mwaka jana mwezi wa 9 na kamuona kwenye video yangu ya #wanandoto kiukweli nilishtuka nikaomba mtangazaji yule aniunganishe na mama huyo. Nikafanikiwa kuongea na mama huyo na kweli akaniambia alipotelewa na mtoto wake aitwaye Adam na kwamba kamuona mwanaye kwenye video yangu. Yule mama akasema amehangaika sana kumtafuta mwanaye kwa utaratibu wa kawaida hadi kwa waganga mbalimbali wa kienyeji bila mafanikio akasema pia ameenda kwenye maombi mbalimbali lakini hakuweza kumpata mtoto wake na akakata tamaa kabisa”. Alisema Kala Jeremiah
Mbali na hilo Kala Jeremiah anasema mama huyo kutokana na kukata tamaa ya kumpata mtoto wake jambo hilo limempelekea kupata athari hivyo amekuwa akizimia zimia mara kwa mara, Kala Jeremiah aliweza kumuunganisha mama huyo na walezi wa kituo cha watoto na kufanikiwa kuonana na mtoto wake huyo.
eatv.tv