-->

Adui wa Wema Sepetu ni Yeye Mwenyewe

WEMA Sepetu na mama yake wameamua kuhama CCM na kuhamia Chama cha Demokrasia na Maendeleo (CHADEMA). Hii ni haki yao ya kikatiba. Ila ajabu katika uhamaji huu ni kauli na matamshi yao.

Mama yake Wema pamoja na mambo mengine ameonekana kuumizwa na kitendo cha mwanaye kukamatwa na kuwekwa  rumande kwa tuhuma za kutumia mihadarati.

Katika maneno yake machache kabla hajahama chama alisema anasikitishwa na kitendo kilichotokea ila anasikitishwa zaidi na viongozi wa Serikali na chama walivyoshindwa kutoa ushirikianao katika sakata hilo la mwanaye.

Mama na mwanaye Wema Sepetu wanashindwa kuelewa shina la tatizo na wao kukimbilia kutokwa na povu bila sababu zozote za kimantiki. Makonda na serikali yake hawakumkamta Wema kwa sababu ni Wema.

Pamoja na watu wengine, Makonda alimtaka kwenda polisi  kutokana na kumuhusisha na tuhuma za  mihadarati. Hapa ndipo mama Wema, Wema na shoga zake wanapotakiwa kupaangalia kwa makini.

Kwanini mrembo kama yeye tena kutoka katika familia yenye heshima anahusishwa katika jambo la kijinga kama hili? Mama, marafiki wa Wema na wote wanaomuonea huruma, wangepaswa kukaa chini kutafakari huku wakijiuliza, kitu gani kinamfanya Wema awe mmoja wa watu wanaoshukiwa kujihusisha na upuuzi huu na siyo kutokwa povu dhidi ya Makonda na CCM yake.

Naamini, kwa kila chama makini chenye kujali watu na kupenda ustawi wa Taifa, kitapingana na aina yoyote ya ujinga ikiwemo uuzaji, utumiaji na usambazaji wa dawa za kulevya.

Alichotakiwa kufanya Wema, mama yake na rafiki zake zao, siyo kuwaza na kuamua kihasira ila walipaswa kutuliza vichwa chini na kutumia busara katika maamuzi yao kama ilivyotokea kwa T.I.D.

Sio kwamba walichofanya siyo busara, lakini majanga aliyokutana nayo Wema, wasingeyaweka kama sababu ya uamuzi wao huo.

T.I.D kama ilivyo Wema alikumbwa na msukosuko wa namna hiyo. Ila yeye badala ya kumchukia Makonda na Kamanda Sirro, yeye kawaona ni watu wenye nia njema ya kukomboa jiji na Taifa kwa ujumla dhidi ya aina yoyote ya ujinga unaotaka kuwafanya vijana wawe mazezeta na wenye ndoto za alinacha.

Martin Kadinda amesema tatizo la Wema linaanzia katika marafiki zake. Hapa ndipo mama Wema angetakiwa kutumia busara kuangalia ni namna gani anaweza kumsaidia mwanaye na siyo kutoa maamuzi ambayo akikaa peke yake anaweza kujishangaa.

Wema mwenyewe inabidi ajitafakari. Akae kwenye kioo ajiangalie namna alivyo na aangalie ni wapi anaelekea. Kila siku kutokea kwenye vyombo vya habari kwa habari zenye ukakasi haipendezi.

Ni kweli yeye ni maarufu, ila umaarufu unaojengwa kwa sifa za ovyo; ni nani atauthamini na kuupa thamani? Ni wajinga pekee.

Ajitafakari na agundue kuwa vituko vyake vinamtia madoa yeye na familia yake huku wengine kwao ikiwa biashara nzuri. Ajitafakari, angepaswa kuwapenda na kuwakumbatia wale watu wanaoonekana kumkanya badala ya kuwakumbatia watu wanaomsifia kwa lolote alifanyalo hata kama ni la ujinga na lisilo na mwisho mwema kwake.

Adui namba moja wa Wema ni yeye mwenyewe.

Na RAMADHANI MASENGA, MTANZANIA

Comments

comments


Unataka kutangaza nasi? Tumia namba ya simu hapo chini.

Please contact us: email : info@bongomovies.com or Mobile: +255 756 348 364