Aunty Fifii Amkumbuka Kanumba, Akiwachana Wenzake
IJUMAA iliyopita ilitimia miaka mitano kamili tangu Steven Kanumba alipofariki dunia ghafla na kuleta majonzi nchini nzima, lakini huwezi kuamini ni wasanii wachache wa tasnia hiyo waliweza kufanya kumbukumbu yake.
Jambo hilo limemkera mno mwingizaji mkongwe aliye pia mtunzi na mtayarishaji, Tumaini Bigilimana ‘Aunty Fifi’ ambaye aliongoza ibada ya kumbukumbu ya kifo cha Kanumba sambamba na mama wa marehemu na wanafamilia wachache.
Fifii alisema inasikitisha kwa namna waigizaji na wasanii wengine walivyoshindwa kuitikia wito wa kushiriki kumbukumbu ya kifo cha Kanumba, msanii aliyejitolea kwa hali na mali kuitangaza tasnia hiyo na nchi kwa ujumla kimataifa.
Alisema wasanii wamepoteza upendo baina yao na wamekuwa wepesi kuhubiri upendo lakini utekelezaji wake ni mdogo.
“Wasanii tumepoteza upendo hatupendani, hatma ya filamu Tanzania naiona na kukumbuka maneno ya Kanumba, alisema hata nikifa hakuna wa kuziba pengo, sasa watu wamebaki wakisema Kanumba kaondoka na tasnia,” alisema Aunt Fifi.
Mama Kanumba aliwashukuru wote waliofika makaburini kwa ajili ya kufanya ibada ya mwanae sambamba na kushiriki kuzuru kwa pamoja makaburi ya wasanii wengine waliotangulia mbele ya haki kama Rachel Haule na Adam Kuambiana ambao kama marehemu Kanumba pia walizikwa katika makaburi ya Kinondoni.
Mwananchi