Young Dee Akiri kutumia Unga, Aomba Radhi
Rapper Young Dee hatimaye amethibitisha tetesi za miaka mingi kuhusu utumiaji wa madawa ya kulevya na kukiri kuwa ametumia kwa kipindi cha mwaka mmoja na nusu.
“Sina mtu ambaye ninaweza kumlaumu, lakini mazingira ambayo nimepitia ndio ambayo yamefanya hivyo, kuna wakati ambao nimeishi sana na watu mtaani, kwa hiyo kidogo kidogo ikanifanya niweze kushawishika na kuingia. Kwahiyo napenda kuwashauri vijana wenzangu kuwaangaliwa sana watu ambao wanatembea nao, ukitembea na wezi wawili, na wewe utakuwa mwizi watatu, kwahiyo mimi tayari nimeshajitenga na watu ambao wanaweza kunishawishi na kurudi kule,” alisema Young Dee.
Kwa muda mrefu rapper huyo alikuwa akikanusha tetesi hizo.
Amesema amepewa ushauri nasaha na wataalam na kwamba ameachana na matumizi hayo. Pia rapper huyo amerejea rasmi kwenye uongozi wake wa zamani, Millian Dollar Boyz, MDB alioachana nao mwaka jana.
Kwa upande wa meneja wake, Max amesema Young Dee alipelekwa rehab kuangalia namna ya kumsaidia.
“Afya ya Young Dee ipo salama, tulienda kuwaona madaktari, tulienda rehab na tulifikiri tutamuacha, lakini tukashauriwa kwamba kwa hali yake, hajafikia mahali ambapo anahitaji kukaa rehab. Lakini aliambiwa kama ameamua kuacha binafsi, bado una nafasi ya kuweza kurejea vizuri katika afya yako, na kikubwa ambacho tumekiona baada ya kuachana na Matumizi ya Madawa ya kulevya anakula sana, yaani anakula sana, lakini tuliambiwa pia hayo ni matokeo ambayo mtayaona,” alisema Max.
Pia Max alizungumzia sababu ya kuamua kumsamehe Young Dee na kusahau yote yaliyotokea.
“Matatizo ambayo yamempata Young Dee ni matatizo ambayo tulikuwa tukiyaongelea toka zamani sana, kwamba jaribu kujiepusha kuwa katika vitendo ambavyo vinaweza kukuangusha kwenye tasnia. Lakini katika maisha ya ustaa wa muziki au filamu, kuna vishawishi, magenge ambavyo mara nyingi vinapotosha wasanii wetu na kuweza kuwaweka katika position ambayo huwa wanajuta au kupotea kabisa kwenye tasnia. Tuliona umuhimu wa sisi kuridhia maombi ya Young Dee ya kuomba msamaha, na kwa kweli ametumia nguvu kubwa sana kututafuta sisi, kwa sababu sisi tulivyomalizana naye tulisema basi bhana, sisi tumeshindwa endelea na mambo yako. Lakini amefanya juhudi binafsi kuweza kuamua kwamba nakwenda nyumbani, nakwenda kuomba msamaha, narejea nyumbani nimeamua kuachana na ujinga natamani kuwa mahali ambapo ni salama. Kwa hiyo alipokuja kuomba radhi, na mimi nilisema hata kwenye interview ya Clouds kipindi kile, kwamba atakapoamua kuomba radhi, mimi siwezi kukunja moyo wangu, mimi ni binadamu na mimi na matatizo yangu, kwa hiyo mimi sina sababu yoyote ya kumng’ania mtu kutokumsamehe au kutokuridhia yale ambayo yalikuwa tofauti,” alisema Max.
Aliongeza, “Kwa hiyo tuliona kwa pamoja kama team, hebu tumsaidie na kwa kweli kabisa hebu niseme ukweli, sijawahi kumuona Young Dee huyu tangu nilipofahamiana naye mwanzoni, kipindi ambacho anatoka kwa Lamar, miaka 8 iliyopita. Huyu ni Young Dee tofauti kabisa na yule mnaemjua, na niwahakikishie kitu kimoja sio tu nidhamu, kwa sababu kitu kikubwa ambacho kilikuwa kinamwangusha Young Dee ni nidhamu.”
“Young Dee sasa hivi anamheshimu hata dada anayemfanyia usafi katika chumba chake, sasa hivi tupo naye kwa muda wa mwezi mmoja, hana access na pombe, hana access na sigara, bangi wala madawa, na tulisema kama ni upepo, utaisha kwenye wiki moja, kwa sababu upepo unavuma na ukishavuma unapita, lakini tumeona kwamba kuna jitihada ndani yake, na mimi nitajaribu kumkumbusha kila siku kaza hivyo hivyo ili uweze kuprove kwamba umebadilika.”
Bongo5