Aunt Ezekiel Ahaha Kuzima Skendo Mbele ya Mwanaye
UKIGUSA ‘Top 5’ ya wasanii wakike wanaofanya vyema kwenye tasnia ya filamu nchini, jina la Aunt Ezekiel ni lazima liwemo ndani yake. Hii imekuja baada ya kuweza kuhimili mabadiliko makubwa yaliyotokea na kuwapoteza wasanii wengi wenye haiba kama yake.
Tulianza kumfahamu pale alipolitwaa taji la urembo jijini Mwanza na kufanikiwa kuliwakilisha Jiji hilo kwenye mashindano ya Miss Tanzania mwaka 2006. Fursa hiyo ilimpa tiketi ya moja kwa moja kuingia kwenye tasnia ya filamu.
Miss Bongo, ni filamu yake ya kwanza iliyodhihirisha ubora alionao pale anapokuwa mbela ya kamera. Chini ya mwongozaji Willium Mtitu anayemiliki kampuni ya 5 Effect tulianza kumuona Aunt Ezekeil akikua kisanaa.
APATA MASHAVU KIBAO
Baada ya kufanya kile kilichowashtua wengi kwenye filamu ya Miss Bongo, Aunt Ezekiel akaanza kupata dili za kushiriki kwenye filamu nyingine nyingi zilizoandaliwa na waongozaji wakubwa Tanzania.
Miongoni mwa filamu hizo ni Yellow Banana, Eyes On Me, Jungu la Urithi, Shoga Yangu, Siri Sirini, Signature, Nampenda Mke Wangu, Young Billionaire, Danger Zone na Mrembo Kikojozi iliyozidi kumpandisha chati.
SKENDO ZAMPA CHATI
Zaidi ya filamu 40 alizocheza mpaka sasa zimetosha kumpa umaarufu. Ustaa huo ulimfanya aanze kuhusishwa na skendo za hapa na pale ambazo zilifanya jina lake lisikauke kwenye midomo ya wapenda burudani.
Licha ya mazuri mengi aliyowahi kuyafanya lakini pale alipoteleza kama binadamu na kujikuta akiwa kwenye dimbwi la skendo, habari zilikuwa kubwa zaidi na hakika ustaa wake uliongezeka kufuatia kuzungumzwa sana.
Skendo kama kutoka na mume wa mtu, kuolewa na kuachika, kuishi kinyumba na mfanyabiashara maarufu ni matukio yaliyompandisha chati kipindi hicho ustaa wake umeshika hatumu.
HOFU YA SKENDO KUMFIKIA MWANAYE
Aunt Ezekiel amekuwa mtu mzima sasa. Ni mama wa mtoto mmoja anayeitwa Cookie aliyezaa na dansa wa Diamond Platnumz, Mose Iyobo, hivyo mambo aliyokuwa anayafanya kipindi cha nyuma ni lazima ayaache ili mwanaye aweze kujifunza mema kutoka kwa mama.
“Kwa wakati ule nilikuwa sijui madhara yake ila kwa sasa naona katika mambo ambayo yatanifedhehesha basi ni skendo nilizonazo, mwanangu Cookie akizisikia au kuziona hii inaniumiza sana kichwa,
“Sitahitaji mwanangu ayapitie maisha niliyopitia mimi, sikujua kama ningeweza kujulikana kwa kufanya kazi zangu pekee, nahisi akijua mabaya yangu nitakosa pa kuficha sura ,” anasema Aunt.
ADHAMIRIA KUFUTA MAKOSA
Aidha alifafanua kuwa hivi sasa ameamua kubadili mfumo wa maisha yake ili afute yale yote mabaya aliyowahi kuyafanya na ikitokea mwanaye Cookie akisikia skendo zake asiweze kuamini.
NENO KWA CHIPUKIZI WAPENDA KIKI
Staa huyo amewataka wasanii wachanga kulinda heshima zao kwa kupata sifa kutokana na kufanya kazi na siyo kutokana matendo machafu kwani baadaye matendo hayo yatakuja kuwasuta na kuwasumbua kwenye maisha.
“Sasa hivi nimeamini na nitawafunza wasichana wengine wafahamu kuwa mbali na maisha ya usichana wanatakiwa wafikirie maisha yanayokuja na madhara yake, wakifanya hivyo watakuwa vioo vya kutazamwa na jamii,” alisema Aunt.
SKENDO ZAYUMBISHA SOKO
Kumekuwa na hali ya sintofahamu kwenye tasnia ya filamu, wadau wanalalamika kuyumba kwa soko la filamu nchini, hali hiyo Aunt Ezekiel anasema matendo machafu ya wasanii yamechangia kwa namna moja ama nyingine kporonmoka kwa soko.
“Kipindi hiki filamu zimepoteza mvuto na watu wamekuwa wakizungumza mengi ila ninachoona mimi ni matendo yetu machafu yanachangia, mbona wasanii kama kina King Majuto bado wanafanya vizuri? Skendo zinayumbisha soko la filamu na siyo kitu kingine,” anasema.
Mtanzania