Alikiba Sina Tatizo na Dully Sykes
Mkali wa wimbo Aje Alikiba baada ya kuondoka na tuzo tatu za EATV, amefunguka na kuzungumzia mahusiano yake na msanii mkongwe wa muziki na producer, Dully Sykes.
Hatua hiyo imekuja kutokana na kuenea kwa taarifa za muda mrefu katika mitandao ya kijamii kwamba wawili hao hawaelewani.
Katika usiku wa tuzo za EATV, Dully ndiye aliyemtangaza mshindi wa video bora ya mwaka Alikiba kupitia video yake ya wimbo ‘Aje’ kabla ya kukabidhiwa tuzo na Katibu Mkuu wa Baraza la Sanaa Taifa (BASATA) Godfrey Mngereza.
Akiongea muda mfupi baada ya kuchukua tuzo hiyo akiwa pamoja na Dully Sykes, Alikiba alizishukuru tuzo hizo kwa kumkutanishwa na Dully Sykes huku akidai yeye anamchukulia kama baba katika muziki.
“Mwenyezi Mungu leo ametukutanisha, huyu mimi ndiye aliyenianzisha, huyu ndiye aliyenifanya niamini mimi najua kuimba, nilichokuwa nikiimba brother Dully Sykes muda mwingine nilikuwa namtoa mpaka machozi,” Ali alikiambia kipindi cha Enewz cha EATV akiwa mbele ya Dully Sykes. “Nisipotokea siku mbili hata siku moja kwao lazima ataniulizia Ali yupo wapi. Sina simu sina nini, Dully Sykes alikuwa ananipenda sana sijajua sasa hivi lakini mimi kwangu Dully ni brother wangu na ninaweza nikamuita baba yangu wa kimuziki wa bongofleva. Mimi sina mengi ya kusema ila nataka ajue kwama mimi nampenda siku zote na nitampenda mpaka nakufa,”
Naye Dully Sykes baada ya kusikia kauli hiyo ya Alikiba na yeye alisema hana tatizo na muimbaji huyo wa Aje na kusema anampenda pia.
Bongo5