Bi Kidude Kukumbukwa Unguja na Dar
FILAMU ya maisha ya Bi Kidude inatarajiwa kuzinduliwa Aprili 16 visiwani Zanzibar katika Ukumbi wa ZanCinema mjini Unguja.
Filamu hiyo pia itazinduliwa Dar es Salaam Aprili 19 mwaka huu.
Mwandaaji na mtayarishaji wa filamu hiyo, Andu Jones, alisema filamu hiyo itabeba ujumbe kuhusu maisha ya bibi huyo na kueleza kifo chake ikiwa katika lugha ya Kiswahili.
“Bi Kidude alikuwa msanii maarufu hapa nchini na dunia nzima kwa ujumla hivyo kila mtu anataka kujua na kusikia nini kimefanyika katika maisha yake,” alisema.
Naye Mkurugenzi wa Tamasha la Sauti za Busara, Yusufu Mahmoud, alisema Bi Kidude alikuwa akipokea 10% ya faida kutokana na mauzo ya kazi zake hivyo watayarishaji hao wapeleke sehemu hiyo ya faida kwenye Chuo cha Mafunzo ya Muziki wa Nchi za Jahazi kilichopo Mji Mkongwe ili kusaidia kuwaendeleza wanamuziki wa kike wanaosoma pale.
“Wakati huu ambao Zanzibar inasonga mbele, ni vyema kuwakumbuka mashujaa waliopita na kupeleka utamaduni wa Mzanzibari kwa watu wengine duniani,” alisema Mahmoud.
Mtanzania