Wakonta: Naomba Mnisaidie Kwa Hali na Mali
MWANDISHI wa muswada (script), Wakonta Kapunda, jana alijitokeza kwa waandishi wa habari akiomba msaada wa hali na mali ili aweze kupatiwa msaada wa vipimo mbalimbali kikiwemo kipimo cha MRI
.
Pia Wakonta ameomba msaada wa makazi kwa Jiji la Dar es Salaam ili iwe rahisi kwake kupata matibabu ya afya yake na kutimiza ndoto zake katika uandishi wa script anaofanya kwa kutumia ulimi.
Wakonta aliyekuwa Zanzibar katika tamasha la Ziff kwa ajili ya masomo ya script, alisema matibabu yanayomkabili yana gharama kubwa na familia yake haina uwezo wa kuhimili gharama hizo.
“Juzi tulikwenda Hospitali ya Muhimbili nilitakiwa niingie kwenye mashine ya MRI lakini sikuweza kwa kuwa sikuwa na fedha zilizohitajika ambazo ni zaidi ya Sh 600,000,” alisema Wakonta.
Anaongeza kwamba kwa sasa bado anaendelea kukabiliwa na changamoto ya usafiri, nyumba ya kuishi na familia yake wakati akiwa katika matibabu pamoja na uandishi wake.
“Nahitaji mtaji wa hali na mali ili niweze kufikia malengo niliyoyakusudia ikiwa ni pamoja na kuanzisha taasisi itakayosaidia watu wenye hali kama yangu kwa kushirikiana na kampuni na taasisi nyingine zitakazoguswa na jambo hili tukishirikiana itawezekana,” alisema Wakonta.
Katika hatua nyingine baba wa Wakonta, Bazilio Kapunda, alisema familia yao inasikitishwa na aliyemsababishia ulemavu huo kutokutoa hata pole kwa familia hiyo wala kutaka kujua kinachoendelea kwa Wakonta.
Mtanzania
MAWASILIANO YAKE
Kutoka kwenye Instagram akaunti yake; wanko (@wakonta_kapunda)